Ufisadi Ole wenu CCM

February 27, 2008

SERIKALI na Chama Cha Mapinduzi (CCM) vina bahati, tena ya mtende. Bahati hiyo si nyingine, bali ile inayoendelea kukipa jeuri ya kuendelea kubakia madarakani kikiunda serikali kila mara kinapokutwa na misukosuko.

Katika kipindi chote cha miaka 15 na ushei ya mfumo wa vyama vingi, CCM na serikali yake, ambacho sina shaka yoyote kukiita ‘Kiota cha mafisadi’, kimeweza kwa kutumia mbinu mbalimbali chafu zinazolenga kuwahadaa wananchi kwa hili au kwa lile kulinda mamlaka yake ya kiutawala.

Uchaguzi mdogo wa Kiteto

Watu wa mwisho kuhadaiwa katika mlolongo huo huo wa kifisadi unaoratibiwa na kikosi maalumu ndani ya serikali ya CCM ni wananchi wa Jimbo la Kiteto, ambao kura walizopiga zimemrudisha mbunge kutoka chama hicho tawala.

Taarifa za awali zinaonyesha kuwa, gharama za kumrudisha mbunge huyo wa CCM ambaye taarifa zinaeleza waziwazi kuwa ni matokeo ya aina ya ufisadi wa kifikra unaoratibiwa na viongozi wa chama hicho na wa serikali, zimejengwa chini ya wigo wa mtindo uliodumu miaka nenda - rudi ya kununua shahada za wapiga kura kwa muda na kuzirudisha baada ya uchaguzi kupita.

Ushahidi wa mazingira unaweza kuyathibitisha maneno haya. Kwamba wapiga kura waliojitokeza kupiga kura siku ya Jumapili hawazidi asilimia 47 ya watu waliopaswa kujitokeza siku hiyo, ni jambo linalotia shaka.

Kwa sababu hiyo basi, ushindi wa Mbunge wa CCM, Benedict ole Nangoro, aliyepata kura 21,506, akiwa amemshinda mgombea wa upinzani Victor Kimesera, aliyevuna kura 12,561, unakuwa usio na mvuto wa kiwakilishi, hasa inapobainika kwamba wapiga kura waliopaswa kupiga kura walikuwa ni 74,626 na badala yake wakajitokeza watu 35,261 tu.

Hali hii inaweza kuyaelezea matokeo hayo kuwa yasiyowakilisha matakwa halisi ya wananchi wa Kiteto ambao ukijumlisha wale waliokuwa na miaka kati ya 15 na 17 mwaka 2005 wakati daftari la wapiga kura likipitishwa, idadi yao inaweza ikawa ilifikia watu 100,000 ambao kimsingi ndio waliopaswa kupiga kura, iwapo zoezi la kusajili wapiga kura wapya lingefanyika mapema.

Kwa sababu hiyo basi, upo uwezekano mkubwa kuwa idadi ya wapiga kura waliojitokeza hiyo Jumapili haikuzidi asilimia 40 ya watu wote wazima wenye umri wa zaidi ya miaka 18, ambao walikuwa na haki ya kumchagua mbunge wa kuwawakilisha. Haya ndiyo matokeo ya ufisadi wa kifikra unaoratibiwa na CCM na serikali yake.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, vyama vya upinzani vinalazimika kunaswa katika mtego huo wa kifisadi ambao unawanyima fursa ya kushinda ubunge wakati wanapostahili, hasa inapoeleweka bayana kuwa hivi sasa wengi wa watu wanaoviunga mkono vyama hivyo ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 na 40.

Kashfa ya Richmond

Wiki moja tu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa Kiteto, taifa lilikuwa likipita katika tanuri la moto kutokana na ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Harrison Mwakyembe (CCM).

Ripoti hiyo ambayo ilifanikiwa kuwatia hamasa wabunge na wananchi walio wengi, hatimaye ilihitimisha uwaziri mkuu wa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, na uwaziri wa Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha, ambao wote majina yao yalitajwa katika ripoti hiyo ambayo nitaendelea kuiita ya kisiasa zaidi kuliko kiutendaji.

Wiki mbili sasa tangu ripoti hiyo itoke, matokeo ya kazi nzuri ya kina Mwakyembe iliyofanywa kwa nia mahususi, yamefanikiwa kuirejeshea heshima serikali ya CCM machoni mwa wananchi na watu wengine wa nje.

Aidha, ripoti hiyo ya Mwakyembe ambayo kwangu mimi ninaiona ikiwa na ubia wa moja kwa moja na matakwa ya Rais Jakaya Kikwete na Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kwa upande mwingine umemrejeshea rais na chama chake heshima iliyoanza kupotea kutokana na makosa ya kimaamuzi, kisiasa na kiutendaji ya watendaji na wanasiasa wa CCM.

Nikiwa mwanahabari na mtu ninayeamini kwa dhati kabisa kuwa ‘Kashfa ya Richmond’ ni ya serikali nzima ya CCM, hili la chama hicho tawala, serikali na Rais Kikwete kurejesha heshima yake kwa sababu tu ya kung’oka kwa kina Lowassa, Karamagi na Msabaha ndilo linalonikera na kunisikitisha.

Ninasikitishwa na kukerwa na tukio hilo kwa sababu kadhaa. Kwangu mimi Richmond iliyoitikisa serikali ni mradi wa wakubwa, wanasiasa na watendaji ndani ya serikali nzima ya CCM ambao wingi wao unaweza kuzidi idadi ya vidole vya mikononi na miguuni.

Ushahidi wa ukweli huu kwamba Richmond ni mradi wa wakubwa wengi serikalini uko bayana kabisa na hata ukisoma vizuri ripoti ya Kamati ya Mwakyembe unaweza ukaliona hili kwa haraka haraka kabisa.

Ukweli kwamba matapeli wa Richmond ambayo ni kampuni hewa ilishinda zabuni ya kujenga bomba la mafuta kati ya Dar es Salaam na Mwanza mwaka 2004, iliweza kupata cheti cha uwekezaji katika Kituo cha Uwekezaji cha Taifa (TIC), ikasajiliwa kinyume cha matakwa ya sheria za usajili wa makampuni (Brela) na ikawa ikipata taarifa zote muhimu za mwenendo wa mambo serikalini na hata ndani ya Tanesco, ni ushahidi wa wazi kwamba matapeli hawa wana mkono mrefu ndani ya serikali.

Kwa sababu hiyo basi, hoja yangu kuhusu Richmond ni rahisi kabisa. Kina Lowassa, Rostam na wenzao wengine ndani ya kampuni hii ni vidole tu vya mkono mrefu ndani ya CCM na serikali, ambao hauna budi kukatwa na sisi sote.

Hilo ndilo linalonisukuma kutaka kuona serikali nzima ya CCM ikiwajibika kwa kuliingiza taifa katika utapeli huu wa fedheha, ambao kimsingi mizizi yake ingali imebakia ndani ya chama hicho tawala na serikalini.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba, wakati baadhi yetu ambao tangu mwanzo tumekataa kuyumbishwa na hili, tukagombana na Lowassa hadharani na kuvutana na kina Edward Hosea waziwazi hata kuhatarisha maisha, kazi na makampuni tuyayofanyia kazi, eti leo hii tunaonekana wasaliti, tunaitwa majina mabaya na kuzushiwa uongo usiovumilika.

Baadhi ya waandishi wa habari ambao hawaifahamu sawasawa CCM na serikali yake na ambao hawajui mbinu chafu za maofisa wa usalama ambao jukumu lao ni kuinusuru serikali hata inapokuwa imejichafua namna gani, ndio ambao wanatumika kututukana matusi mabaya baadhi yetu tunaolipigania hili.

Ni jambo la kufedhehesha kwamba leo hii masilahi ya serikali ya CCM ndiyo yanayotaka yachukuliwe kuwa ndiyo masilahi ya taifa. Ni jambo la kusikitisha kwamba aibu ya baraza zima la mawaziri inataka kugeuzwa kuwa ya watu wachache tu. Hili kwangu haliwezekani.

Mwenendo wa mambo kadhaa serikalini unaonyesha pasipo shaka kwamba, tangu ripoti ya Redet ilipotoka mwishoni mwa mwaka jana, ikionyesha kuporomoka kwa umaarufu wa serikali na kuzorota kwa mvuto wa Rais Kikwete, mambo yalianza kubadilika miongoni mwa viongozi wetu.

Nina hakika kwamba matukio kama yale ya ushindi wa hoja za Buzwagi za Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), kuibuliwa kwa kashfa ya wizi ndani ya Benki Kuu (BoT) na baadaye kuzomewa kwa wabunge na mawaziri wa CCM, huku baadhi yao wakifikia hatua ya kurushiwa mawe, ni sehemu ya mambo yaliyosababisha mabingwa wa masuala ya usalama wa taifa na viongozi wa juu wa CCM watafute mbinu ya kujitakasa, ikiwa ni pamoja na kuwasaka wale walioifikisha serikali mahali ilipokuwa kabla Mwakyembe hajatokea na kuwa mwokozi wa CCM na serikali yake.

Hali hiyo ya mambo ndiyo ambayo kimsingi ilisababisha Rais Kikwete alazimike kukubali Bunge liunde Kamati Teule kuichunguza Richmond na kabla ya hapo akawa ameridhia BoT na hususan akaunti ya malipo ya madeni ya nje (EPA) kuchunguzwa na baadaye akaamua kuahirisha kufanya mabadiliko ya baraza la mawaziri.

Mambo hayakuishia hapo, naamini mwenendo huo wa serikali kupoteza mvuto kulikokuwa kukiendelea kumdidimiza Kikwete binafsi na kuporomosha hadhi ya CCM hata kwa makada na wananchi wa kawaida, ndiko ambako kulimfanya rais akishirikiana na washauri wake, wamlazimishe Spika Sitta kusitisha ziara yake ya Marekani, lengo likiwa ni kuinusuru dola ambayo dalili zote zilikuwa zikitoa mwelekeo wa kuanguka.

Miongoni mwa maamuzi yaliyokuwa yamefikiwa nyuma ya pazia ili kuinusuru dola, ilikuwa ni kuwamaliza nguvu pacha wawili wa kisiasa, Rostam Aziz na Edward Lowassa, ambao wakati fulani walifikia hatua ya kuonekana machoni mwa watu ndani ya CCM na serikalini na hata nje wakiwa ni wabia wa urais wa Kikwete.

Baadhi yetu tuliokuwa na jeuri ya uanahabari tulipata kuliweka hili bayana, tena ana kwa ana mbele ya Kikwete mwenyewe na tukamuuliza alikuwa akimaanisha nini alipowatangazia Watanzania kwamba urais wake ulikuwa hauna ubia na mtu yeyote?

Ingawa yeye mwenyewe alilipiga chenga swali hili hadharani, jibu lake ni rahisi kabisa; Rais alikuwa ameshafikishiwa taarifa za kuwapo kwa dukuduku lililokuwa likithibitisha kuwapo kwa ubia katika madaraka yake.

Ni wazi kwamba hali hii ya mambo haikuwafurahisha wakuu wa usalama wa taifa. Ni dhahiri pia kwamba, hata Rais Kikwete mwenyewe alisononeshwa na hali hii ya mambo na hapo ndipo ulipoanza mkakati wa ama kuusafisha urais wa rais wetu.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, wakati baadhi ya wana habari walikabiliana moja kwa moja na ‘utatu usio mtakatifu’ ndani ya CCM na serikali yake siku hizo, wenzetu kadhaa waliokuwa wakijifanya marafiki na maswahiba wa Kikwete, Lowassa, Rostam na wenzao wengine wengi wa CCM na wale wanamtandao, walijificha chini ya uvungu wakitishwa na mamlaka ya urais, uwaziri mkuu, uanamtandao na u-CCM.

Leo hii sehemu ya vita tuliyoiongoza ambayo sisi washiriki wake tunaiona kuwa ushindi uliopatikana, ni mwembamba na ambao haukustahili, tunaanza kuonekana ni wasaliti pale tunaposimama na kusema hapana; vita hii hatukutaka iishie hapa. Bado waliotoka ni wachache sana, wengi wangali wamo ndani ya CCM, na kimsingi ndani ya serikali.

Matokeo haya yasiyoridhisha ndiyo yanayonipa jeuri ya kudai matokeo ya ziada, ndio msingi wa hoja ya kuhamasisha kuunganishwa kwa nguvu za kujenga uhalali wa kuing’oa CCM madarakani kupitia sanduku la kura wakati wowote hata kama hatua hiyo ingefikiwa kabla ya mwaka 2010. Jambo hilo ndilo linalobakia kuwa ndoto zangu mimi na za mwanahabari mwenzangu Ansbert Ngurumo.

Kwa sababu hiyo basi, wale wa ndani ya CCM wanaojidanganya kwamba baadhi yetu tumeanza kumsafisha Lowassa, wanajidanganya. Wale wanaodhani kwamba kuondoka kwa mawaziri hao watatu kwa kujiuzulu na kusutwa kwa watu wengine kadhaa kutakinusuru chama hicho tawala dhidi ya ukali wa kalamu zetu au mwelekeo wa mtazamo wetu, wanapotoka. ‘CCM must go’ hiyo ndiyo dhamira yetu ya wazi.

Napenda kuhitimisha makala yangu ya leo nikiweka bayana msimamo wangu katika hili. Ripoti ya Kamati ya Mwakyembe imetoa matokeo dhaifu (cosmetic changes). Tatizo la CCM, viongozi wake na serikali yake ni kwamba imechoka. Imefikia ukomo wa uadilifu, umakini na uwajibikaji. Watanzania tunapaswa kuangalia mbele huku tukijua tunalazimika kuiondoa madarakani kupitia sanduku la kura hata kama itatulazimu kufanya hivyo ndani ya kipindi kisichozidi miaka mitano.

Watanzania wenzangu wangelitambua hilo mapema, wangebaini kuwa Kashfa za EPA na hii ya Richmond peke yake vilikuwa ni fursa adhimu ambayo ilikuwa ikilipa Bunge mamlaka ya kujenga msingi imara wa kuiangusha CCM. Hili halikutokea kwa sababu ya janja ya kina Kikwete, Mwakyembe, Sitta na wenzao wengine wengi. Hatujakata tamaa. Huko ndiko TUENDAKO.


Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post
 |  TrackBack URI for this post

Comments

Got something to say?