Udhamini wa TBL kwa Yanga, Simba haulengi kukuza soka Tanzania
August 20, 2008
NAJIKUTA nikiandika makala hii kwa lengo la kutoa maoni na mtazamo wangu kuhusu udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa klabu za Simba na Yanga.
Awali ya yote, naomba nianze kuzungumzia kwanza klabu husika, yaani Simba na Yanga, zenye maskani yao Kariakoo, jijini Dar es Salaam.
Hizi ni maarufu na kongwe nchini kuliko nyingine zilizoanzishwa zaidi ya miaka 70 iliyopita, Yaani Yanga mwaka 1935 na Simba mwaka 1936.
Hivyo, kama ni binadamu, Yanga na Simba, zilipaswa kupewa hadhi ya mtu mzima mwenye uwezo wa kujikimu yeye na familia yake na ikiwa sivyo, basi itakuwa ni bahati mbaya.
Kama mtu huyo angekuwa anajihusisha na biashara au kazi nyingine zozote zile kama za kuajiriwa au kujiajiri na akawa mtu makini katika malengo yake, basi tunaweza kusema kwa kweli maendeleo ya mtu wa umri huo, yangeonekana wazi wazi.
Narudia tena, kwa mtu inaweza kuwa tofauti kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, kwamba mja, hakuweza kubahatika pamoja na jitihada kubwa alizofanya katika maisha yake.
Baada ya utangulizi huo, nirejee kwenye mada yangu kuhusu klabu hizi za Simba na Yanga.
Imekuwa ni kawaida kuona, kusikia au kusoma magazeti, redio au televisheni habari mbalimbali za klabu hizi za Yanga na Simba, kiasi hata cha kutia kichefuchefu.
Wakati fulani, unaweza kujiuliza hivi hakuna habari nyingine za michezo na burudani zaidi ya Simba na Yanga?
Ukiwauliza wahusika, watakueleza kuwa, habari za klabu hizo ndizo zenye mvuto kwa wasomaji, kwa maneno mengine biashara iko katika klabu hizo na si vinginevyo.
Sina maana kuwa habari nyingine haziandikwi, la hasha; ninachosema ni kile kiwango cha kuandikwa kwake, kwani hakulingani na hizi za Simba na Yanga.
Binafsi sikubaliani hata kidogo na dhana hiyo, haingii akilini mwa mtu makini kila wakati kuona habari za klabu mbili tu za Simba na Yanga zikipewa umuhimu mkubwa kuliko nyingine.
Kila kukicha, habari zenyewe ni migogoro ya uongozi, wanachama, posho za wachezaji, mikataba na madudu mengine ambayo yamekuwa sehemu ya maisha ya klabu hizi hata kutia aibu.
Imewahi kutokea hata baadhi ya viongozi wa serikali, hususan wenye dhamana ya michezo, kupoteza muda au hata kutumia fedha za walipa kodi kujiingiza katika kutatua migogoro binafsi ya klabu hizi.
Si vibaya kwa kiongozi wa kitaifa kama waziri kufanya hivyo, lakini ninachohoji hapa ni kiongozi husika kufanya hivyo akiwa kama waziri au kiongozi wa kitaifa ndani ya ofisi za umma huku akitumia rasilimali za umma.
Binafasi, ninatoa ushauri kwa viongozi wa aina hiyo kwamba hata kama ni shabiki wa klabu mojawapo ya hizi mbili kwa sababu si kosa, basi afanye hivyo kama mtu binafsi.
Na hata anapoamua kwenda kuhudhuria mechi za timu hizo au nyingine, isipokuwa timu ya taifa, aende kwa gharama zake kama mashabiki na wapenzi wengine wanavyofanya si kwa kutumia fedha za walipa kodi.
Nimelazimika kuyasema haya yote kwa kuwa hizo ni klabu kama zilivyo nyingine, hazina sababu ya kupewa kipaumbele cha ziada tofauti na timu zingine, tofauti na ilivyo kwa timu ya taifa.
Kama akifanya hivyo kwa timu ya taifa, ni sawa kabisa na si kwa timu ya taifa ya mpira wa miguu pekee, bali kwa michezo yote.
Inasikitisha kuona michezo mingine hususan timu za taifa za michezo mingine zikiachwa bila msaada wowote.
Hapa tunawaona viongozi wa juu wa serikali wenye dhamana ya kusimamia michezo wakijikita kwenye klabu binafsi, hii si sawa.
Juni mwaka huu, kulikuwa na michezo ya riadha ngazi ya taifa mkoani Singida, ambayo kila mmoja alisikia ilivyoendeshwa katika mazingira magumu ya ukata, hali iliyofanya kuwe na huduma duni.
Hali hiyo ilisababisha hata vyama vya michezo kutaka kuhamisha michezo hiyo kwenda mkoa mwingine, wakidhani hiyo ingekuwa suluhisho la tatizo.
Nakumbuka fedha ambazo zilihitajika kufanikisha yale mashindano ya kitaifa, zilikuwa ni kati ya sh mil. 30-40, ambazo waandaaji hawakuwa nazo.
Baada ya kuhangaika kwa muda mrefu wakitafuta wadhamini, hatimaye mashindano hayo yalifanyika, lakini katika hali duni mno.
Tulisikia wanariadha wakilalamika kufanya mazoezi bila hata kula, hii ni aibu kubwa na fedheha kwa wizara husika.
Ni aibu kwa sababu ni mashindano ambayo yalijulikana na hakuna asiyejua umuhimu wa mashindano yale ya taifa ambayo hukutanisha nyota wa mikoa yote ya Bara.
Aidha, tumeshuhudia Ligi Daraja la Kwanza ya netibali 2008 iliyofika kikomo kwa Jeshi Stars kutwaa ubingwa ambayo kutokana na ukata, timu nane zilishindwa kushiriki.
Kwa kushindwa kushiriki, kwa sasa zinalazimika kulipa faini ya sh 300,000 kila moja kama zinataka kuepuka kushuka daraja, huku zikipewa muda wa kukamilisha hilo hadi Agosti 30.
Kadiri itakavyokuwa, hakuna timu isiyopenda kushiriki mashindano kwani ndiyo mantiki ya uwepo wake, lakini ukata ndiyo tatizo kubwa.
Tujiulize kitu kimoja, kama timu ilishindwa kushiriki mashindano kwa kukosa fedha, hizo za kulipa faini zitatoka wapi?
Yote haya yangeepukwa kama Ligi ya Netiboli ingekuwa na wadhamini kama vile TBL katika kukuza mchezo huo nchini ambao ni ajira kwa vijana.
Baada ya kueleza hayo, kama kweli TBL lengo lao si biashara, walikuwa wapi kusaidia mashindano kama yale ya riadha mkoani Singida au Ligi Daraja la Kwanza netiboli ?
Aidha, kama kweli lengo la TBL ni kuinua kiwango cha michezo Tanzania kwa maana michezo ni ajira, walikuwa wapi kusaidia timu ya Tanzania iliyokwenda kushiriki michezo ya Olimpiki inayoendelea Beijing, China?
Nakumbuka namna viongozi wa vyama vya michezo hata Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), walivyokuwa wakihaha kusaka fedha za kuandaa timu na kuisafirisha.
Kama TBL haikuwa na fedha za kusaidia timu ya Olimpiki na mashindano ya taifa ya riadha kule Singida, hizo za kumwaga kwa Yanga na Simba zimetoka wapi?
Tuna haki ya kuhoji kwa kuwa TBL, ni kampuni ya umma, hivyo pamoja na kusaidia mchezo wa kikapu, ina wajibu wa kuangalia michezo mingine pia kama lengo ni kukuza michezo kwa ujumla.
Ukija katika kikapu, TBL imedhamini ligi yote na siyo timu moja na ndiyo maana najiuliza kwa nini TBL wasitoe udhamini kwa timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu kama ilivyo kwa wenzao wa Serengeti Breweries kwa timu ya taifa, Taifa Stars?
Na hiki ndicho kinanifanya nieleze hisia zangu kwamba kwa kitendo cha kudhamini timu mbili kati ya 12 katika ligi, si kukuza soka bali ni kujielekeza katika biashara zaidi.
Kama TBL ina uwezo wa kutoa sh bil. moja kwa mwaka kwa Simba na Yanga kwa muda wa miaka mitatu, imeshindwa nini kudhamini ligi hiyo kwa manufaa ya timu zote?
Chini ya mkataba kati ya TBL na klabu za Simba na Yanga, sh mil. 754 kati ya sh bil. moja kwa kila klabu, zitakuwa kwa ajili ya timu huku nyingine ni kwa ajili ya uendeshaji.
Hapa sasa ndipo ninapothibitisha tena yale niliyoyasema awali kwamba, hii ni kampuni ya umma, ingawa imebinafsishwa kwa kiasi fulani, lakini serikali ingali na hisa zake.
Hisa hizo za serikali, ni fedha za walipa kodi. Sasa iweje TBL ijiingize kwenye udhamini wa klabu mbili tu katika ligi moja na kuziacha nyingine?
Nirudie tena, hii ingekuwa kampuni ya mtu binafsi, nisingelalamika. Kwa mantiki hiyo, kauli ya TBL kupitia kwa Mkurugenzi wa Masoko, David Minja, kuwa, udhamini wao kwa Yanga na Simba umelenga kukuza kiwango cha soka nchini, ni kichekesho.
Migogoro isiyoisha kila siku pamoja na Yanga kugomea mechi, kulikoiletea aibu Tanzania kwenye Kombe la Kagame!
Nikija kwenye hoja ya kukuza soka, hivi udhamini wa timu mbili kati ya 12 ndiko kukuza soka?
Hivi kwa mfano timu nyingine zikajitoa katika Ligi Kuu (sipendi litokee), Yanga na Simba zitabaki peke yao zikicheza ligi?
Ni wazi, ikiwa hivyo hata hicho kiwango kinachoelezwa kwa Yanga na Simba, hakitaonekana, kwa sababu bila hizo zinazobezwa na TBL, umahiri wa Yanga na Simba hauwezi kuonekana.
Aidha, kama kweli lengo la TBL, ni kukuza soka, kwa nini hizo fedha zisielekezwe katika programu ya soka ya vijana kuanzia shuleni kwa nchi nzima?
Huko ndiko ambako vipaji vinapaswa kuibuliwa na kukuzwa kama ambavyo sera ya michezo ya serikali kuhusu michezo shuleni ilivyoeleza.
Jingine tunalopaswa kujiuliza ni kwamba, hivi kwa umri wa Simba na Yanga, zinapaswa kubebwa kwa mbeleko?
Hatukatai kubebwa kwao, lakini na wengine nao wabebwe kwa sababu ni wachanga kuliko wao, hivyo kama udhamini huu ungekuwa kwa timu zote za Ligi Kuu, ile dhana ya kukuza kiwango cha soka, ingekuwa imetimia na hakuna mtu ambaye angehoji.
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
One Response to “Udhamini wa TBL kwa Yanga, Simba haulengi kukuza soka Tanzania”
Got something to say?


nakubaliana na wewe kabisa, kama ni binadamu simba na na yanga ni watu wazima waliokomaa, na kwa level ya ligi yetu tunaweza kusema timu hizi ndio zenye uzoefu mkubwa na zimefika mbali kisoka.
Sasa hii dhana ya TBL kwamba inaendeleza soka haileti maana kamili iwapo inaendeleza soka kwa kudhamini timu mbili ambazo ziko more adavanced kuliko wengine, nilifikiri badala yake ingedhamini timu zingine changa kwenye ligi kuu ili kuleta ushindani zaidi, hivi leo ukizungumzia ubingwa ligi kuu lazima awepo simba au yanga sasa hapa exitement ya ligi kuu inakuwa ni hizo timu mbili tu, na ukipima maendeleo unaangalia kuanzia level ya chini an kuieta juu.