Waislamu washauriwa kuondoa tofauti zao
December 21, 2007
RAIS Jakaya Kikwete ameyataka makundi ya waumini wa dini ya Kiislamu nchini yanayotofautiana katika siku za kusali Iddi kukutana na kumaliza tofauti zao.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo alipokuwa akitoa salamu za Idd katika Baraza la Idd lililotanguliwa na sala ya Iddi El Hajj kitaifa, katika msikiti wa Al-Farouq, ulioko Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), jijini Dar es Salaam jana.
Alisema hafurahishwi kuona waumini wa Kiislamu nchini wakiendelea kutofautiana katika suala hilo, wakati tofauti hizo ambazo zimekuwa zikiwagawa kwa muda mrefu kila inapofikia kipindi cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na siku ya kusali Iddi, zinazungumzika.
“Hatuishiwi na tofauti za mwandamo wa mwezi na siku ya kusali Iddi. Ombi langu ni kwamba kaeni chini yazungumzeni. Inasikitisha kuona hata yasiyostahili mnatofautiana. Tatizo ni kwamba hamtaki kukaa pamoja,” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema hawezi kuitisha kikao cha mazungumzo hayo kwa kuwa hilo halimo katika majukumu yake na kwamba wanaopaswa kufanya hivyo ni viongozi wa Kiislamu pekee.
“Mimi si Sheikh ni mwanasiasa. Kama CUF na CCM wanatofautiana, ndiyo ninaweza kuitisha kikao ili wamalize tofauti zao. Hivyo, mkae myazungumze,” alisema Rais Kikwete katika baraza hilo lililoongozwa na Naibu Mufti, Sheikh Abubakar Zubeir na Katibu wa Mufti, Sheikh Abdushakur Omar.
Alisema tofauti za dini haziwezi kuwa sababu ya Watanzania kufarakana na kuonya kuwa jambo hilo ni hatari kwa kuwa linawafanya watu waishi kwa kuwindana, badala ya kuishi kwa amani, upendo na mshikamano.
Aliwataka masheikh kuongoza vizuri na kuacha kugombana baina yao, akisema kuwa kitendo hicho ni kibaya zaidi kwa kuwa mbali ya kuwatia misukosuko waumini, pia yanachangia kuufedhehesha uislamu.
“Wanapogombana masheikh ndiyo inakuwa tatizo zaidi. Kwa kuwa mnachokifanya ni kuufedhehesha uislamu. Ongozeni vizuri, msitafute umaarufu kwa kuwatia misukosuko waumini,” alisema.
Alisema mahujaji wa Tanzania waliokwenda nchini Saudi Arabia kutekeleza ibada ya Hijja mwaka huu, wako salama na kwamba, hakuna taarifa zozote za maafa zilizokwishatangazwa kuwatokea kama ambavyo imekuwa ikitokea miaka iliyopita.
Aliwataka Waislamu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwajalia mahujaji hao kutekeleza salama ibada hiyo licha ya safari yao kutoka nchini kwenda Makka, kukumbwa na misukosuko.
“Safari yao (mahujaji) ilikuwa na misukosuko na maneno yakawa mengi na wanasiasa tukaingia humo humo. Lakini wakasafiri. La kuomba, warejee salama na yaliyotokea yawe fundisho na yasitokee tena,” alisema Rais Kikwete.
Alisema Shirika la Ndege Tanzania (ATC) ambalo kwa muda mrefu halikuwa na ndege na badala yake likategemea ndege mbovu ya Kampuni ya Ras-Alkhaima ya Saudia kusafirisha mahujaji hao, mwakani litakuwa na ndege zake.
“Mwaka huu (ATC) walikuwa wakala tu, walitegemea ndege ya Ras-Alkhaima lakini ikawa mbovu. Namshukuru Waziri Mkuu, Waziri (Andrew) Chenge na viongozi wa ATC kwa kuhakikisha kuwa mahujaji wanasafiri,” alisema na kuzitaka mamlaka zinazohusika kuhakikisha kuwa zinaandaa mapema safari za mahujaji.
“Mambo ya zimamoto ndiyo yanayotufikisha hapa. Hilo si jambo la dharura ni jambo ambalo maandalizi yake yana muda wa miezi sita,” alisema rais na kuwataka Waislamu kuiombea nchi amani na utulivu.
Aliwataka Waislamu kuomba ili matatizo yaliyopo hivi sasa, ikiwamo kutonyesha mvua za vuli katika maeneo kadhaa nchini.
“Pamoja na matatizo kuwa madogo, lakini mvua za vuli zinatia wasiwasi. Maeneo yaliyotarajiwa mvua hakuna, hivyo tuombe mvua za masika zisikosekane,” alisema Kikwete.
Aliipongeza Bakwata kwa kuanzisha kitengo cha kushughulikia masuala ya wanawake akisema kuwa anaamini kwamba kitasaidia kujenga uchumi na kujiendeleza katika maisha yao.
Awali, akitoa nasaha katika baraza hilo, Naibu Mufti, Sheikh Zubeir, aliwataka Waislamu kujenga utamaduni wa kumtii Mwenyezi Mungu, Mtume (S.A.W.) na wenye mamlaka ili kujenga mshikamano na kupata baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
“Matunda ya utii yanaenea katika jamii na hasara yake ni kusababisha mgawanyiko na baraka kupotea,” alisema Sheikh Zubeir.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Ali Mzee alimshukuru Rais Kikwete na serikali yake kwa kuhakikisha mahujaji waliokwama kwa siku zaidi ya kumi na moja katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wanaondoka, akisema kuwa jambo hilo si faraja tu kwa mahujaji bali pia limeliletea heshima taifa.
“Tunawashukuru mahujaji kwa uvumilivu. Mwenyezi Mungu awarejeshe salama nchini,” alisema Sheikh Mzee.
Hata hivyo, alisema Bakwata kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti wa Zanzibar, wameunda chombo maalum kijulikanacho kama Tanzania Hajj Mission kwa ajili ya kushughulikia suala hilo.
Alifahamisha kuwa chombo hicho kiko chini ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Issa bin Shaaban Simba (Mwenyekiti), Mufti wa Zanzibar, Khalid bin Khelef (Makamu Mwenyekiti), Rais akiwa ni Sheikh Abdulrazak na Makamu wake, Naibu Mufti, Sheikh Zubeir.
“Taasisi zote zitambue uwepo wa chombo hicho ili kurahisisha safari za mahujaji na kuwafanya wasafiri na kupata huduma zote zinazotakiwa,” alisema Sheikh Mzee.
Alisema Bakwata imeanzisha juhudi za kufufua ari ya wanawake kwa kuanzisha kitengo chao kilicho chini ya uongozi wa Aisha Sururu na Mbunge wa Kibaha Mjini, Dk Zainab Gama.
Naye Kaimu Sheikh wa Bakwata Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Ngeruko akisoma hotuba ya sala ya Iddi katika msikiti huo, alikemea vitendo vya umwagaji damu na kuharibu heshima za watu miongoni mwa waumini.
Sala hiyo iliyoongozwa na Naibu Mufti, Sheikh Zubeir, ilipambwa na Kur’ani Tukufu iliyosomwa na Mnajimu Maarufu wa Afrika Mashariki, Sheikh Yahya Hussein, Fat’ha iliyosomwa na Sheikh Hassan Kiburwa na tafsiri ya Kur’ani Tukufu illiyosomwa na Sheikh Alhad Mussa Salum.
KUTOKA: MWANANCHI

