Waandishi wanaotetea watuhumiwa wa Richmond ni majasiri wa kifisadi

February 25, 2008

GEORGE Walker Bush katika siku nne za ziara yake kuanzia Februari 16, mwaka huu pamoja na mambo mengine aliweza kufunika mjadala kuhusu Richmond.

Siku nne za Bush Tanzania, pamoja na kuonekana kuitangaza nchi hii katika anga za kimataifa bado ziara yake imeweza kuwa gumzo kutokana na mambo mbalimbali ikiwemo kufungwa kwa barabra za miji aliyotembelea, kuingiliwa kwa mawasiliano ya simu na ulinzi mkali ambao hatukuwahi kuuona kwa viongozi wetu.

Binafsi, ni mmoja wa Watanzania kwa upande wa waandishi ambaye nilionja ugumu wa ziara hiyo lakini ikinifunza mengi makubwa, hasa jinsi ya kufanya kazi katika mazingira yenye ulinzi wa hali ya juu sawa na mazingira ya kivita.

Bush sasa ameondoka, ametuachia Sh 850 bilioni za MCC, vyandarua milioni tano na tumepata ahueni kuwa sasa Tanzania haitakuwa kituo kijeshi cha Marekani. Ni wakati sasa wa kuangalia gumzo letu la Richmond lililokuwa limeahirishwa kwa muda lichukue nafasi yake na kuendelea kuitikisa mitaa yetu.

Wiki hii nilitaka nisiandike mada ya Richmond kwani nimeshaandika mara mbili, nilianza na Kauli ya Nyerere kwa Lowassa nikaongeza Mvua ya Thailand. Leo nimeona nilijadili kwa mara ya tatu baada ya kujitokeza mambo mapya.

Uamuzi huo unatokana na mwenendo wa suala hilo ambao sasa unatanua wigo kwa kugusa eneo nyeti la vyombo vya habari, likituhusisha sisi waandishi wa habari.

Kubwa ambalo limejitokeza, ni kwamba kuna timu ya waandishi katika vyombo mbalimbali inajaribu kucheza mchezo ambao ni wa hatari, unafiki na aibu wa kutaka kuonyesha kwamba waliotiwa hatiani na Kamati Teule ya Bunge walionewa, kudhulumiwa na kutolewa kafara.

Bila kuuma maneno, moja kwa moja nasema kwamba waandishi wa aina hii hawawezi kukwepa kuingia katika kundi la ‘majasiri wa kifisadi’ katika nchi yetu.

Ujasiri wa kifisadi kwa baadhi ya waandishi umejitokeza bila aibu wala kificho, baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na wenzake akina Naziri Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha kujiuzulu nyadhifa zao.

Waandishi hawa wamekuwa wakitumia kigezo cha uhuru wa kutoa maoni kujaribu kujenga hoja nyepesi za kifisadi kujaribu kuwapaka mafuta waliojiuzulu kwa kashfa ya Richmond.

Uhuru wa kutoa maoni sasa unaonekana kuwa mhuri wa kutetea watu ambao wenyewe wamejipima wakaona hawawezi kuwa watumishi wa umma, wakaamua kujiuzulu wakijua kwamba walishindwa kuwajibika katika nafasi zao.

Ile dhima ya vyombo vya habari kuwa taswira ya jamii na zile sifa tele zilizotolewa na Kamati ya Bunge, Wabunge na wananchi kuhusiana na suala hili inaweza kupotea kama waandishi wa aina hii wataendeleza nia yao na kujifanya viziwi wakati wana masikio na vipofu wakati wa macho.

Upofu na ukiziwi unaojitokeza sasa unasikitisha na kutia aibu baadhi yetu, ambao maandishi yetu ya siku za nyuma yanatusuta na kuweza hata kuwa kitanzi kwetu cha msimamo wetu wa leo.

Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu maoni na mitazamo ya kichambuzi, kabla na hata baada ya Bunge kuamua kuunda Kamati Teule kuchunguza mchakato wa zabuni ya Richmond.

Kubwa ambalo nimegundua ni kuwepo mchezo mchafu, wa kinafiki, aibu na wa kusikitisha na unaokatisha tamaa kuhusu mustakabali wa nchi hii hasa baada ya kuona baadhi ya waandishi hadi wale wanaoitwa waandamizi wameangukia katika ujasiri wa kifisadi.

Nimegundua, baadhi ya waandishi wakati gumzo kuhusu Richmond likiwa limepamba moto baada ya kusainiwa mkataba huo na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Juni mwaka 2006, kwa namna moja au nyingine waliandika na kumhusisha aliyekuwa waziri mkuu.

Walitumia kalamu zao kuandika kwa mapana na mtiririko maalumu kuhusu sakata hilo huku wakisisitiza kwa kujaribu kuashiria si kutaja moja kwa moja jinsi Waziri Mkuu alivyokuwa akihusika kusimamia mchakato.

Lakini kwa mshutuko mkubwa, naona aibu na fedheha kubwa, baadhi yetu waandishi tumegeuka ‘vinyonga’ tunabadilika rangi katika aina ya mazingira tunayoingia.

Hili ndilo nimebaini baada ya kujiuzulu kwa mawaziri hao na Rais Jakaya Kikwete kuvunja baraza na kuliunda upya.

Ni dhahiri sasa baada ya matokeo hayo vita hii inahamishiwa kwenye vyombo vya habari, baadhi ya waandishi miongoni mwetu sijui kwa ushawishi gani, tunanaonekana kupofuka macho na kuziba masikio kuwa viziwi na kuyapa kisogo maslahi ya taifa.

Ni ajabu kuona miongoni mwa Watanzania maskini wanaolilia kupanda kwa gharama za umeme, ugumu wa maisha na nchi kuhujumiwa kwa mkataba mbovu wa Richmond, wanaibuka baadhi ya waandishi bila woga wala aibu wanajaribu kujenga hoja za kitapeli kutetea maslahi ya watu wachache.

Sawa, waliowajibika kwa kujiuzulu ni Watanzania wenzetu na ndugu zetu, lakini lazima tukubaliane katika msingi wa uwajibikaji kwamba hakukuwa na njia ya mkato zaidi ya kujiuzulu vinginevyo bunge lingewang’oa.

Nimejaribu kusoma, wengine wanajenga hoja kwamba ndani ya chama kuna watu wana chuki na Lowassa, wengine wanasema utendaji kazi wake na azma ya kugombea urais 2015, ni mambo ambayo yamemfikisha hapo.

Wengine wanahoji uwajibikaji wa pamoja (Collective Responsibility) ambao ni utamaduni wa kiutendaji katika serikali za CCM, pasipo kubainisha uwajibikaji wa pamoja katika jambo lipi.

Hili la uwajibikaji wa pamoja linaonekana ni jambo kubwa ambalo baadhi yetu waandishi tunalijengea hoja ya kitapeli, lakini hatuangalii upande wa pili vipi maamuzi ya baraza la mawaziri nayo yalipindishwa katika mchakato huu?

Watu wamekaa katika baraza la mawaziri chini ya uenyekiti wa Rais, halafu wengine kutoka hapo wanapindisha maamuzi hayo na kufanya ya kwao, je hapo uwajibikaji wa pamoja uko wapi?

Dhana ya uwajibikaji wa pamoja inakuja pale tu watu wanapokaa pamoja wakapitisha jambo fulani lakini baadaye likaleta matatizo. Lakini hapa unaweza kujiuliza, kama wanaotetewa wanajua uwajibikaji wa pamoja, vipi walipindisha maamuzi ya baraza la mawaziri?

Hapo utaongeza, kama watu walikaa ndani ya baraza la mawaziri wakaamua maamuzi fulani halafu, wengine wakaamua hivi kwa maslahi yao binafsi bila kuangalia maslahi ya taifa na yaliyopitishwa na vikao halali, nani wa kuwajibika?

Isitoshe ni aibu kusema Lowassa katolewa kafara na kamati ya bunge na kutoa taarifa za uzushi, kuchochea na zilizokuwa na nia mbaya naye. Hii si kweli, kamati ilitamka bayana watu wote waliopaswa kuwajibishwa na kuchukuliwa hatua za kinidhamu, lakini haikusema Lowassa ajiuzulu bali kwa nafasi yake apime uzito wa suala la lenyewe kisha achukue uamuzi.

Lowassa alipima uzito wa sakata hilo la Richmond na nafasi yake ya Uwaziri Mkuu jinsi ilivyotumika vibaya katika utoaji wa zabuni hiyo, akaamua kufungua mlango na kujiuzulu akifuatiwa na Karamagi na Dk Msabaha.

Amesema tatizo ni Uwaziri Mkuu ni kweli, tatizo si Lowassa bali ni madaraka ya umma yametumika vibaya katika mkataba wa Richmond, hivyo alipaswa kuyaachia.

Bahati mbaya aibu iliyoje, baadhi ya watu wanaacha ukweli uliozunguka suala lenyewe na maamuzi ya wazi aliyoyachukua Lowassa kuanza kujenga hoja zisizo na kichwa wala miguu.

Huu ni mtandao mpana, upo unajengwa ndani ya vyombo mbalimbali vya habari kwa lengo la kuwasafisha waliojiuzulu na kuwapaka matope waliounga mkono maamuzi ya kamati na wale wajumbe wa kamati husika.

Waandishi hao ‘vipofu na viziwi’ wengine wanajaribu kumchonganisha Lowassa na Rais Kikwete, kwamba kamtosa mwenzake, wanasahau kwamba inapofika wakati wa kuwajibika ‘umwenzake’ unawekwa kando, maslahi ya nchi yanachukua nafasi yake.

Lakini wakati baadhi ya waandishi wameamua kufanya ujasiri wa kifisadi, wenzao wenye fikra za kimapinduzi wanazidi kula kiapo cha kupigania maslahi ya taifa, hawaogopi mafisadi na majambazi wa kisiasa.

Fikra za kimapinduzi zinazidi kusambaa, watu wamechoka kuona nchi yao ikigeuzwa kapu la mjinga kila mtu anatia mkono, kazi ni moja kulinda na kutetea maslahi ya nchi.

Vita itapiganwa, waandishi wanaotetea maslahi ya taifa watashinda na wale wanaotetea maovu kwa kigezo cha uhuru wa kutoa maoni mbadala huku wakijaribu kujifanya mabingwa wa kupanga hoja za kifisadi, watashindwa na umma utawabaini na kuwahukumu.

Fedheha kubwa, haiwezekani baadhi ya waandishi watumie kigezo cha uhuru wa kutoa maoni kujenga hoja sawa na baadhi ya mawakili mahakamani, ambao kwa ujanja wa vifungu vya kisheria huweza kusaidia watuhumiwa hata wa mauaji kuweza kukosa adhabu ya kunyongwa na kuachiwa huru.

Kibaya zaidi, utakuta baadhi ya waandishi hawa watetezi wa watuhumiwa wa ufisadi nyumbani kwao ndugu zao hawana maji safi ya kunywa, hakuna huduma za afya, lakini wao wako Dar es Salaam wanapewa fedha kidogo wanasahau kabisa matatizo hayo, hawa ni majasiri wakubwa wa ufisadi katika nchi.

Ramadhan Semtawa ni mwandishi wa mwananchi;0782 528229 semtawa@yahoo.co.uk


Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post
 |  TrackBack URI for this post

Comments

Got something to say?