Simba, Yanga zisitafute mchawi
April 7, 2008
APRILI 5 na 6, zitabaki kuwa kumbukumbu, kwani ndizo siku ambazo mbio za Simba na Yanga katika michuano ya kimataifa zilifika ukingoni, baada ya kufungwa katika mechi zao za marudiano.
Yanga iliyokuwa ikihitaji ushindi wa aina yoyote au sare dhidi ya Al Akhdar ya Libya, ikicheza mbele ya mashabiki wake, ilisalimu amri kwa kunyukwa bao 1-0, hivyo kung’olewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho kwa jumla ya mabao 2-1.
Yanga iliyong’olewa katika raundi ya pili, katika raundi ya kwanza, ilifanikiwa kuing’oa AS Adema ya Madagascar na kama ingeshinda, ingetinga raundi ya tatu ya michuano hiyo.
Siku moja baada ya Yanga kung’olewa, watani wao Simba nao wamefuata nyayo baada ya kufungwa jumla ya mabao 7-1 katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo Tanzania kwa sasa kutokuwa na timu yoyote katika michuano ya kimataifa.
Katika mechi yake ya kwanza iliyopigwa kwenye dimba la Aba, Nigeria, Simba ilifungwa mabao 4-0, hivyo jana ilishuka katika dimba la taifa, ikihitaji ushindi wa mabao 5-0.
Kwa mazingira hayo, Simba imetupwa nje ya michuano ya kimataifa, hivyo zinarejea katika Ligi Kuu ya Bara, iliyo katika ngwe ya lala salama katika mbio za kusaka ubingwa na nafasi za uwakilishi kwa msimu ujao.
Kabla ya Yanga na Simba zilizong’olewa katika raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa, timu za Miembeni na Chipukizi za Zanzibar, zilikuwa za kwanza kuaga katika raundi ya kwanza ya michuano husika.
Miembeni iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, ilifungwa na Mamelodi Sundows ya Afrika Kusini huku Chipukuizi ikiondoshwa katika Kombe la Shirikisho na Green Buffaloes ya Lusaka, Zambia.
Kimsingi, hakuna anayefurahia hali hii kwani matarajio ya wengi ilikuwa ni kuona timu hizi zinafika mbali katika michuano ya kimataifa, kwani mbali ya masilahi yanayoweza kupatika kwa timu husika kufanya vema, pia ni fursa kwa wachezaji kujitangaza.
Hata hivyo, tukiwa sehemu ya wadau wa michezo na maendeleo kwa ujumla, tunatoa wito kwa wachezaji wa timu zote mbili kwamba hawapaswi kukata tamaa, badala yake kushindwa kwao uwe mwanzo wa kujipanga vema kwa msimu ujao.
Ni wakati muafaka kwa viongozi wa klabu za Simba na Yanga, kukaa chini na kufanya tathmini ya kina ili kubaini sababu za kitaalamu zilizochangia kufanya vibaya kwa timu zao katika michuano hiyo ya kimataifa.
Tunaamini kama pande husika zitapata jawabu sahihi la kile kilichosababisha timu zao zikafanya vibaya, utakuwa mwanzo mzuri wa kujipanga vema kwa msimu ujao, vinginevyo itakuwa ni rahisi kurejea katika makosa ya kila mwaka.
Tunaamini, Simba na Yanga, ni timu zilizo chini ya makocha wenye utaalamu wa kutosha katika ufundishaji na viongozi wenye uzoefu mkubwa, hivyo ni wakati sasa wa kuketi pamoja na kuangaliwa chanzo cha tatizo.
Hata hivyo, ingawa kufungwa huchangiwa na sababu nyingi, lakini kwa timu kukosa maandalizi ya uhakika, huwa ni sababu kubwa kwa timu kufanya vibaya.
Maandalizi tunayozungumzia hapa, ni aina ya wachezaji waliomo katika timu, ubora wa makocha walioko katika timu na mwishowe, aina ya maandalizi yanayofanyika ambayo kimsingi hupaswa yalingane na mashindano husika.
Ni kituko kwa timu ya Simba au Yanga inayojiandaa kucheza na timu kama Enyimba au Al Akhdar, zikajipima na timu za ‘mchangani’, kwani huko kutakuwa si kujiandaa kushinda, isipokuwa ni kujiandaa kushindwa.
Kutokana na kipigo hiki, Simba na Yanga, zinapaswa kuketi chini kujiangalia kama maandalizi yaliyokuwa yamefanyika katika kujiandaa kwa mechi za kimataifa yanalingana na ugumu wa mashindano yenyewe.
Kama Simba na Yanga, zitajiridhisha kwamba, zilikuwa zimejiandaa vema kiufundi, basi zijiangalie pia katika maeneo mengine, kwa sababu, suala la ushindi au kushindwa kwa timu, huchangiwa na vitu vingi.
Tunamaliza maoni haya, tukiwasihi viongozi na makocha wa Simba na Yanga, kutokata tamaa kwa kuondoshwa katika michuano ya kimataifa, badala yake matokeo haya yawe changamoto ya kujipanga upya kwa msimu ujao.

