ZFA yamng’oa Bushiri Stars
December 20, 2007
KOCHA Msaidizi wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Ali Bushiri, ameng’olewa katika nafasi hiyo, na nafasi yake kutwaliwa na Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, Abdulghan Msoma. Hayo yalisemwa jana na Makamu wa Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Al Hajj Haji Ameir, muda mfupi baada ya kuupokea msafara wa Zanzibar Heroes katika Bandari ya Zanzibar, ukitokea jijini Dar es Salaam.
Ameir alisema, hiyo ni kutokana na kiwango bora kilichoonyeshwa na Zanzibar Heroes iliyokuwa chini ya Msoma, hivyo wanaamini anaweza kuwa msaada mkubwa kwa Stars.
Kiongozi huyo amesihi kuwa, uamuzi huo unapaswa kuheshimiwa na wadau wa soka wa Bara na Visiwani kwa sababu unalenga ufanisi wa Stars katika michuano ya kimataifa.
“Msoma ni kocha mwenye uwezo mkubwa na kila mmoja amejionea kiwango kilichoonyeshwa na Zanzibar Heroes katika Chalenji, hivyo kwa kushirikiana na Maximo, Stars itafika mbali,” alisema na kuongeza:
“Hivyo, natangaza rasmi kumuondoa Bushiri katika timu ya Stars kuanzia leo (jana) na nafasi yake itazibwa na Abdulghan Msoma,” alisema Ameir ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kuimarisha Taifa Stars.
Aidha, uamuzi huo wa ZFA huenda ukazua mjadala kwani hoja hiyo iliwahi kuibuka, lakini ikazimwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na kuungwa mkono na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Msafara wa Zanzibar Heroes jana uliwasili Visiwani hapa saa 7 mchana kwa boti ya Sea Star na kupokewa na Makamu wa Rais wa ZFA, Haji Ameir, Katibu Mtendaji, Mzee Zam Ali na Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Wilaya ya Mjini, Nassor Salum Al Jazeera.
Wachezaji wa timu hiyo walikabidhiwa kitita cha sh mil 1.1 zilizotolewa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mahmoud Thabit Kombo.
KUTOKA: TANZANIA DAIMA
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

