TANESCO ilivyofikishwa ICU
March 25, 2008
SHIRIKA la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) lipo taabani kuichumi, kiasi cha kushindwa kuzalisha umeme unaotakiwa, na hivyo kuwa wanunuaji wakuu wa umeme kutoka katika kampuni binafsi.
Miongoni mwa kampuni zinazozalisha umeme na kuiuzia TANESCO ni Dowans (zamani Richmond), Aggreko, Songas, IPTL na nyinginezo.
TANESCO inahitaji kiasi cha sh trilioni 1.6 ili iweze kujikwamua na kuweza kuzalisha umeme utakaokidhi mahitaji ya wateja wake pamoja na kufika vijijini na ziada itakayouzwa nje ya nchi ifikapo mwaka 2012 kulingana na malengo yao.
Njia ya kuelekea ICU ilianza mwaka 1996, wakati nchi ilipokumbwa na tatizo la kutokuwa na umeme wa kutosha, kutokana na kutokuwapo kwa maji ya kutosha ambayo ndiyo chanzo kikuu cha uzalishaji wa umeme hapa nchini.
Katika kuhangaika huko ilipatikana kampuni ya kuzalisha umeme wa mafuta ya iliyoitwa Independent Power Tanzania Limited (IPTL) iliyoingia mkataba na Serikali wa kutoa umeme 100MW. Hapo mwanzo ilionekana ni mkombozi mkubwa, lakini mkataba wake ulijaa kila aina ya madudu.
Kampuni hiyo ilipoanza kuzalisha, umeme ulikuja kuonekana ni ghali zaidi na serikali iliamua kuvunja mkataba na kampuni hiyo lakini ikashindwa mahakamani baada ya IPTL kuiburuza mahakamani kwa kuvunja mkataba.
Kushindwa huko kwa serikali kulimaanisha kuendelea kwa mkataba au kulipa gharama zote za ujenzi wa mradi pamoja na faida ambayo ingepata katika kipindi chote cha mradi.
Kutokana na sakata hilo, TANESCO inalizimika kulipa sh billioni 3 kwa mwezi ama inunue umeme au isinunue huku umeme unaozalishwa ukiwa wa bei ya juu na usiohitajika kwa kiasi kikubwa na TANESCO.
Hali hiyo haikuishia hapo bali mwaka 1997, serikali iliamua kuliweka shirika hilo kwenye orodha ya kampuni zitakazobinafsishwa chini ya Taasisi ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC), lakini halikuweza kupata mwekezaji.
Baada ya kuona mambo magumu mwaka 2002, serikali iliamua kuliendesha shirika hilo kwa kukodisha menejimenti (NetGroup Solutions).
Hii ilipingwa vikali na wabunge pamoja na wafanyakazi, lakini kutokana na mitutu ya FFU walilazimika kusalimu amri.
Menejimenti hiyo kutoka Afrika Kusini ilikuwa na watu watano ambao kila mmoja kwa mwezi mshahara wake ulikuwa haupungui milioni 21 na kwa kiasi kikubwa waliamua kuachana na miradi mingi iliyokuwa ikiendeshwa na shirika ikiwamo ya kiwanda cha kuchemsha nguzo na kununua vifaa vya umeme.
Menejimenti hiyo iliamua kuanza kuagiza vifaa mbalimbali kutoka Afrika Kusini kwa kile walichokieleza ni nafuu zaidi kuliko hapa nchini ambapo hutozwa kodi nyingi Kiufupi safari ya ICU ilikolea zaidi katika kipindi cha miaka sita kuanzia mwaka 2002 ambapo shirika hilo limepata hasara ya zaidi ya sh bilioni 500.
Hasara hiyo ni pamoja na kulipa madeni kwa kampuni zilizoingia mikataba mibovu na hewa ya kuzalisha umeme na serikali bila kuangaliwa kwa uwezo na gharama za kampuni hizo katika kuzalisha umeme.
Mwaka 2002 walipata hasara ya bilioni 72.2, mwaka uliofuata sh bilioni 177.6, uliofuata sh bilioni 15, mwaka 2005 milioni 900 huku mwaka 2006 ikivunja rekodi kwa kupata hasara ya bilioni 183 na mwaka jana likipata hasara ya bilioni 72.
Kwa ujumla asilimia 98 ya mapato ya TANESCO huishia katika kampuni za uzalishaji umeme ambazo nyingine hugharimiwa kila kitu kuanzia leseni, bima, kiwanja na mengine na TANESCO ambayo imegeuzwa mti wa mzambarau kwa kila mwenye kikapu kutingisha na kujaza kikapu chake kikijaa huondoka zake.
Kutokana na hali hiyo, shirika hilo hulazimika kuongeza bei ya umeme inaoutoa kwa wananchi ili kufidia gharama wanazozitumia na matokeo ya hali hiyo ni kuzidisha ugumu wa maisha kwa mwananchi wa kipato cha chini.
Pamoja na hali mbaya ya kiuchumi inayowakabili TANESCO, serikali imeamua kuanzisha sheria ambayo itaruhusu kampuni binafsi kuzalisha na kuuza umeme bila kupitia TANESCO kama inavyofanyika hivi sasa.
kimsingi uamuzi huu unatafsiriwa kama njia ya serikali kuiua TANESCO, kwani haina uwezo wa kabiliana na kampuni hizo ambazo zimeonekana kujizatiti vilivyo kuchukua nafasi hiyo huku TANESCO ikiwa hoi bin taabani kifedha.
Uamuzi huo wa serikali unaonekana kupata upinzani mzito kutoka kwa wabunge ambao wameonyesha kupinga katika muswada uliowasilishwa kwao kwenye semina ya kujadili miswada ya sheria mpya za umeme na biashara za mafuta ya petroli iliyofanyika Machi 20, Dar es Salaam.
Kwa ufupi wabunge walisema si sahihi kwa TANESCO kushindanishwa na kampuni hizo na ni mapema mno kwa Tanzania kuwa na sheria ya aina hiyo na kinachotakiwa hivi sasa ni kwa Serikali kuimarisha Shirika hilo.
Mikakati ya kujinasua ICU
Kwa mujibu wa Mkuruenzi Mkuu wa TANESCO, Dk. Idris Rashid, wana mipango ya kununua kampuni ya uzalishaji wa umeme wa mafuta ya IPTL na kuigeuza mitambo yake ili iweze kutumia nishati ya gesi ambayo ni rahisi na hivyo kuzifanya gharama za umeme kushuka tofauti na ilivyo sasa.
Anasema umeme wa mafuta ni ghali zaidi kutokana na uagizaji wake kutegemea soko la dunia na kila mara hupanda kulingana na mahitaji ya soko hilo tofauti na nishati ya gesi ambayo hupatikana hapa nchini.Anasema mpango mwingine ni kununua hisa za Kampuni ya Songas ambayo huiuzia umeme TANESCO, ambapo kila siku TANESCO hutoa sh milioni 200 kwa ajili ya huduma hiyo fedha ambazo zingetumika kuboresha miundombinu ya TANESCO zingesadia kupeleka umeme vijijini.
Anasema ununuzi wa hisa hizo kutawafanya wapunguze gharama za kuilipa Songas na hivyo kuokoa kiasi cha sh bilioni moja kwa mwezi hivyo kujiongezea uwezo wa kiuchumi.
Aidha, alisema mkakati huo kwa sasa upo kwenye hatua nzuri kwani wameshakubaliana na Benki ya dunia kupata kiasi cha fedha ili kutimiza adhma yao hiyo.
Mbali na mpango huo pia kushirikiana na mradi wa makaa ya mawe wa Kiwira ili uweze kuanza kuzalisha umeme wa MW 100 ifikapo mwaka 2010 ili kukabiliana na matatizo ya uhaba wa umeme yanayoweza kutokea kutokana na uhaba wa maji. Anasema mikakati mingine ni kufunga mita za Smart kwenye viwanda ili kuhibiti wizi wa umeme unaofanywa na watu wasio waaminifu na wenye kutaka kutajirika kwa haraka na kwa kutumia njia zisizo halali.
Aidha, anasema mpango huo ni mkakati wa kupunguza upotevu wa umeme kutoka asilimia 23 hadi kufikia asilimia 13 mwaka 2012 na kuongeza wateja 100,00 kila mwaka kutoka wateja 32,000 wapya waliongezeka mwaka jana.
Pamoja na hayo lakini pia alisitiza kuwamulika wafanyakzi wao wanaojihusisha na vitendo vya rushwa vinavyochangia kushusha ufanisi wa shirika pamoja na kulikosesha mapato.
Kuongeza watumiaji wa umeme kutoka asilimia 10 ya hivi sasa hadi kufikia asilimia 15 mwaka 2015.

