Tusikubali misaada na sifa za matusi

November 18, 2007

KATIKA mahusiano ya kimataifa, falsafa ya kutoa na kupewa inajumuisha wajibu, rushwa, fadhila, uporaji na biashara. Hakuna misaada ya nchi kwa nchi pasipo maafa. Msaada kwa binadamu asiye mlemavu, au kwa nchi isiyokuwa na maafa, ni tusi la nguoni.

Ni tusi la kuwakwaza wabunifu ili wasitumie akili zao kujiletea maendeleo. Pengine misaada inachukiwa kwa sababu, fahari ya kuishi ni kufanya kazi na kujitegemea.

Ndiyo maana baba wa kaya maskini hawezi kukubali baba tajiri ampe mkewe misaada, na wala mama wa kaya maskini hawezi kukubali mama tajiri ampe mumewe misaada. Maumbile yanawataka wanaojiweza watoe misaada kwa wasiojiweza, yaani walemavu, wagonjwa, wazee na watoto. Vitabu vitakatifu havijaamuru nchi tajiri zisaidie nchi zinazofinyanga umaskini.

Tunahoji kwamba, nchi tajiri zina wajibu wa kutoa sehemu ya utajiri kwa nchi maskini, kama ilivyo wajibu wa watu tajiri kutoa sehemu ya utajiri kwa maendeleo ya nchi zao.

Utajiri unapatikana kwa kupora jasho la maskini, na kwa maana hiyo ni wajibu wa matajiri kurudisha sehemu ya jasho hilo ili maskini wasigutuke wakadai haki yao kwa nguvu. Anayebisha kwamba utajiri hautokani na kupora jasho la maskini, ahamie kwenye kisiwa, halafu aone kama atakuwa tajiri kwa jasho lake mwenyewe. Uchumi wa nchi tajiri utaporomoka kama zitawekewa vikwazo vya kuthibiti uporaji wa rasilimali za nchi maskini.

Maskini ni binadamu aliyekosa kiungo muhimu cha kufanya kazi. Binadamu wazima wasiotaka kufanya kazi wamelaaniwa wasile. Kwa mtazamo huo, umaskini wa nchi haupo, maana hakuna nchi iliyokosa kiungo cha kufanya kazi. Utajiri wa nchi unatokana na matumizi bora ya bongo za wananchi wake, na Mwenyezi Mungu amezijalia nchi zote bongo za kutosha kujipatia utajiri. Tofauti ni kwamba, nchi nyingine zinatawaliwa na ubinafsi, unaozifanya zifinyange umaskini kwa kukataa kutumia bongo za watu wake kwa ufasaha.

Ni makosa kuita matoleo yenye masharti �misaada�. Matoleo ya namna hiyo ni rushwa. Laiti kama wachumi wa nchi maskini wangechambua undani wa masharti ya matoleo ya nchi tajiri, wangegundua kwamba yameficha makucha ya uporaji wa rasilimali za nchi hizo. Ndiyo maana umaskini unazidi kuota mizizi katika nchi kama Tanzania, licha ya kupokea kinachoitwa misaada, kutoka pande zote za dunia ya mataifa tajiri, kwa zaidi ya miaka arobaini na tano.

Ni makosa kuita matoleo yanayosukumwa na urafiki wa viongozi, �misaada�. Matoleo ya aina hiyo ni fadhila inayoweza kuwa ahsante kwa mauzo ya siri ya rasilimali za nchi maskini. Kwa mfano, kiongozi wa nchi maskini anaweza kufanikisha mauzo ya migodi ya madini ya nchi yake, kwa viongozi wa nchi tajiri, halafu akapewa fadhila kwa kazi hiyo. Fadhila inaweza kugawanyika katika mafungu mawili, moja la kibinafsi, na la pili likiwa ni matoleo yaitwayo misaada kwa nchi.

Ni makosa kuita marejesho ya sehemu ya faida �misaada�. Biashara za kidhalimu baina ya nchi tajiri na nchi maskini zinaweza kuzipatia nchi tajiri faida kubwa mno, kiasi cha kuwajibika kurejesha sehemu ya faida hiyo kwa nchi maskini, lengo likiwa ni kujenga mazingira bora zaidi ya kukuza biashara hizo, pamoja na kuibua biashara mpya za kidhalimu. Huu ni wajibu wa nchi tajiri kwa raia wake, wanaofanya biashara na nchi maskini.

Ni makosa kuita ujenzi wa miundombinu, katika nchi maskini, �misaada� kwa sababu miundombinu hujengwa kwa ajili ya kufanikisha uporaji wa rasilimali. Kwa mfano, ujenzi wa barabara ya lami kwa ajili ya kusafirisha dhahabu kutoka migodini kwenda uwanja wa ndege, hauwezi kuwa msaada. Ujenzi wa zahanati kwa ajili ya kutibu wafanyakazi katika shamba la miwa linalomilikiwa na wageni, hauwezi kuwa msaada. Hata ujenzi wa reli enzi zile za ukoloni haukuwa msaada. Reli zilijengwa kwa ajili ya kusafirisha mali ghafi, kama pamba, kwenda ulaya. Kung�olewa kwa reli ya Mtwara na Mpanda ni kielelezo hai. Rasilimali zilizokuwa zinaporwa ziliisha.

Ukweli ni kwamba, matoleo ya nchi tajiri kwa nchi maskini ni moja kati ya wajibu, rushwa, fadhila, uporaji, ama biashara ya kidhalimu. Kwa mfano. matoleo ya kufadhili wasomi, kutoka nchi maskini, katika vyuo vya nchi tajiri, ni uporaji wa rasilimali bongo. Uvumbuzi wa wasomi hao una thamani maradufu kulinganisha na gharama za ufadhili. Kama utafiti unahusu viwanda vya nchi tajiri, basi matokeo yake yatatumika kuboresha viwanda hivyo.

Kama utafiti unahusu uchumi wa nchi maskini, basi matokeo yake yatatumika kubuni mbinu bora zaidi za nchi tajiri kupora rasilimali za nchi hizo maskini. Kitendawili ni kwamba, nchi maskini zinatuma wanafunzi wake kwenda nchi tajiri kupata shahada, bila kujali ni ya kitu gaini.

Kama vile kashfa hiyo haitoshi, wasomi wanaporudi wanahamasishwa wafanye tafiti kwenye eneo lolote, hata kama halina maslahi kwa taifa lao kwa miaka elfu moja ijayo. Ndiyo maana hatuoni aibu kuendelea kupokea fedha kutoka nchi tajiri kwa ajili ya kufadhili tafiti za wasomi wetu. Hii ni kashfa inayoimarisha mila ya kutegemea wageni.

Tunahoji kwamba, matoleo mengi, yanayoitwa misaada kwa makosa, ni ya kulemaza bongo za wazalendo ili zisinzie milele. Ni sindano za usingizi, tunazodugwa kila tunapoonyesha dalili za kuamka. Kwa kuwa mishipa ya fahamu ya nchi ni viongozi wake, wataalam wa kudunga sindano hizo wanawatafuta kwanza viongozi wa nchi maskini. Wataalam wa uporaji wanaweza kuwamwagia viongozi hao sifa za matusi, ama kuwapa rushwa, kama hatua ya kuwaandaa kudungwa sindano za usingizi.

Kwa mfano, katika karne hizi za sayansi na tekinolojia, ni matusi kwa nchi tajiri kumsifu kiongozi wa nchi maskini kwa jitihada za kujenga shule za msingi au visima vya maji, au kwa kukaribisha wawekezaji kutoka nchi tajiri. Wanatakiwa wasifiwe kwa kupora tekinolojia kutoka nchi tajiri, na kwa kujenga viwanda vinavyomilikiwa na wazalendo.

Matoleo ya nchi tajiri kwa ajili ya kujenga vibarabara vidogo, au visima vya maji, au vyoo, au madarasa, katika nchi maskini, ni kashfa ya ubaguzi wa bongo. Kunaashiria kwamba, wabongo hawana uwezo wa kufanikisha ujenzi huo, na wala hawajui matumizi bora ya fedha za kigeni. Je, ni vipi tulipiga vita ubaguzi wa rangi, halafu tunaruhusu ubaguzi wa bongo? Rangi ilibaguliwa, halafu ikakombolewa na bongo. Je, ubongo ukibaguliwa, utakombolewa na nani?

Mahusiano sahihi kati ya nchi na nchi ni ya biashara za kistaarabu. Hizi ni biashara za uwazi na za kutumia mbinu za kisayansi kuchambua faida na hasara. Kwa maana hiyo, ni biashara za kutokomeza umaskini. Tatizo ni kwamba, ubinafsi wa viongozi wa nchi maskini unafungua milango kwa waporaji. Siku zote, lengo la mfanyabiashara ni kupata faida kubwa iwezekanavyo, na kwa maana hiyo waporaji hawawezi kulaumiwa ikiwa watakuta milango wazi usiku.

Viongozi wa nchi maskini wanapaswa wajiulize maswali kadhaa, na wapate majibu, kabla ya kupokea matoleo yanayoitwa misaada. Maswali hayo yanajumuisha yafuatayo. Je, ni kwa nini zinapewa misaada angali nchi hizo siyo vilema?

Je, wanaozipatia misaada wanataka kupata nini? Je, mila ya ombaomba itayafikisha wapi mataifa maskini? Je, ni taifa lipi liliondokana na umaskini kwa kukumbatia sera za ombaomba? Je, nchi maskini zitakwepaje athari za kukimbilia misaada? Shida ni mama wa maarifa, na kamwe nchi haiwezi kupata maendeleo kama wataalam wake watawekwa kando katika ufumbuzi wa matatizo ya nchi.

Viongozi wa nchi maskini wanatakiwa waelewe kwamba, misaada pasipo maafa ni rushwa ya kuandaa mazingira ya kuuza nchi. Waelewe kwamba, rushwa inatumika kulinda rushwa. Je, ni mbinu gani zitumike kuvunja miduara ya rushwa?

Tunanena kwamba, matatizo ya kiuchumi yanayozikabili nchi maskini yanajikita kwenye miduara ya rushwa. Kwa kuwa rushwa na ubinafsi ni kaka na dada, vita dhidi ya rushwa haiwezi kufanikiwa kama wenye dhamana ya kutokomeza rushwa watakuwa na chembechembe za ubinafsi au rushwa.

Je, mamlaka zinazoteuwa wataalam wa kutokomeza rushwa zinaweza kuwa takatifu, halafu zikateuwa wataalam walarushwa? Tunahoji kwamba kuwepo, na kuendelea kuwepo kwa walarushwa miongoni mwa wataalam wa kutokomeza rushwa, ni ushahidi tosha kwamba, mamlaka zilizowateuwa ni za walarushwa.

Kwa upande wa Tanzania, ni vema kama wakuu wa nchi watahakikisha kwamba, wataalam wa TAKUKURU ni watakatifu katika upokeaji na utoaji rushwa. Vinginevyo watajipaka matope, maendeleo hayatakuwepo, na tutaendelea kunyanyaswa na wageni wanaotumia mbinu chafu kwa ajili ya kuhalalisha uporaji wa rasilimali zetu. Nchi maskini zinahitaji viwanda, zinahitaji sayansi na tekinolojia, na zinahitaji uhuru wa kutumia bongo za wazalendo kutatua matatizo ya nchi.

Profesa Leonard K. Shayo ni mtaalam wa Hisabati na Program za Kompyuta


Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post
 |  TrackBack URI for this post

Comments

Got something to say?