Spika Sitta, hili usilinyamazie

March 27, 2008

NINAFUATILIA sana nyendo za kisiasa za Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kwa sababu ni mmoja wa wanasiasa ninaowahusudu. Mimi ni shabiki wake kisiasa! Sipendi apate doa.

Anajua Spika, kama mimi ni mtu wake. Ingawa mawasiliano yetu kwa muda mrefu yamekuwa si ya ana kwa ana, mara nyingi tunawasiliana kupitia kwenye vyombo vya habari, na hii ni kwa sababu wote (mimi na yeye) tuko busy sana.

Mwenzagu yuko busy na shughuli za Bunge, yeye ni Spika wa Bunge, taasisi muhimu na nyeti kabisa katika nchi yetu, ina mambo mengi, hivyo hana muda wa kupiga porojo.

Kama ilivyo kwa Spika, mimi naye niko busy kweli, nina kazi nyingi sana, sina muda wa kupoteza. Lakini kazi inayoniumiza sana ni hii ya kufuatilia nyendo zake za kisiasa.

Nikiwa kama shabiki wake kisiasa, nina kazi nzito ya kufuatilia kila hatua anayopiga, kisha kwa sababu hatuonani uso kwa uso, ninawajibika kuandaa ripoti ya kumpongeza au kumkosoa kulingana na yale anayoyafanya kama mbunge na Spika na kuiwasilisha kwake kwa njia niliyoileza hapo juu.

Kabla sijataka kumwambia ninachokusudia kumwambia katika makala hii, nitangulie kumpongeza kwa namna ya pekee Spika Sitta kutimiza miaka 40 ya ndoa yake. Nilifurahi sana kumuona kupitia mawasiliano yetu yale yale ya habari (katika picha) akichekelea kwa furaha yeye pamoja na mkewe, Mama Sitta. Nampongeza sana.

Wiki iliyopita, vyombo vya habari kadhaa vilitangaza habari zilizonishtua zikimuhusisha Spika Sitta na kashfa mbaya ya matumuzi mabaya ya madaraka aliyonayo ya u-Spika.

Baadaye nikazisoma kashfa hizo kwenye mtandao. Hazikunifurahisha, hivyo nikaamua nitimize wajibu wangu wa kumwandikia Spika. Kama ambavyo nimekuwa nikifanya.

Naandika nikijua kwamba Spika Sitta haamini taarifa zinazosambazwa kupitia mtandaoni, ziwe za kweli au la! Lakini ninatofautiana naye katika hili, kwa sababu mimi huwa sizipuuzi taarifa hizi. Sababu ni moja tu, kwamba mara kadhaa zimekwishathibitika kuwa kweli.

Nimesoma habari zinazodai kwamba Spika Sitta, amekuwa akitumia vibaya fedha za umma na hususan kasma yake ya u-Spika kwa ajili ya masuala yake binafsi.

Habari zinamtuhumu Spika kuwa anamtumia msaidizi wake mmoja kuchota mamilioni ya fedha kwa kisingizio kuwa ni masurufu ya safari za ndani na nje ya nchi, na zinaainisha kulipwa kiasi kikubwa kwa ajili ya safari anazofanya ndani na nje ya nchi, huku akidaiwa kujilimbikizia deni kubwa linalotajwa kufikia sh milioni 60.

Haziishii hapo, zinaendelea zaidi kwamba amekuwa akiyatumia vibaya magari mawili ya Bunge kwa ajili ya matumuzi yake binafsi, na yasiyotambulika kisheria na kikanuni kwa madaraka yake ya u-Spika.

Mlolongo wa tuhuma ni mrefu, unadai zaidi kwamba Spika Sitta anatumia vibaya fedha za Bunge hata kusababisha kamati moja ya kudumu ya Bunge kugundua upungufu huo, na unarudi nyuma na kujaribu kuipekua historia ya utendaji kazi wake wakati akiwa Mwenyekiti wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC).

Katika hilo la TIC, anadaiwa kutumia wadhifa wake kuingia ubia na wafanyabiashara wengi wa kigeni, hata kumwezesha kununua hisa katika kampuni moja ya Kichina inayosafirisha magogo.

Imenichukua siku kadhaa nikitafakari tuhuma hizi, katika kipindi hicho chote nimekuwa nikipima tuhuma hizi katika vipimo tofauti na jibu nililopata katika vipimo vyote, linamtaja Spika Sitta kuwa ndiye mtu pekee anayeweza kutoa ufumbuzi wa tuhuma hizi.

Na nadhani nimekuwa nikipata jibu hili kwa sababu historia ya matukio kadhaa makubwa ya tuhuma za kifisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma ambayo wamekuwa wakielekezewa wakubwa yamekuwa hayatolewi majibu wala ufafanuzi.

Historia inaonyesha kwamba, wapo viongozi wengi waliokwishatuhumiwa na wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali, lakini hata siku moja hawajawahi kujitokeza hadharani kuzizungumzia tuhuma hizo dhidi yao. Wanachofanya ni kukaa kimya mpaka tuhuma zinapofutika au kusubiri waundiwe tume ziwaumbue ndipo wanaanza kulalama.

Kwa Spika Sitta, sitaki ajifananishe na hao wanaokaa kimya wakati wakiandamwa na tuhuma nzito za kukiuka miiko ya uongozi au kwa makusudi kufanya vitendo vya kifisadi.

Ninataka Spika Sitta ajibu tuhuma hizi. Ninataka ajibu kwa sababu sitaki akae kimya na kuwafanya watu waamini kwamba na yeye ni fisadi au kiongozi anayetumia nafasi aliyonayo kujinufaisha yeye binafsi na jamaa au ndugu zake wa karibu.

Sitaki akae kimya kwa sababu akifanya hivyo watu wataamini kwamba alikuwa akitetea wabunge wapewe maslahi manono ili yeye aweze kuneemeka zaidi. Kwa sababu ni wazi kwamba kama wabunge wanalipwa vizuri, yeye atakuwa analipwa vizuri zaidi, hivyo inaweza kuleta hisia kwamba aliamua kutumia mgongo wa wabunge ili afanikishe azma yake ya kujilipa zaidi ya vizuri.

Lakini zaidi ni kwamba, sitaki Spika Sitta akae kimya kwa sababu akiwaiga wenzake wenye tabia kama hiyo, basi Watanzania wanaweza kuamini kwamba wabunge hawataki mishahara yao ifahamike kwa sababu ni mikubwa mno kwa viwango vya mishahara ya Watanzania kiasi kwamba inaweza kuitwa kufuru.

Naamini Spika Sitta hataniangusha, kama ambavyo amekuwa akitoa mwongozo wake bungeni katika hoja zinazowatatiza wabunge, basi hata katika hili atafanya hivyo, atatoa mwongozo kwa Watanzania kwa kufafanua tuhuma moja baada ya nyingine ili wale wanaotaka kumtia doa, washindwe na walegee!