TBF Barrick Gold Cup 2007 sawa, lakini….

October 29, 2007

OKTOBA 20 hadi 26 mwaka huu, kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, jijini Dar es Salaam, kulifanyika mashindano ya mpira wa kikapu kuwania Kombe la Taifa ‘Barrick Gold Cup 2007′ na kushirikisha mikoa 11 huku timu za kombaini ya Mkoa wa Dar es Salaam ‘The Dream Teams’ zikishuhudiwa zikitetea mataji yao. Mashindano hayo yaliyodhaminiwa na Kampuni ya Barrick Gold na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro, yalifunguliwa Oktoba 20 na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Nkaya Bendera, na kushuhudiwa na timu nyingi zikionyesha upinzani wa hali ya juu.

Mbali ya wachezaji wengi kuonyesha vipaji vya hali ya juu, pia mashindano hayo yalivuta mashabiki lukuki tofauti na mashindano mbalimbali yanayohusisha mpira wa kikapu, yanapofanyika sehemu mbalimbali.

Dar es Salaam, wanaume na wanawake, waliibuka kidedea baada ya kuwatoa nishai wapinzani wao wa jadi ‘The Rock City’ ya Mwanza kwa pointi 100-79 kwa wanaume huku katika fainali ya wanawake wakitetea ubingwa wao dhidi ya Shinyanga, baada ya kuibuka na ushindi wa pointi 58-27.

Mikoa mingine iliyoshiriki mashindano hayo ni pamoja na Tabora, Arusha, Mwanza, Pemba, Mbeya, Unguja, Shinyanga, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Dodoma na Lindi.

Dalili za The Dream Teams, kutetea ubingwa wao zilianza kuonekana mapema, baada ya kuanza kwa kishindo kwa kuwanyuka Morogoro kwa pointi 122-44 kabla nusu fainali kuwagaragaza Mbeya 94-55.

Nafasi ya pili kwa upande wa wanaume ilinyakuliwa na Mwanza huku mshindi wa tatu ikiibuka Unguja kwa upande wa wanaume, huku kwa wanawake nafasi ya pili ilinyakuliwa na Shinyanga na kufuatiwa na Mwanza.

Katika mashindano hayo wachezaji wengi walionyesha uwezo wa hali ya juu, lakini baadhi yao ni Nelly Anyingisye na Elizabeth Masenyi wa Dar es Salaam, Marry Meshacky na Levina Julius wa Shinyanga.

Kwa upande wa wanaume ni pamoja na Juma Kisoki wa Mwanza, Edmund Pastory na Mohammed Ally ‘Dibo’ wa Dar es Salaam na Frank Mlelwa wa Ruvuma.

Licha ya mashindano hayo ambayo yalikuwa yakipigwa kalenda mara kwa mara, kutokana na kukosekana kwa wafadhili, kufana lakini yalikumbwa na upungufu kadhaa, ambao kwa namna moja ama nyingine ulipunguza ufanisi.

Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), awali kabla ya mashindano hayo lilitangaza baadhi ya mambo ambayo, litayafanya kwa timu shiriki ikiwamo kutoa posho, malazi na vifaa, lakini hayo hayakufanywa kama ilivyokuwa imetangazwa awali na kuzusha usumbufu, manung’uniko na malalamiko kutoka kwa mikoa shiriki.

Baadhi ya viongozi wa timu za mikoa walitoa malalamika kadhaa ingawa kwa masharti ya kutotajwa majina, wakisema kwamba maandalizi yalikuwa mabovu na kuwashauri viongozi wa TBF, kujitahidi mashindano mengine kujipanga na kutafuta wadhamini wengi ambao watamudu gharama na kuepusha malalamiko yasiyo na msingi.

Viongozi hao, walieleza kuwa waandaji wa michano hiyo awali waliwaahidi kutoa posho ya sh 10,000, lakini walipunguza dakika za mwisho na kutoa sh 8,000 kwa wachezaji, huku viongozi wakipewa sh 10,000 na wachezaji waliotoka mikoa ya jirani na Dar es Salaam walilipwa sh 3,000 kwa siku.

Mbali na upungufu huo katika masuala ya posho, pia dosari ya udhibiti wa wachezaji kwa timu husika, ulikuwa hafifu na kusababisha timu nyingi kuchezesha wachezaji wa kukodisha, maarufu kama mamluki, ambao wengi wao walikuwa wakitoka jijini Dar es Salaam.

Pia madai ya mikoa ililaumiwa kwa kuchezesha wachezaji ambao si raia wa Tanzania, ambako Mkoa wa Morogoro ulilaumiwa siku ilipokipiga na Mwanza na kuibuka na ushindi wa pointi 52-27.

Timu hiyo ya Mwanza wanawake iliamua kukata rufaa dhidi ya wapinzani wao, kwa kuwatuhumu kumchezesha mchezaji huyo Jascar Loziuk, waliyedai ni raia wa Canada.

Kadhalika hali ya usalama ndani ya uwanja ulikuwa hafifu na kusababisha baadhi ya mashabiki waliokuwa wakizidiwa na pombe kuingia na chupa na kuleta vurugu, na kusababisha shabiki mmoja kujeruhiwa vibaya kwa chupa ya bia.

Akizungumzia upungufu huo, Makamu wa Rais wa TBF, Musa Mziya alikiri na kuahidi kuyafanyia kazi na kwamba mashindano yajayo watahakikisha wanafanyia kazi upungufu huo ili kuboresha ufanisi.

TBF inatakiwa kujifunza kutokana na makosa na kuhakikisha kuwa masuala mbalimbali ikiwamo ulinzi unakuwepo pamoja na masuala mengine ya utawala