Wasanii wa Bongo wanavyokamuliwa

April 4, 2008

WASANII wa Tanzania wamekuwa wakilia kilio cha samaki. Machozi yao yanaishia bahari ya ukimya na dharau.

Hakuna anayewajibu. Chombo kilichopo sasa - Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), na ambako wangekimbilia, kinaonekana kuwa na malengo ya kuwanyonya wasanii na si kuwasaidia. Maisha ya wasanii wenye majina hayafanani na hadhi waliyo nayo.

Utashangaa kuona msanii maarufu, mwenye kazi ambazo zinavuma sana katika vituo vya televisheni na redio, anakuomba nauli ya daladala. Sawa!

Wapo wachache waliofanikiwa, lakini wengi ‘wamepigika’. Inasikitisha. Inatia simanzi. Na kauli za viongozi wa Basata zinadhihirisha Baraza halifanyi lolote kuinua wasanii.Bunge lilikaa na kutunga sheria.

Sheria hiyo iliwezesha kuundwa kwa Basata kwa maslahi ya wasanii. Lakini hivi sasa nia na madhumuni vimebadilika. Basata imekuwa kama kijiwe cha kukusanya wakipatacho wasanii, bila ya kuwaangalia wasanii hawa watawezaje kunyanyua mguu na kupiga hatua mbele.

Ukiangalia maisha ya wasanii wa nchi nyingine utagundua ukweli wa ninachosema. Natamka kauli hii pasipo kuogopa kuwa sisi tuna “wanyonyaji.”

Hili nalizungumza kwa maana moja pana. Viongozi wa Basata hawaangalii ni jinsi gani wataweza kumsaidia msanii. Wakikaa katika vikao vyao, wanachokijadili ni jinsi gani watambana msanii ili aweze kulipa ada ya leseni kila mwaka.

Mtu makini angetaka kujua, kwa nini wasijadili ni jinsi gani watamsaidia msanii wa Tanzania ili naye aweze kuboresha kipaji chake na kuliletea sifa taifa letu?

Hili wamelifumbia macho na kulizibia masikio huku wakiandaa mikakati ya kuwabana wasanii maskini kujiandikisha na kulipa ada za leseni. Huu ni ukupe!

Kilichonisikitisha ni kauli ya Mwenyekiti wa Basata, Frowin Nyoni, mwaka jana, pale alipotamka wazi, tena bila woga kile alichodai ni kiasi cha fedha “wanachokipoteza kwa mwaka kwa wasanii kutolipa ada za leseni.”

Basata wanasema kuwa milango yao iko wazi na wanawataka wasanii waende wakaulize ni “wapi watakapopata haki zao.”

Je, kazi ya Baraza hili ni ipi? Mbona kwenye suala la fedha Baraza linasema litawabana wasanii, lakini kwa kuwasaidia au kuwawezesha linasema litawaelekeza wapi pa kupata haki zao?

Nijuavyo mimi ni kwamba Baraza lina jukumu la kukuza sanaa. Kukuza sanaa ni kutambua wasanii na sanaa zao na kuwawezesha wahusika ili kuboresha sanaa.

Hili ndilo linaendana na kuwasaidia.Sasa Nyoni atueleze, ni chombo gani kiwasaidie wasanii kama siyo Basata?

Na kama Basata haiwezi kufanya kazi hiyo, kwa nini isivunjwe, maana imekosa kazi?Inasikitisha kumsikia Nyoni akisema yafuatayo, “Kutokana na tathmini ambayo tumeifanya imegundulika kuwa tunakosa fedha nyingi kwa mwaka. “Endapo mikakati mizuri itapangwa tutaweza kuwa wakusanyaji wazuri kama Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA).”

Hii ilikuwa ni katika mojawapo ya vikao vya hivi karibuni vya wafanyakazi wa Basata. Hapa ndipo nashindwa kuelewa kama nchi hii ni ya Watanzania wote au baadhi.

Ni hivi: Basata wanakaa chini. Wanaunda mikakati ya kukusanya fedha kutoka kwa wasanii lakini baya zaidi ni kwamba fedha hizo hazinufaishi wasanii.

Ukweli ni kwamba sanaa ni kitu muhimu, bali wahusika wamekaa kimya. Lakini wakiongea, ni juu ya kuandaa mikakati ya kuwabana wasanii wasiojiweza.

Nyoni anasema, “Tungekuwa mamilionea…ila wasanii wengi ni wajanja, pamoja na wauzaji wa kazi zao, lakini tutahakikisha tunawabana waje kujisajili Basata.”

Kauli hizi zinalenga kumsaidia vipi msanii? Kwani wasanii wenyewe wanasema hawajui pa kukimbilia kwa kuwa baraza linawakana.Mwaka jana nilizungumza na mwimbaji Rogati Anatory, maarufu kwa jina la Rogati Katapila. Kilio chake kilikuwa ni juu ya Basata.

Joan Matovyolwa, mwimbaji na mwigizaji. Kilio chake kilikuwa juu ya Basata kushindwa kuwasaidia kuondokana na umaskini waliomo.

Sikuacha kukutana na Charles Gabriel, maarufu kwa jina la Charls Baba.

Ni kilio hicho hicho, “Nani atawasaidia wasanii wa Tanzania kukuza vipaji vyao.” Orodha ni ndefu.

Nimekutana na Peter Simalenga, maarufu kwa jina la Dimera. Analilia wasanii kutoendelea na kukosekana kwa chombo cha kuwainua.

Rehema Hamis Tajiri hana tofauti na wasanii wenzake.

Katika mahojiano nami pia mwaka jana, anarejea kilio cha wengi cha kukosekana mwezeshaji anayejali vipaji vya wasanii.

Hapa kuna Kalala Junior, Ramadhani Mkonde, maarufu kwa jina la Taff, Deo Mwanambilimbi na mkongwe wa taarab, Khadija Omar Kopa. Wote hawa wamerekodiwa katika mahojiano maalum wakililia umuhimu wa kuwa na chombo, siyo cha kukamua wasanii, bali cha kutumia mapato kutoka kwa wasanii kuendeleza wasanii wenyewe.

Wengi niliohojiana nao walipendekeza Basata ya sasa ivunjwe, kwa maana ya kuondoa viongozi waliopo na kuweka wale wanaotoka miongoni mwa wasanii.

Walitoa mifano mingi, mmojawapo ukiwa Baraza la Habari Tanzania (BHT), wakieleza kuwa wanahabari ndio walipigania kuundwa kwake na ni wao wanaoliongoza.

“Hivi kwa nini Basata lisiundwe na wasanii na kuendeshwa na wasanii wenyewe? Kama kuna sheria zinazozuia hivyo, basi wakati umefika zibadilishwe,” ameeleza mmoja wa wasanii.Viwango vya ada ya leseni vilivyotajwa ni sh 30,000 kwa kila msanii.

Makusanyo waliyokadiria kukusanya kwa mwaka jana ni sh bilioni moja (1,000,000,000) kwa mwaka kutoka kwa wasanii milioni sita nchini.

Hakika Basata ni wataalamu wa kukusanya takwimu za watu wa kukamua, lakini siyo wa kutafuta jinsi ya kuinua vipaji vya wasanii.

Hivi kwa nini kusiwe na mfuko wa kuwezesha wasanii huku Basata wakijiwekea malengo ya kukusanya baada ya wasanii hawa kufaidika? Lakini kama kazi pekee ya Basata sasa imebakia kuwa ukusanyaji kodi, basi jukumu hilo waachiwe TRA.

Imeandikwa na: George Kyatika na kutolewa katika gazeti la Tanzania Daima la April 4, 2008