Wabunge kujadili petroli
March 25, 2008
HATIMA ya mjadala wa wabunge juu ya Muswada wa Sheria ya Nishati ya Umeme na Biashara ya Mafuta itajulikana leo baada ya kufungwa kwa semina ya wabunge inayojadili muswada huo.
Mjadala huo ambao ulianza wiki iliyopita kwa wabunge wengi kuukataa muswada huo, hususan katika eneo la nishati ya umeme, wakisema unalenga kuliua Shirika la Umeme nchini (TANESCO), leo unatarajia kuendelea kwa kuangalia maendeleo na changamoto ya biashara ya mafuta ya petroli pamoja na mbinu za kuimarisha Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Baadhi ya wadadisi wa mambo wanauona mjadala huo kuwa changamoto kubwa kwa Waziri mpya wa Nishati na Madini, William Ngeleja, ambaye ndiye aliyeteuliwa kubeba dhamana hiyo tangu Rais Jakaya Kikwete alipounda upya Baraza la Mawaziri, Februari mwaka huu.
Kikubwa kinachotarajiwa kugusa maoni ya wabunge wengi kitakuwa hatua iliyofikiwa katika kuiwezesha TPDC kuanza kufanya biashara ya mafuta, lengo likiwa ni kuleta ushindani wa haki na kupunguza mzigo kwa watumiaji wa nishati hiyo, tangu uamuzi huo upitishwe bungeni mwaka 2006.
Aidha, mjadala huo utachagizwa zaidi na takwimu zilizotolewa na Wizara ya Nishati na Madini ambazo zinaeleza wazi kuwa, serikali haina akiba ya mafuta na yaliyopo hivi sasa ni ya biashara ambayo haizidi matumizi ya wiki mbili.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima tangu kuanza kwa semina hiyo Jumatano iliyopita unaonyesha kuwa baadhi ya wabunge wameonyesha dhamira yao ya kuhoji sababu za serikali kuifunga iliyokuwa Kampuni ya Kuagiza na Kusafisha Mafuta ghafi (TIPER) mwaka 2000.
Kwa mujibu wa mtazamo huo, baadhi ya wabunge kama ilivyo kwa baadhi ya wataalamu wa masuala ya nishati, wanaamini kuwa uamuzi wa kuifunga TIPER kwa kiwango kikubwa ulifikiwa kimakosa na ndiyo chachu kuu ya kupanda kwa kasi kwa bei ya mafuta ya petroli katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa mujibu wa wabunge hao, kuwepo kwa kampuni hiyo kwa kiasi kikubwa kulikuwa kukisaidia kushuka kwa bei ya nishati ya mafuta, hivyo kupunguza gharama za uzalishaji viwandani.
Wabunge hao wanaamini kwamba, kufungwa kwa kampuni hiyo kuliruhusu biashara ya mafuta ya petroli kuendeshwa kwa ushindani usiozingatia hali halisi, jambo lililowafanya waagizaji wajipangie bei licha ya serikali kuwaonya mara kwa mara bila ya mafanikio.
Mwaka jana, serikali iliagiza bei ya mafuta ya petroli isizidi sh 1,400, lakini hivi sasa mafuta hayo yanauzwa mpaka sh 1,600 kwa lita kulingana na matakwa ya muuzaji.
Moja ya mambo yanayotarajiwa kuibuka ni tabia ya baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kuchanganya mafuta ya petroli na vitu vingine, hali hiyo kuhatarisha mitambo na magari ya wananchi, huku Mamlaka ya Kudhibiti Nishati ya Mafuta na Maji (EWURA) ikishindwa kuonyesha meno yake kutokana na kukosa meno kisheria.
Kwa ujumla majadiliano ya kesho ndiyo yatakayotoa dira ya kule Tanzania inakoelekea katika nishati ya petroli pamoja na umeme, ambavyo siku za hivi karibuni bei yake imekuwa ikipanda mara kwa mara.
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

