Wauza mafuta waanza mgomo Dar
January 13, 2009
HALI ya upatikanaji wa mafuta jijini Dar es Salaam, hasa Petroli, inazidi kuwa mbaya kutokana na vituo vingi kutouza bidhaa hiyo kwa kile kinachoonekana kuwa, ni njama za waziwazi za wafanyabiashara ya mafuta kuikwamisha serikali kudhibiti upandaji holela wa bei ya nishati hiyo.
Lakini Wizara ya Madini na Nishati imesema inasubiri kupata taarifa kutoka kwa watendaji leo asubuhi, kabla ya kuanza kuchukua hatua kwa wote waliokiuka sheria iliyotangazwa kwenye Gazeti la Serikali kuhusu bei elekezi za mafuta, kwa mujibu wa naibu waziri kwenye wizara hiyo, Adam Malima.
Mafuta ya dizeli ndiyo yanayopatikana bila ya shida kwenye vituo vingi na inauzwa kwa bei iliyotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
Katika kile kinachoonyesha kutii agizo la Ewura, vituo hivyo vilivyokuwa vikiuza dizeli pekee, vimeweka mabango yanayoonyesha kuwa petroli inauzwa kwa bei ya Sh1,233 ikikaribiana na ya Ewura, ingawa inakuwa haiuzwi.
Hayo yametokea wakati Ewura imetangaza bei mpya ya nishati hizo kwa mikoa 21 ya bara, ikiwa imeongeza senti kadhaa kwenye bei ya awali.
Mgomo huo baridi ulisababisha vituo vichache vilivyokuwa vikiuza petroli kwa bei ya Ewura kufurika magari mengi na watu wenye madumu kwa ajili ya kununua petroli ya ziada, katika wiki ambayo bei ya mafuta katika soko la dunia imezidi kuporomoka na kufikia chini ya dola 39 kwa pipa.
Ewura imewataka wauzaji wa bidhaa hiyo kuuza petroli kwa Sh1,166 kwa lita, ingawa vituo vinavyouza bidhaa hiyo vimekuwa vikiuza kwa Sh1,233 kwa lita, tofauti na bei ambayo ilikuwa ikitumiwa awali na wafanyabiashara hao ambayo ilikuwa kati ya Sh1,450 na Sh1,600 kwa lita ya petroli.
Ewura pia imetaka dizeli iuzwe kwa Sh1,271 kwa lita na karibu vituo vyote vilikuwa vinauzwa nishati hiyo kwa bei inayolingana na ya mamlaka hiyo, yaani kati ya Sh1,280 na Sh1,300 kwa lita huku vingine vikidiriki kuuza hata kwa Sh1,180 kwa lita.
Ewura imeeleza kuwa, imeshawasilisha bei hizo mpya kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili atangaze kwenye Gazeti la Serikali na kuanzia hapo yeyote atakayekiuka bei hiyo atakabiliwa na adhabu ya faini ya Sh3 milioni au kunyang’anywa leseni au adhabu zote mbili kwa wakati mmoja.
Ewura pia ilisema bei mpya ilitakiwa kuanza Jumatatu iliyopita na kwamba, wale ambao wamekiuka tangu kipindi hicho, sheria itawakumba mara tu Mwanasheria Mkuu atakapotangaza bei hizo kwenye Gazeti la Serikali.
Katika kipindi cha kuelekea Krismasi, petroli ilipanda ghafla na kufikia hadi Sh1,800 na wauzaji walisingizia kuwa hiyo ilitokana na shehena walizokuwa wakitegemea kushindwa kufika kwa wakati kutokana na meli zilizobeba mafuta hayo, kuhofia kupita pwani ya Somalia ambayo ina maharamia wanaoendelea kuteka meli za mizigo na kudai donge nono ili waziachie.
Lakini umoja wa waagizaji wa mafuta, ulipingana na maelezo hayo ukidai kuwa mafuta yaliyo kwenye akiba yangeweza kutosheleza nchi kwa kipindi cha mwezi mmoja kabla ya shehena nyingine kuingia.
Jana Ewura ilitangaza bei mpya za mafuta zitakazotumiwa kuanzia Januari 13. Kwa mujibu wa bei hizo, jijini Dar es salaam, petroli itauzwa kati ya Sh1,171 na Sh1,259 kwa lita, wakati dizeli itauzwa kati ya Sh1,301 na Sh1,390 kwa lita.
Katika mikoa mingine, petroli itauzwa kati ya Sh1,201 kwa bei ya chini kabisa wilayani Kibaha, hadi Sh1,535 kwa bei ya juu kabisa katika mkoa wa Kagera, wakati dizeli katika mikoa hiyo itauzwa kati ya Sh1,339 kwa bei ya chini kabisa mkoani Morogoro na Sh1,693 kwa lita, ikiwa ni bei ya juu kabisa katika mkoa wa Singida.
Bei ya mafuta ya taa Wakazi wengi wa Dar es Salaam walioongea na Mwananchi, walielezea kuwa tatizo hilo ni mgomo uliopangwa na wafanyabiashara hao kama njia ya kukwamisha mkakati wa serikali wa kudhibiti bei ya mafuta.
“Hakuna kitu kingine ni ujanja tu wa kuikomoa serikali,” alisema mkazi wa Dar es Salaam, Jeseph Nkele ambaye alikuwa kwenye foleni ya petroli katika kituo cha Oilcom, Mlalakuwa, Mwenge.
“Kama serikali ina uwezo wa kuwabana kweli na tuone makali yao.” “Suala la mafuta sasa hivi limeshakuwa kero, kwa kuwa vituo vingi vimegoma kuuza… vinadai kuwa mafuta yameisha, wakati yapo kwenye akiba zao na ndio maana umetuona tumesongamana katika kituo kimoja kwa kuwa ndicho kinachotoa huduma katika maeneo haya,” alisema Juma Abdalah ambaye ni dereva wa daladala kati ya Mwenge na Kariakoo.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, wanaiomba serikali kuchukua hatua kali kwa wale waliokaidi na wanaogoma kuuza mafuta hayo kwa madai ya kukataa kupunguza bei.
Naye dereva mwingine wa daladala anayehudumia kati ya Mwenge na Tegeta, Yusuph Khamis alisema kuwa vituo vinavyouza mafuta katika maeneo hayo ni vichache ukilinganisha na wingi wa vituo.
“Kuna vituo vingi sana vya kuuza mafuta katika maeneo haya, lakini mpaka sasa vinavyotoa huduma ni vichache ambavyo viko Tangi Bovu na Africana. Vilivyobaki vyote vimegoma, na ukienda wanakwambia mafuta yameisha. Hili ni tatizo. Lazima serikali ichukue hatua kali kukomesha hali hii,” alisema Khamis.
Habari hii imeandaliwa na Leon Bahati, Patricia Kimelemeta na Benton Nolo wa Mwananchi
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

