Ufisadi ni matokeo ya ukosefu wa maadili
February 28, 2008
SAMAKI mkunje angali mbichi, akisha komaa, hakunjiki, kwani ukimkunja, atavunjika. Huu ni usemi ambao umekuwa ukitumika sana hususan pale mtu anapozungumzia suala linalohusu maadili na nidhamu katika maisha ya binadamu yeyote.
Kwa Tanzania, usemi huu na kwa wakati huu, una maana kubwa sana kwani ni wazi kuwa kwa mtazamo wa mambo mengi, suala la maadili kwetu limetutoka na kila mtu anaamua kuishi kivyake jinsi anavyoona kuwa inamfaa yeye kuishi.
Taifa limebaki na watu wabinafsi, wachoyo, wakorofi, wezi na wasio na uzalendo hata kidogo na wasio na upendo kwa maskini.
Hili ni tatizo kwani hakuna wa kumnyoshea mwenzake kidole na kumwambia ‘Acha!’ hii kwani wote tuna matatizo ya kinidhamu.
Kwa kuwa nidhamu ina maana pana kwa mtazamo wa nidhamu ninayotaka kulenga leo, nitazungumza tu upande wa maadili katika kutumikia taifa kama watumishi na wataalamu wa Kitanzania.
Kwa kipindi cha miezi kadhaa sasa toka mwaka jana na hasa tangu kipindi cha Bunge la Bajeti la mwaka jana, Bunge, serikali imekuwa ikishutumiwa kwa kuficha na kufumbia macho uozo wa viongozi wake na kuwahifadhi baadhi ya watu wanaoitwa mafisadi, wezi, wahujumu na wala rushwa.
Kundi hili la watu wa namna hii wametajwa sana katika vyombo vya habari na hata marehemu Mwalimu Nyerere alizungumza sana wakati wa uhai wake na akakemea kuwa watu hawa watakuja kuliangusha na kulifilisi taifa baadaye.
Mambo yameanza. Tanzaania watu wanashangaa, inawezekanaje viongozi kuanikwa hadharani na kutajwa majina eti wamehusika kula rushwa na kuchezea mali za umma?
Nini chanzo cha mambo yote haya? Kwa mtazamo wangu, hii ni ukosefu wa nidhamu na heshima kwenye taaluma zetu. Watu hawaheshimu nafasi walizo nazo kabisa na hili ndilo tatizo limefanya kila mtu anamwone mwezake kama mwovu, yeye ni safi, tunasema ni nani wa kumnyoshea mwenzake kidole?
Kila mtu hasa wenye madaraka na maamuzi ya juu wanaogopa kuwakamata au kuwaadhibu waliotajwa kwa sababu nao hawako safi.
Wanaona wakiwaadhibu nao watataja madhambi yao, nani wa kumnyoshea mwenzake kidole?
Hii imetokea katika idara za serikali baada ya watu fulani kutajwa kuwa ni wala rushwa, mafisadi na wahujumu uchumi, wameshindikana kuadhibiwa kwa sababu wanaotakiwa kuwaadhibu wote ni ‘Waarabu wa Pemba wanajuana kwa vilemba’.
Anayetajwa na anayetaja, wote wanashutumiana kuwa ni wadhambi, je, ni kweli kuwa Watanzania tunataka kubadilika? Ni kweli kuwa kwa kuwataja tu bila kufuatilia kuna linaloweza kusaidia? Au ni kuwatisha ili wapunguze? au kuwafumba macho Watanzania?
Hivi karibuni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete alisikika akiwaambia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM huko Dodoma kuwa serikali itawaadhibu wote waliotajwa au wanaohusika na ufisadi.
Je, ni kweli kuwa CCM watakubali kuwaadhibu wanaotajwa wakati wengi wao kulingana na majina yaliyotajwa ni makada wazuri na baadhi ni wafadhili wa chama hicho?
Je, hatua ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha, inatosha kujiuzulu bila kuchukuliwa hatua za kisheria?
Hapa ndipo penye shida, kwani pamoja na kuwa wote hatuko safi lakini yule anayedaiwa kuwa mchafu anatusaidia na kutuwezesha kuishi. Je, chama kipo tayari kuwaadhibu?
Hapa ndipo suala la maadili linapokuja kufanya kazi, na suala la kusaliti masilahi binafsi na kuangalia masilahi ya taifa.
Dk. Charles Kitima, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mt. Augustino, anasema “Wasomi wengi wanasoma wakifikiria tu namna watakavyokwenda kufaidika wao wenyewe na kujikusanyia mali kuwa matajiri, watu hawahesimu maadili ya taaluma zao (Professional Ethics and Integrity).
Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa amejaribu kutamka hadharani baadhi ya majina ya watu wanaodaiwa kuwa ni mafisadi, kundi hilo ni baadhi tu ya wanaohusika na mambo kama hayo, je, tangu majina yametajwa, wale ambao hawakutajwa wamejirekebisha?
Watu wanaonekana kuwa sugu, hawaogopi tena, wengine wanajivuna kwa kuwa wana pembe na hakuna wa kuwagusa, kwani kila anayehusika kugusa tayari ni rafiki yake au labda wamewahi kula pamoja.
Hili ndilo tatizo la maadili. Nani wa kumkamata mwingine? nani achukue jiwe amtupie mwenzake? Kila mtu anajitazama anajiona mwovu kuliko aliyetajwa ambaye anapaswa kusulubiwa.
Wachambuzi wa haya mambo wanasema ukiangalia wanaoshutumiwa sana si watu waliosoma zamani kabla ya uhuru au muda mfupi baada ya uhuru.
Wengi ni watu wa makamo na waliokuwa shuleni wakati wa miaka ya 1970 na walijifunza vizuri na kuona harakati za Azimio la Arusha lililoendeshwa na Mwalimu Julius Nyerere na hayati Edward Sokoine.
Wanaelewa wazi kuhusu vita iliyopigwa juu ya ufisadi, rushwa na kuhujumu mali za umma, lakini leo hii baada ya miaka 30 wana sahahu na wanayatenda yale ambayo Mwalimu na Sokoine waliyakataa.
Ndicho kizazi ambacho wengi wao ni walimu wanaandaa wanataaluma wa baadaye na viongozi wa taifa hili. Ni kweli kizazi kilichopo hakina maadili? Je, kizazi kijacho kitakuwa na maadili? Nani mwenye jukumu la kuelimisha mwingine juu ya hilo?
Mwandishi ni mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Mwanza.
Barua pepe: deojkt@yahoo.com
Simu: 0784-686575

