Ya Kiteto ni majuto dhidi ya ukombozi na uhuru mpya
February 27, 2008
MWAKA 1992, Idara ya Utawala na Sayansi ya Siasa ya Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilikuwa na mfululizo wa mijadala ya kisiasa. Wakati huo ndiyo kwanza mfumo wa vyama vingi ulikuwa umerejea nchini. Wenyeviti wa vyama vilivyokuwa vimepata usajili walikuwa wamealikwa kwa ajili ya kueleza sera za vyama vyao. Kwa kifupi mijadala hiyo ilikuwa yenye kutia hamasa hasa kutokana na wazungumzaji wengi waliofika kuwakilisha vyama vyao kuwa na upeo mkubwa wa kuzungumza.
Miongoni mwa watu waliofika kuzungumza walikuwa ni pamoja na James Mapalala (Mwenyekiti wa Chama cha Watu); Mabere Marando (Mwenyekiti NCCR-Mageuzi); Emmanuel Makaidi (Mwenyekiti wa NLD); Christopher Mtikila (Mwenyekiti wa DP); Kingunge Ngomale-Mwiru (kutoka CCM akiwa ni Katibu wa Itikadi na Uenezi); pia walifika viongozi wengine.
Kulingana na hali ya mambo ilivyokuwa eneo la Mlimani la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati huo, kiongozi aliyeonekena kuwa na wakati mgumu zaidi katika kujibu na kutosheleza kiu ya wasikilizaji, alikuwa ni Kingunge. Si kwa sababu Kingunge hajui kusema au alikuwa hana hoja, la hasha! Kwa sababu CCM kilikuwa ni chama ambacho kimepimwa na wananchi, ili kudhihirika kama kinaweza kuibadili nchi kwa sera zake au la.
Nakumbuka swali mojawapo ambalo Kingunge aliulizwa na mmoja wa washiriki wa mijadala hiyo lilikuwa linasema; nini kinakupa ujasiri wa kusimama hapa na kutetea sera za CCM wakati ukijua kwamba imeshindwa kuongoza nchi hii; hali ya umaskini ni kama unavyoijua, maradhi yanayotibika yanazidi kuua watu wetu na kwa ujumla badala ya kusonga mbele kwenye maendeleo kama taifa tunarudi nyuma?
Kingunge alizungumza akiwa mtulivu. Alijaribu kugusia mambo mbalimbali ambayo Tanu na hatimaye CCM wamefanya kwa mafanikio makubwa. Hata hivyo alipomaliza kuzungumza na kukaa chini, Mwenyekiti wa mjadala huo siku hiyo, Dk. Rwekaza Mukandala (Sasa Profesa na Makamu Mkuu wa chuo), alimuuliza, unaweza vipi kutetea sera hizi wakati zimethibitika kushindwa kuzaa matunda yaliyokusudiwa?
Alimtajia azimio la Arusha na siasa ya ujamaa na kujitegemea jinsi vilivyoshindwa, siasa ni kilimo, kilimo cha kufa na kupona na mikakati mingineyo.
Lakini Kingunge alisimama na kusema, maendeleo haya yanayoonekana ndiyo mafanikio ya siasa hizo. Chochote kidogo kilichopo ni matunda ya CCM. Kwa hakika majibu ya Kingunge yalikuwa marahisi kwa maswali magumu. Kwamba kwake sera za CCM hazijashindwa bali zimefanikiwa kwa kiwango cha kuwa na wanafunzi chuo kikuu akiwamo mwendesha mjadala.
Kumbukumbu za hali hii zilinijia juzi baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiteteo ambako mgombea wa CCM, Benedict ole Nangoro ameshinda na kumwacha kwa mbali mgombea wa Chadema, Victor Kimesera, aliyekuwa akiungwa mkono na vyama vitatu vya siasa – CUF, TLP na NCCR. Nangoro amepata kura 21,506 kati ya kura halali 34,477. Kimesera alipata kura 12,561.
Kwamba katika hali ya kushindwa kwa CCM kutawala nchi hii inaweza kuwa na ujasiri wa kuomba kura kwa wananchi wa kawaida? Je, katika hali ya njaa, ukosefu wa ajira, tuhuma za ufisadi kila mahali na kushindwa kwa chama tawala kutekeleza ilani yake ya uchaguzi, hivi wananchi wanaweza kupiga kura kwa chama hicho katika hali hii kweli?
Hakuna asiyejua sasa kwamba taifa hili lipo katika mkesha wa baa la ufisadi. Ufisadi kila mahali, wakubwa wamejineemesha kwa kodi za wananchi, serikali imesambaratika. Kwamba CCM inanuka rushwa inayoitafuna serikali yake si jambo la kujiuliza tena, lakini swali linarudi pale pale, kwamba wananchi wa Kiteto wamepata wapi ujasiri wa kuipa CCM kura?
Je, wananchi wa Kiteto wanafurahishwa na ufisadi; je, wananchi wa Kiteto hawana uchungu na nchi yao? Au hawajui kinachotokea katika taifa hili?
Yupo mwananchi mmoja alipata kusema hadharani kwamba kinachoiponza Tanzania isisonge mbele ni upole wa watu wake ambao aliuita ukondoo.
Leo nasema kwamba hali ya ukondoo ya kukataa kutambua kwamba shida zetu zinasababishwa na watawala walafi, wanaokula na kusaza bila kujali kwamba wapo mamilioni ya Watanzania waliopoteza matumaini ya kuishi; ndiyo chimbuko la kuzidi kudumaa kiuchumi kwa taifa hili.
Tanzania ina takriban watu milioni 40 sasa, lakini katika kundi hili, si watu milioni tatu wanaweza kusimama hadharani na kutetea haki zao. Kiteto iko Manyara, ni kati ya wilaya za wafugaji kama ilivyo Monduli na Ngorongoro kwa Mkoa wa Arusha.
Kiteto hakuna maji, hakuna majosho ya kutosha kwa ajili ya wafugaji; Kiteto ukisimama kokote utaona umaskini wa wananchi kwa macho.
Lakini pamoja na hali hiyo na bila kujali taarifa za sasa hivi ambazo zinaonyesha jinsi wakubwa wanavyopora mali ya umma, wamethubutu kupiga kura kwa mgombea wa CCM.
Kama alivyoulizwa Kingunge kwenye Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1992, kwamba anapata wapi ujasiri wa kusimama hadharani na kutetea sera za CCM zilizoshindwa kuzaa matunda, leo naazima maneno ya muhadhiri yule aliyeuliza swali hilo na sasa nawauliza wananchi wa Kiteto wamepata wapi ujasiri wa kuchagua mgombea wa CCM?
Mgombea wa chama kilichojaa mafisadi; mgombea wa chama kilichoshindwa kuongoza taifa; mgombea wa chama ambacho serikali yake imeangushwa kwa ufisadi?
Maswali haya ni msingi wa kutambua kwamba CCM pamoja na kujua udhaifu wake, kwamba imeshindwa kuleta maendeleo ya kweli kwa taifa hili kwa miaka yote hii, na kwamba hata kama serikali yake ikiwa inanuka rushwa, inakuwa haina wasiwasi kwa sababu wananchi walio wengi hawajijui. Hawajui haki zao, hawajui kama wana njia ya kuiadabisha hata kama wataendeleza rushwa.
Yaliyotokea Kiteto ni majuto kwa wote wanaoitakia nchi hii mema, lakini ni kicheko kwa mafisadi, ni kicheko kwa walaji wa mali ya umma, ni kicheko kwa sababu kitakachoendelea ni business as usual.
Ujasiri wa wananchi wa Kiteto ni ujasiri wa mtu anayejitafuna mwenyewe; ni ujasiri wa kukataa ukombozi.
Ni ujasiri wa kukubali kukandamizwa na ni ujasiri unaostahili kulaaniwa na kuzomewa kwa sababu unazima vuguvugu jipya la kujikomboa na kukomboa rasilimali zetu ambazo kwa miaka takriban 47 zimetafunwa na mafisadi. Ya Kiteto ni majuto kwa ukombozi na uhuru mpya.
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

