Ufisadi ni sehemu tu ya matatizo ya BoT

January 29, 2008

SASA hivi, kama ilivyo ada kwa jambo lolote jipya, matatizo ya uendeshaji wa Benki Kuu Tanzania (BoT) (chombo ambacho, pengine ni nyeti kuliko vyote katika usimamizi wa masuala ya uchumi katika nchi yoyote ile duniani), ndiyo habari kubwa nchini. Kila mmoja kwa nafasi yake analo la kusema. ‘Ballali akamatwe’, ‘Mgonja naye asiachwe’, ‘Mramba naye yumo kwenye skandali nzima’; basi ilimradi kama hadithi ya paka na panya kila aliyemo na asiyekuwamo anapaswa kuhusika.

Wako wanaotwambia Ballali kesharejea nchini, wako wasemao kaonekana Malta, na hata baadhi kutabiri kuna vigogo hawataki aguse ardhi ya Tanzania eti ana siri nyingi za kuwaumbua kuhusu ufisadi ndani ya benki hiyo.

Baadhi walimshikia bango Rais amtimue kazi lakini, leo hii, kaja Profesa Ibrahim Lipumba na kusema Rais kumweka benchi Ballali ili uchunguzi ufanyike ni kujitafutia umaarufu wa muda. Sasa, Rais afanyeje? Ukweli ni upi?

Ballali na hao wengine, kama akina Mgonja, Mramba na pengine hata Waziri wa sasa wa Fedha, Zakia Meghji, tunaowashikia bango kila kukicha kuwa wanahusika na sakata lote, bado hawajashitakiwa na mahakama yoyote nchini kwa kosa linalohusu ufisadi wa benki hiyo nyeti nchini.

Kama Rais, kwa dhamana aliyonayo, tayari amemweka benchi Ballali na kuteua tume ya wataalamu kuchunguza sakata zima na kuipa miezi sita sasa, nini cha kusababisha tafrani yote hii? Kwa nini tusiwe na subira ya miezi sita? Kama ni ufisadi uliofanyika miaka nenda miaka rudi, kweli, miezi sita ni mingi kusubiri?

Inaelekea kuna baadhi ya wenzetu wanaotaka kulazimisha agenda zao zifanikishwe kwa kupitia mitafaruku mbalimbali katika jamii yetu. Na haya si mara ya kwanza nayaandika katika safu za gazeti hili.

Binafsi, na wengi wetu, hatufurahishwi na yaliyofanyika Benki Kuu. Katika makala ya nyuma nimeandika mawazo yangu, na ya wengi ninaowasiliana nao, kuhusu ufisadi uliofanyika.

Lakini, yaliofanyika si ajabu katika anga za masuala ya benki duniani. Uingereza na hata wakati naandika makala hii pia Ufaransa kuna skandali kubwa tu za masuala ya ufisadi unaohusu baadhi ya benki za nchi hizo. Hakuna cha ajabu!

Midhali taasisi, ziwe nyeti au vyinginezo, zinaongozwa na binadamu na kuwa binadamu tuko wa kila aina, basi, kutakuwa na walakini na mushkeli katika uongozi na kuziongoza Taasisi hizo.

Huu ndiyo ukweli wa kimaumbile unaotuongoza. Na ndiyo maana ndani ya utawala wa serikali zimewekwa taratibu na miongozo ya kuendesha shughuli za uongozi wa vyombo mbalimbali vya serikali.

Taratibu hizo zinapokiukwa basi wenye dhamana za kuhakikisha taratibu hazikiukwi na kuwa waliokabidhiwa dhamana za madaraka hawajisahau kiasi hicho, huwa wanayarekebisha mambo haraka yanapoharibika. Mfano hai ndiyo kama huo wa Rais Jakaya Kikwete kumvua madaraka na dhamana ya ugavana, Daudi Ballali.

Sambamba na uchunguzi kuhusu tuhuma za ufisadi wa hizo shilingi bilioni 133 na ushei, lakini pia, ndani ya Benki Kuu kunafanyika uchunguzi wa ukaguzi wa ndani wenyewe ndani ya chombo hicho, kuangalia kama uko upotevu na ufisadi wa ama zaidi ya huo ama mwingineo uliofichika.

Katika masuala ya ukaguzi wa masuala ya fedha na mambo yanayohusiana na hayo, kilichofanywa na wakaguzi wa nje wa Benki Kuu, ni kuhoji kuhusu malipo yasiyo na maelezo, basi! Hamna zaidi ya hicho.

Inawezekana kabisa baadaye yakapatikana maelezo ya kukidhi maswali yaliyoibuliwa na hao wakaguzi wa nje. Iwe matumizi yaliidhinishwa na Juma au Abdu si cha msingi.

Ni kwamba yaliidhinishwa pengine kwa kauli tu. Hamna cha ajabu kwenye hili. Yanafanyika kote duniani. Lakini yote haya tutayajua baada ya hiyo miezi sita. Kwa nini subira itushinde Watanzania ambao, moja ya sifa yetu kubwa duniani, ni subira?

Tumesubiri vipindi vingapi vya hali ngumu chini ya Mwalimu Nyerere? Au wapo waliosahau tulivyoombwa na kuambiwa kuendelea kufunga mikanda hadi kiuno kwisha? Sasa hii miezi sita, kweli, itushinde? Ama baadhi ya wenzetu wana visa tu na uongozi huu wa Kikwete? Hakika, sitaki kuamini hivyo!

Kama Ballali anao ufisadi kaufanya tuvute subira, tutajua, kama Mgonja anahusika tuvute subira tutajua. Kama Mramba anahusika tusubiri, tutajua na tutamzomea ikibidi baada ya vyombo husika kumhukumu. Tusiwe sisi wa kutoa hukumu kabla ya watoa hukumu hawajatoa hukumu.

Hapa nachelea kuwa mbele ya sheria endapo sisi jamii tutatoa hukumu kwa kudhani fulani ana hatia kabla ya ushahidi madhubuti kufikishwa na kuitosheleza mahakama kuwa ushahidi huo ni madhubuti wa kumhukumu mhusika mbele ya mahakama, basi huyo tunayemtuhumu atajinusuru mbele ya mahakama kwamba tayari jamii tumeshamtuhumu na kuwa mahakama haiwezi kumtendea haki kwa kuogopa kwenda kinyume na tuhuma za jamii.

Tusifike huko na tusizifikishe mahakama na vyombo vyetu vingine vyenye dhamana hizo huko. Tutapotoka na kwenda kusipo.

Watanzania tunayo yetu. Tunazo sifa zetu zinazotutenganisha na wengine duniani. Wapo wanaotaka kutulazimisha tusiwe tulivyo. Pengine na Mungu atuepushe, wanataka tuwe kama wa wenzetu Kenya! Kwa dhana na mawazo yao potofu kuwa Uchina walitusaidia kuiba kura za mwaka 2005, basi, mwaka 2010 kama na hapa narudia, kama Uchina wataisaidia tena CCM kuiba kura basi watakaoshindwa waingie mitaani tuuane! Sasa nani amuue nani?

Kuna serikali yoyote duniani ambayo haina kashfa ya ufisadi kwenye taasisi yake yoyote? Ni ipi? Marekani, Urusi, Uingereza au Ujapani? Anisahihishe bingwa yoyote wa hoja! Na namkaribisha kwa moyo mkunjufu, kabisa! Kwa nini hiki kitu ‘due process’ tuna kizungumzia kwa mdomo tu lakini, kamwe, hatupendi kitendeke? Rais kaamuru fedha zilizofujwa zirejeshwe, uchunguzi ufanyike na ikibidi wale wenye wakosa wafikishwe kunakostahili hukumu ya makosa yao.

Benki Kuu ina matatizo mengi na makubwa sana licha na hata hilo la ufisadi, Benki Kuu imeanzishwa na imetokana na mfumo tofauti na mtazamo mwingine kabisa wa siasa kuliko ambao tulio nao hivi sasa.

Yapo mengi ambayo benki hiyo kama Benki Kuu ingepaswa kufanya na kusimamia katika mtazamo mzima wa uchumi (na, pengine, macro-economic policies) wa nchi. Kuna mambo kama ya ‘price stability’, ‘interest rates’, ‘employment’ na mengine kama ya ‘fluctuation’ ya shilingi yetu kwa dola.

Tulifika mahali kwa siku moja shilingi inaporomoka mara tatu dhidi ya dola na benki ipo. Miujiza na hata mtu unajiuliza hivi Benki Kuu ipo kweli?

Mifumo ya uendeshaji wa Benki Kuu ni mingi na inatofautiana kati ya nchi na nchi duniani. Kuna baadhi ya nchi benki kuu zao ni huru na haziingiliwi hata na Rais wa nchi husika.

Zinaachwa kuendesha masuala ya usimamizi wa fedha na mambo ya nchi kama inavyoona yenyewe. Hapa kwetu ni tofauti. Benki Kuu yetu haina uhuru mpana wa kusimamia masuala ya fedha, pamoja na kuwa gavana wake alipewa madaraka na uhuru mkubwa sana.

Gavana mpya ameahidi mabadiliko na uwazi wa jinsi chombo hicho kitakavyoendeshwa chini ya uongozi wake. Yote ni mambo muhimu kwa ufanisi wa muda mrefu wa chombo hicho. Pengine, usiri ndiyo chimbuko kubwa la matatizo mengi ya uendeshaji wa Benki Kuu yetu.

Yote haya, na kama nilivyoainisha mwanzoni, tuyape muda. Wahusika wanasema yatashughulikiwa. Sisi ni nani wa kutilia shaka kauli zao? Si tuvute subira tu! Tusubiri na tuwape muda wajikaange kwa kauli zao wenyewe!

Waandishi habari tuna jukumu kubwa la kuiarifu jamii nini kinachoendelea ndani ya Benki Kuu. Wenyewe tukianza na kutokuwa na subira ni wazi kuwa tutaipotosha jamii kwenye kuwaeleza ukweli.

Serikali ina mambo na majukumu mengi ya msingi. Kama kushughulikia hilo la ufisadi ni wazi kuwa linafanyika. Kwa nini tusiiache ikaendelea na shughuli zingine?


Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post
 |  TrackBack URI for this post

Comments

Got something to say?