Watatu TMK Wanaume Halisi kuzindua Z’bar
December 21, 2007
WASANII watatu wa kundi la muziki wa kizazi kipya la TMK Wanaume Halisi, wanatarajia kuzindua albamu zao katika shoo tofauti za kundi hilo zinazotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu Zanzibar, imefahamika. Wasanii hao ambao wamepania kuuwasha moto usiozimika kisiwani humo katika shoo zao tofauti ikiwamo ya siku ya mkesha wa mwaka mpya itakayofanyika katika ukumbi wa Ngome Kongwe ni pamoja na ndugu wawili, Baraka Sekela ‘BK’ na Noweli Sekela ‘Bob Q’ watakaozindua albamu yao ya ‘Kwa maisha’ na Francis Moses ‘Dolo’ akiwa na albamu yake ya ‘Kuishi na watu’.
Akizungumza na Tanzania Daima, mmoja wa wasanii hao, BK, alisema kuwa wanawaomba wapenzi na mashabiki wa fani hiyo kujitokeza kwa wingi ili kushuhudia kile walichoandaliwa.
“Hii ni albamu yetu ya kwanza kuzindua mimi na Bob Q, hivyo tumepanga kuwapagawisha mashabiki wetu katika kila wimbo na staili tutakazotumia jukwaani,” alisema.
Albamu hiyo ya ndugu hao wawili ina jumla ya nyimbo kumi huku Dolo albamu yake ikiwa na nyimbo nane, ambazo ni kwa mara ya kwanza zinakwenda kuzinduliwa kisiwani humo kabla ya kuja kuzinduliwa hapa jijini mapema mwakani.
Kundi hilo linatarajiwa kuondoka mwishoni mwa mwezi huu na kurejea Januari mwakani.
KUTOKA: TANZANIA

