Umaarufu wa CCM wazidi kuporomoka hadi 40%
August 20, 2008
UMAARUFU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) umeshuka kutoka asilimia 71 mwaka 1999 hadi asilimia 40 Oktoba 2007, utafiti uliofanywa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (REDET) umeonyesha.
Kwa mujibu wa utafiti huo, wakati umaarufu wa CCM ukipungua, upinzani umezidi kujiimarisha katika kipindi hicho.
“Kama jedwali linavyoonesha hapa, mwaka 1999 asilimia 71 ya wahojiwa wote walisema wanaridhika sana na utendaji kazi wa CCM katika mfumo wa vyama vingi, kiwango hicho cha kuridhika sana kilipungua hadi kufikia asilimia 40 Oktoba 2007,” alisema Dk Killian.
Alisema katika kipindi hicho idadi wanaoridhika na utendaji wa vyama vya upinzani imeongezeka kidogo ikilinganishwa na watu waliotoa maoni yao kuhusu CCM.
Alisema ingawa idadi ya wanasema wameridhika utendaji wa vyama vya upinzani ulipungua kutoka asilimia 43.4 mwaka 1999 hadi asilimia 18 mwaka juzi, kiwango hicho kinaonekana kuanza kupanda katika kipindi cha mwaka jana.
Awali, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala, alisema CCM kimepata misukosuko mingi zaidi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kuliko wakati mwingine wowote tangu kuanzishwa kwake.
Profesa Mukandala alisema hayo jana alipokuwa akifungua Mkutano wa 16 Redet unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Alisema pamoja na ukweli kwamba CCM bado inafurahia matunda ya kushika dola, mpasuko uliojitokeza ndani yake tangu wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, umetoa mwanya kwa wapinzani kukipa changamoto.
“Hii ni mara ya kwanza kwa wanachama wa CCM kusimama wakiungana na wapinzani kukemea maovu ndani ya chama hicho kama ilivyo kwa tuhuma za ufisadi,” alisema.
Profesa Mukandala alitaja mambo yanayoipa CCM changamoto kuwa ni migogoro ya kitaifa ikiwamo Mahakama ya Kadhi, suala la Muungano na hoja ya Zanzibar kutaka kujitenga na Unguja.
Mambo mengine ni tuhuma za ufisadi zinazotokana na mikataba mibovu na matumizi mabaya ya mali za umma, migomo ya wafanyakazi, ubinafsishaji na uwajibikaji wa watendaji wake.
Kwa mujibu wa Profesa Mukandala, wakati CCM ikionekana kuwa na wakati mgumu, upinzani umejiimarisha na kuonyesha nguvu ambayo haikuwahi kuwapo miaka ya nyuma.
“Moja ya mambo yanayoonyesha upinzani umejiimarisha ni uwezo wa kutengeneza bajeti mbadala yenye kutoa changamoto kwa serikali na kuwa mstari wa mbele kuibua hoja na mijadala ya kitaifa yanayowagusa hata viongozi wa seriakali,” alisema.
Akizungumza katika mjadala huo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, alisema hali ya kisiasa nchini ni mbaya na kwamba kunahitajika jitihada za makusudi kunusuu hali hiyo.
Alisema kauli za baadhi ya viongozi wa serikali kuhusu mijadala mbalimbali ya kitaifa ni za kuligawa taifa badala ya kuliunganisha na hali hiyo ni mbaya kwa hatma ya taifa.
“Inaogopesha kusema hali ya nchi ni mbaya sana, kauli za baadhi ya viongozi kuhusu Mahakama ya Kadhi, Muungano na hoja zingine za kitaifa ni za kuligawa taifa badala ya kuchochea umoja,” alisema Zitto.
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

