Vikongwe 7,680 wauawa

December 21, 2007

VIKONGWE 7,680 wameuawa kikatili kwa kukatwakatwa mapanga katika mikoa ya Tabora, Mwanza na Shinyanga kwa kipindi cha miaka 10 kilichoishia Desemba 2005, Tanzania Daima imethibitishiwa. Mwenyekiti wa Shirika linalojishughulisha na mapambano dhidi ya mauaji ya vikongwe nchini (COEL), Jamathon Magodi, aliliambia gazeti hili kuwa kati ya vikongwe waliouawa katika kipindi hicho, wanaume ni 114 tu.

Akizungumza na Tanzania Daima ofisini kwake juzi, mwenyekiti huyo alisema kwamba takwimu hizo zimeonesha kuwa mauaji hayo yanawalenga zaidi wanawake, ambao wengi wao wanaishi vijijini na kwamba yamekuwa yakiwasababisha baadhi ya wanawake kuishi kwa woga na wasi wasi.

Aliishauri serikali kutafuta njia za kukomesha mauaji hayo ambayo mengi yanatokana na imani za kishirikina na kushauri kuwa serikali inaweza kuiga kampeni kama za kupambana na kuzuia rushwa na ugonjwa wa ukimwi katika kupiga vita mauaji ya vikongwe.

“Vikongwe wengi sana wamekuwa wakipoteza maisha yao… hii ni hatari sana kwa usalama wa wazee wetu hao, na isitoshe kuna matukio kama hayo yanatokea na hayaripotiwi,” alisema.

Kufuatia kukithiri kwa mauaji hayo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, shirika hilo limeanzisha mafunzo maalumu ya wawezeshaji watakaokuwa wakielimisha wananchi kuachana na mauaji hayo.

“Lengo la mafunzo haya ni kuwawezesha wataalamu wetu kufikisha elimu ya kudhibiti mauaji hayo kwa jamii nzima kote nchini,” alisema.

KUTOKA: TANZANIA DAIMA


Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post
 |  TrackBack URI for this post

Comments

Got something to say?