Siwezi kuachia ngazi - Maximo
December 20, 2007
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Mbrazil Marcio Maximo, amesema licha ya kutupiwa lawama na baadhi ya watu, hawezi kung’atuka kwa sababu haoni sababu ya msingi ya kufanya hivyo. Maximo aliyetua nchini Julai 26 na kukabidhiwa Stars Agosti 19, alisema hawezi kuachia ngazi hadi pale mkataba wake utakapofika ukomo.
Maximo aliyasema hayo jana katika ofisi yake iliyoko makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Karume jijini Dar es Salaam, huku akiaga kwenda kwao Brazil kwa mapumziko ya Krismasi na mwaka mpya.
Alisema hawezi kuachia ngazi kwa sababu hakuna sababu ya msingi hata kuamua hivyo kwa sababu kwa kipindi cha miezi 16, ameipandisha soka ya Tanzania ingawa wengine hawaoni.
Alisema kwa wenye kuijua soka na kuona mbali, wakiwamo waajiri wake, wanaona ni kwa jinsi gani amebadili kiwango cha soka ya Tanzania.
Maximo alisema, inawezekana baadhi ya watu wanamkosoa kwa kutojua, hivyo hawachukii kwa hilo, kwani ipo siku watabaini ukweli na kufurahia matunda ya mafanikio.
“Baadhi ya mashabiki wanasema ning’atuke, siwezi! Mimi si kocha wa ‘bla bla’, ni kocha ninayejua kitu gani ninafanya kwa timu yangu… sifanyi kazi hii kwa kubahatisha, nitang’atuka pale itakapoonekana kuna ulazima wa kufanya hivyo,” alisema Maximo kwa kujiamini.
Alisema, anashangazwa na baadhi ya mashabiki, ambao hawataki kuukubali ukweli kwamba, kadiri siku zinavyokwenda, vijana wake wanazidi kuimarika, hivyo ipo siku Tanzania itapaa kisoka.
Maximo alisema, wakati anakuja nchini, aliikuta Tanzania ikiwa nafasi ya 167, lakini baada ya miezi 16, Tanzania ni ya 89 na kuongeza kuwa hata hivyo hilo halionekani.
“Niliikuta Tanzania iko nafasi ya 167, katika rekodi ya kimataifa, leo hii Tanzania ni ya 89, bado naonekana sifai… ni kweli?” alisema na kuhoji.
Hata hivyo, alisema hashangazwi sana na hilo, kwani duniani kote wapenzi wa soka wana kasumba ya kusahau kwamba soka ni tofauti na utabiri, soka ina kushinda, sare au kufungwa.
Alisema, ingawa Kilimanjaro Stars imetolewa katika robo fainali ya michuano ya Chalenji, lakini amefarijika na kiwango cha vijana wake.
“Ninakwenda Brazil kwa mapumziko mafupi kwa ajili ya Krismasi na Mwaka Mpya na nitarudi Januari 15,” alisema Maximo.
Alisema, akiwa Brazil atajitahidi kuonana na Rais wa Shirikisho la Soka nchini humo, kuomba mechi ya kirafiki na Brazil kabla ya fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.
Maximo alisema kinachomshangaza ni hatua ya mashabiki hao kulaumu kukosekana kwa nyota wa Yanga na Simba wakati awali walipiga kelele waachwe.
Alisema anaamini kupitia michuano ya Chalenji, vijana wake wamezidi kuimarika kwa ajili ya kujenga kikosi bora cha siku za usoni.
“Wachezaji hawa ni hazina ya taifa, ukiangalia viwango kama vya Uhuru Selemani, Castory Mumbala, Ally Mustapher, Sango Magae na wengine, vimezidi kuimarika,” alisema.
KUTOKA: TANZANIA DAIMA
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

