Yanga yatakata kwa Ashanti Utd

January 27, 2008

YANGA, jana iliianza vizuri ngwe ya pili ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuifunga Ashanti United mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Kwa ushindi huo, mbali ya kufikisha pointi 24, pia Yanga imefanikiwa kulipa kisasi cha kufungwa 1-0 katika mechi ya ufunguzi wa ligi hiyo, Septemba 22, mwaka jana.

Safari hii ikiwa chini ya kocha Mserbia, Dusan Kondic, Yanga ilionyesha uhai mkubwa katika dakika 20 za mwanzo kabla ya Ashanti nao kuzinduka.

Yanga walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Abuu Ramadhan kufuatia mpira uliotokana na kona iliyochongwa na Abuu Mtiro katika dakika ya 20.

Bao hilo lilionekana kuwaamsha vijana wa Ashanti waliofanya mashambulizi kadhaa na katika dakika ya 33, walipata bao la kusawazisha.

Bao hilo, lilifungwa na Seleman Kibuta baada ya kupokea pasi maridadi kutoka kwa Said Omar kutoka wingi ya kulia.

Kabla ya kufungwa kwa bao hilo, kiungo wa Yanga, Athumani Idd aligongana na beki John Mabula wa Ashanti na kupasuka juu ya jicho.

Licha ya Idd kukabiliwa na maumivu, alilazimika kucheza hadi mwisho kwani Yanga ilishamaliza wachezaji wa kubadili.

Aidha, kutokana na kiwango bora alichokionyesha, mashabiki walipinga kutolewa kwa nyota huyo.

Mbali ya Idd, mchezaji Hashim Kaongo wa Ashanti, naye aliumia na kupoteza fahamu hata kukimbizwa hospitalini.

Baada ya hapo, kila timu ilifanya mashambulizi, lakini hadi mwamuzi Kenedy Mapunda wa Dar es Salaam akipuliza filimbi ya mapumziko, timu hizo zilikuwa 1-1.

Katika kipindi cha pili, Yanga ilifanya mabadiliko kwa kumuingiza Jerry Tegete badala ya Abuu Ramadhan.

Mabadiliko hayo yaliinufaisha kwani, katika dakika ya 62, Tegete aliwainua mashabiki wa Yanga kwa kuifungia timu yake bao la pili.

Alifunga bao hilo baada ya shambulizi kali langoni mwa Ashanti na kutokea piga nikupige.

Hadi mwisho wa mechi, Yanga ndiyo iliyotoka kifua mbele kwa mabao 2-1, hivyo kufikisha pointi 24.

Naye Ramadhan Siwayombe, anaripoti kutoka Arusha kuwa, timu ya JKT Ruvu, jana ilivuna pointi tatu baada ya kuifunga Polisi Dodoma 2-1.

Polisi walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 28 likifungwa na John Kanakamfumo.

JKT Ruvu iliyo chini ya Fredy Felix Minziro, walisawazisha bao hilo katika dakika ya 66, likifungwa na Bakar Kondo kabla ya Hussein Bunu kupiga la pili katika dakika ya 73.


Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post
 |  TrackBack URI for this post

Comments

Got something to say?