Wabunge acheni kuingiza itikadi za kisiasa bungeni
January 29, 2008
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaanza kikato chake cha kwanza kwa mwaka huu leo mjini Dodoma. Katika kikao hicho wabunge watajadili mambo mbalimbali huku serikali ikipata nafasi ya kujibu maswali na hoja za wabunge kwa lengo la kuiendeleza nchi yetu kiuchumi na kijamii.
Kwa kawaida, katika vikao vya Bunge serikali huwasilisha miswada inayopendekezwa kuwa sheria, kupokea na kujadili hoja mbali mbali za wabunge pamoja na ripoti za kamati na tume za Bunge zilizopewa kazi maalumu.
Moja ya miswada itakayojadiliwa kwenye kikao cha sasa ni ule wa Ukimwi ambao unalenga kuweka sheria mpya kuhusu adhabu inayostahili kutolewa kwa watakaobainika kusambaza ugonjwa huo kwa makusudi.
Hata hivyo hoja inayotarajiwa kuvuta wengi ni mjadala wa Ripoti ya Kamati ya Richmond ambayo ilishakamilika na kukabidhwa kwa Spika wa Bunge, Samwel Sitta kwa ajili ya kutolewa bungeni.
Ripoti ya Richmond inasubiriwa kwa hamu si tu na wabunge bali hata wananchi wengi kufuatia utata wa zabuni na mkataba ulioihalalisha kampuni hiyo kuanzisha mradi wake wa kufua umeme.
Watanzania wanataka kujua kamati hiyo ambayo ilipewa kazi ya kuchunguza suala hilo ilipata nini na kama kuna udhaifu ni hatua gani zitakazochukuliwa au kama hakuna tatizo lolote ni nini kilisababisha mradi huo utiliwe mashaka.
Hamu ya watu wengi inachochewa zaidi na matokeo ya ripoti ya ukaguzi wa mahesabu ya Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT) ambayo ilibainisha kuwepo kwa ufisadi mkubwa wa fedha za umma, unafikia Sh133 bilioni.
Ripoti hiyo ilimfanya Rais Jakaya Kikwete kumwajibisha aliyekuwa Gavana wa BoT, Daudi Ballali kwa kumwachisha kazi au kukatisha mkataba wake wa kuiongoza benki hiyo ambao ulikuwa uishe Mei mwaka huu.
Tunaamini kuwa safari hii wabunge watakuwa makini katika kujadili hoja mbalimbali zinazotolewa bungeni tofauti na huko nyuma ambapo Bunge liligeuzwa kuwa jukwaa la kisiasa kwa kutanguliza mbele itikadi za vyama vyao vya siasa.
Ni kweli kwamba wabunge huchaguliwa na wananchi kupitia vyama vyao, lakini hilo halibadilishi maana ya Bunge na wabunge kwani lipo au wapo kwa ajili ya kuwatetea wananchi na maslahi ya taifa letu.
Hivyo basi tusingependa itikadi za kisiasa ziingizwe kishabikia katika kutoa maamuzi juu ya mambo muhimu yenye maslahi kwa wananchi wa Tanzania kwa ujumla.
Ushabiki wa kisiasa haulengi kuleta maendeleo na kulinda maslahi ya taifa kama ilivyotokea kwenye Kikao cha Bunge la Bajenti ambapo kambi yenye wabunge wengi ilizuia hoja za wapinzani kwamba hazina ukweli, lakini baadaye ndizo zilizofichua uozo ndani ya BoT.
Si hivyo tu, hoja ya kuunda kamati maalunu ya Bunge ya kupitia upya mikataba ya madini ambayo iliwasilishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe ikatupwa chini, lakini kutokana na uzito wake Rais Kikwete akaunda Tume chini ya uenyekiti wa Jaji Mark Bomani.
Hatua hiyo ni kama ilionyesha kuwa wabunge hawakufanya kazi yao inavyostahili, hivyo hatutarajii mambo kama hayo yatokee kwenye kikao hicho.
Bungeni ndiyo mahali pekee ambapo wananchi wanawasilisha hoja zao kupitia wabunge wao ili kwa pamoja, wananchi wa kutoka pande zote za Tanzania, waweze kuzijadili na kuzipatia ufumbuzi. Hivyo tunaomba wabunge wajitambue kwamba wako pale kama wananchi hivyo wajadili hoja za kujenga taifa letu na si itikadi za kisiasa.
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

