Utafiti huu umechelewa sana
April 1, 2008
HALI ya elimu nchini imekuwa hairidhishi katika baadhi ya maeneo (ya kijiografia na yasiyokuwa ya kijiografia) kwa muda mrefu sasa.
Tukihusisha maeneo ya kijiografia, kuna baadhi ya mikoa, wilaya na shule mahususi hapa nchini, ambayo imekuwa sugu kwa kufelisha wanafunzi.
Tunaiita sugu kwa sababu katika matokeo ya kila mwaka, mikoa, wilaya na shule hizo zinakuwa zikishika mkia. Hatuna hakika iwapo hawa wanalielewa tatizo linalowakabili, kwani jitihada zao hazijaonyesha kuzaa matunda.
Tukija katika maeneo ambayo si ya kijiografia, yapo masomo ambayo wanafunzi wengi wanaonekana kutofanya vizuri. Masomo ya Hisabati, Sayansi na Kiingereza yanaongoza miongoni mwa masomo yanayoogopwa na wanafunzi wengi kutokana tu na historia na uzoefu wa wanafunzi wengi kufeli.
Hali hiyo imewajengea woga wanafunzi wapya ambao ili kujisalimisha, wanaamua kusoma masomo tofauti na hayo na kuifanya nchi kuwa na mrundikano wa wanataaluma wa aina fulani, huku ikiwa na upungufu mkubwa wa wanataaluma katika baadhi ya fani.
Ni jambo lililo wazi kuwa Tanzania ina uhaba mkubwa wa wanasayansi, wakiwamo madaktari na mainjinia. Hali hii imedumu kwa muda mrefu na jitihada za kuikwamua nchi kutokana na hali hizo zinaonekana kuendelea bila kutoa matunda tarajiwa.
Lakini inaelekea Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeamua kwenda hatua moja mbele, kwa kufanya utafiti juu ya tatizo hilo.
Kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wizara imesema kuwa inapanga kufanya utafiti wa nini kinasababisha wanafunzi wasiyapende masomo ya Hisabati na Sayansi.
Tunaipongeza wizara kwa hatua hii, kwani hii ni safari muafaka katika kutafuta kiini cha hali hii inayozidi kuwa mbaya kila mwaka. Lakini hapa tungependa pia kuieleza wizara kuwa hatua hii imechelewa sana.
Hii ni kwa sababu suala la wanafunzi kufeli masomo haya halikuanza juzi wala jana. Ni suala ambalo lipo kwa muda mrefu na wizara, kama mlezi na msimamizi mkuu wa masuala ya elimu, ilipaswa kulibaini na kulifanyia utafiti miaka mingi iliyopita. Iwapo hili lingefanyika, tuna uhakika hali yetu isingekuwa kama ilivyo leo.
Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Dk. Hamis Dihenga, inadhaniwa kuwa tatizo huenda likawa mada zinazotumika kufundishia, walimu, vifaa vya kufundishia au vitu vingine vya namna hiyo, hivyo wizara itaangalia ni kipi cha kufanya kuweza kubadili hali hiyo.
Tungependa kuishauri wizara kwamba, yule atakayefanya utafiti huo, utafiti uhusishe mambo nje ya hapo.
Tunaamini kuwa zipo sababu nyingi sana zinazomfanya mwanafunzi afeli somo la Sayansi na Hisabati, hivyo kuyachukia.
Nyingi ya sababu hizi zinaweza kuwa nje kabisa na mazingira na mfumo rasmi wa elimu tulio nao.
Kwa hiyo, ni vema utafiti ukaangalia masuala mengi ambayo yana uhusiano na kujifunza moja kwa moja, pia kuangalia masuala ambayo hayana uhusiano wa moja kwa moja na kujifunza.
Utafiti unapaswa kuiangalia jamii kwa upana wake, kwani mambo yaliyomo katika jamii yanaweza kuathiri maamuzi yanayofanywa na mwanafunzi anapoamua asome nini kwa ajili ya maisha yake ya baadaye.
Kwa mfano, wakati ambapo mwanafunzi anaona kuwa wanasayansi hawathaminiwi katika nchi yao, ni vigumu kwake kuamua kusoma masomo hayo, na hata kama atasoma, anaweza kufeli kutokana na woga tu wa jinsi wanasayansi wanavyoishi maisha yasiyo na uhakika.
Na hili lifanyike kwa umakini mkubwa kwani huu utakuwa ndio msingi unaoweza kutumika kupanga mipango ya baadaye kama taifa, kupitia kwa watoto watakaokuwa wanafundishwa.
Iwapo tutaliona hili kama aina nyingine ya ulaji kwa watafiti, tutakuwa tunafanya kosa kubwa.
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
One Response to “Utafiti huu umechelewa sana”
Got something to say?


Naipongeza Wizara kwa uamuzi huu, sio siri masomo ya sayansi yanaongoza kwa
wanafunzi kufeli mitihani yao, hivyo basi suala hili litiliwe manani.