Wangwe: RC Mara anachochea vita
November 26, 2007
MBUNGE wa Tarime, Chacha Wangwe (CHADEMA), amelaani vurugu zilizotokea juzi wilayani Tarime baada ya Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Issa Machibya kuharibu njia za mpakani kwa lengo la kuzuia wafanyabiashara wa samaki.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Wangwe alisema chanzo cha vurugu hizo ni kitendo cha RC huyo kuwazuia wafanyabiashara kuuza bidhaa zao nchi jirani ya Kenya.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, taarifa za vurugu jimboni kwake alizipata kutoka kwa wananchi anaowaamini na baadhi ya viongozi wa chama hicho mkoani Mara.
Alisema kuwa, Kanali Machibya aliingia nchini Kenya kupitia kijiji cha Kumumwamu na kwenda kuwakamata wafanyabishara wa dagaa hali iliyosababisha vurugu.
Wangwe alisema, ushahidi wa matukio hayo anao katika picha alizotumiwa na watu anaodai kuwaamini zaidi na kwamba busara za Mbunge wa Kenya ambaye hata hivyo hakumtaja jina lake, zilisaidia kutuliza vurugu hizo.
Alisema wakazi wengi wa Tarime ni wafanyabiashara kati ya Kenya na Tanzania kutokana na ukweli kwamba wamekosa kazi ndani ya migodi inayozunguka maeneo yao.
Wangwe alisema, nia mbaya ya Kanali Machibya inakwamisha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuathiri safari za wanafunzi wanaosoma Kenya.
“Nadhani huu ni mpango wa ‘kuwa-harass’ wakazi wa jimbo langu… tena kwa makusudi kabisa, pale kuna wafanyabiashara na wanafunzi wanaotegemea nchi jirani katika shughuli zao.
“Machibya, amechimba mashimo yapatayo futi 20 chini kwenye barabara za vijiji zinazounganisha Tanzania na Kenya, wakazi wangu wanapata shida sana,” alisema Wangwe.
Aidha, mbunge huyo aliiomba serikali kumchukulia hatua za kisheria mkuu huyo wa Mkoa wa Mara kwa vile amechochea vita na kuhatarisha amani.
“Amani ya wakazi wa Tarime haina uhakika kutokana na vurugu zinachochochewa na Kanali Machibya… naiomba serikali kumchukulia hatua za kisheria RC huyu,” alisisitiza Wangwe.
Imeandikwa na Irene Mark wa Tanzania Daima

