Siku 15 za Zombe
May 27, 2008
HATIMAYE kesi ya mauaji yaliyotokea zaidi ya miaka miwili iliyopita, inayomkabili aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam, (ACP), Abdallah Zombe, imeanza kunguruma katika Mahakama Kuu ya Tanzania, kwa mashahidi wawili wa upande wa mashitaka, mtu na mkewe, kuanza kutoa ushahidi.
Katika siku ya kwanza ya kusikilizwa kwa kesi hiyo jana, shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka, Alex Ngonyani, aliieleza mahakama kuwa wafanyabiashara wa madini waliouawa, walikuwa na madini yaliyokuwa na thamani ya kati ya sh milioni 150 na sh milioni 200.
Aidha, shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa pamoja na madini hayo, wafanyabiashara hao, ambao walikuwa rafiki zake kutokana na kufanya shughuli moja, walikuwa na fedha taslimu sh milioni 18.
Akitoa maelezo yake mbele ya Jaji Salum Masati, Ngonyani alidai wafanyabiashara hao aliofahamiana nao tangu mwaka 1990, kuwa ni Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi au ‘Jongo’ na Mathias Lunkombe, waliokuwa na madini aina ya spin na rubi, yenye thamani isiyopungua kiasi hicho cha fedha hadi siku ya tukio walipokamatwa na polisi, wakituhumiwa kuwa ni majambazi.
Aliendelea kueleza mahakamani hapo kuwa, siku ya tukio, rafiki zake walikuwa wakitokea nyumbani kwake Sinza, ambako alikuwa amewaagiza kumpelekea fedha za matumizi mkewe na baada ya muda mkewe aliyemtaja kwa jina la Bernadeta, alimpigia simu na kumweleza kuwa marafiki zake hao wamekamatwa na polisi kwa madai kuwa ni majambazi.
Aliendelea kueleza kuwa, baada ya kusikia taarifa hizo, alijitahidi kuwasiliana na rafiki zake kwa kuwapigia simu, lakini hakufanikiwa kuzungumza nao, kwa sababu simu zao zilikuwa zimezimwa.
Alisema alipiga simu kwa mmiliki wa Hoteli ya Bondeni iliyopo Magomeni, aliyemtaja kwa jina moja la Hashim, ambako rafiki zake walikuwa wamefikia, na kupewa taarifa kuwa rafiki zake hao walikuwa wameuawa, kwa madai kuwa ni majambazi.
“Nilipiga simu kwa watu mbalimbali ambao ni marafiki zangu kutoka Dar es Salaam, lakini wote walinithibitishia kuuawa kwa wafanyabiashara hao,” alidai Ngonyani.
Alisema kuwa baadaye alipigiwa simu na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Celina Kombani, ambaye pia ni Mbunge wa Ulanga Mashariki, na alimweleza waziri huyo kuwa waliouawa kwa madai kuwa ni majambazi ni wafanyabiashara, tena ni rafiki zake wa karibu, ambao anawafahamu fika.
Shahidi huyo aliendelea kueleza kuwa Waziri Kombani alimwambia kuwa wasihangaike kwenda Dar es Salaam, kwa kuwa miili ya marehemu hao ilikuwa inasafirishwa kuelekea Mahenge, Morogoro kwa ajili ya mazishi.
“Mbunge Celina ndiye aliyenisaidia kupata ukweli kwamba waliouawa walikuwa ni marafiki zangu kutokana na kuwa alikuwa mtu wetu wa karibu sana,” alidai Ngonyani.
Aliieleza mahakama kuwa hakushuhudia tukio la mauaji, lakini aliziona maiti za rafiki zake zikiwa na majeraha ya risasi sehemu za kichwani.
Shahidi mwingine, Bernadeta Ngonyani, ambaye ni mke wa shahidi wa kwanza, alidai mahakamani hapo kuwa, siku ya tukio, wafanyabiashara waliouawa walifika nyumbani kwake kwa ajili ya kumpatia fedha za matumizi, lakini mara baada ya kupatiwa fedha hizo alishangaa kuona wanakamatwa na polisi na kuwekwa chini ya ulinzi.
Bernadeta alishangaa kuona shemeji zake hao wakiwa wanafungwa pingu na kuanza kupekuliwa katika gari walilokwenda nalo nyumbani kwake.
Alidai kuwa Sabinus alikataa kupekuliwa na ndipo askari walipompiga kibao na kuchukua mkoba mkubwa uliokuwa katika gari lao, na kuurushia katika gari dogo la polisi, ambalo walikuja nalo eneo hilo.
“Nilishangaa sana, lakini mara baada ya kupekuliwa walichukua ule mkoba ambao nadhani ulikuwa na fedha zao na kuuhamishia katika gari la askari hao, ambao walikuwa wamekuja nalo, likiwa na askari polisi mwanamke mmoja,” alidai Bernadeta.
Alisema kuwa baada ya kupekuliwa, aliona Sabinus akitolewa bastola mfukoni pamoja na simu.
Alidai kuwa, pamoja na kunyang’anywa mkoba, shemeji zake hao, ambao kwa sasa ni marehemu, walinyang’anywa pia simu zao za mikononi kabla hawajachukuliwa na kuingizwa katika magari matatu ya polisi.
Alisema hakuweza kujua idadi ya askari wote waliokuwepo lakini katika moja ya magari, walikuwamo askari wa kiume wawili pamoja na askari mmoja wa kike.
Alisema kuwa baadaye, zilipopatikana taarifa kuwa vijana hao walikuwa wameuawa, alionywa na mumewe na kuamua kuondoka katika eneo hilo, yeye na mtoto wake, na kuelekea mkoani Ruvuma alikokaa kwa muda wa wiki mbili na kurudi tena Dar es Salaam.
Kabla ya kuanza kutolewa ushahidi, washitakiwa wote 13 walisomewa mashitaka yao na kutakiwa kujibu, ambapo wote walikana kuhusika na mauaji hayo.
Mshitakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Ahmed Makele, alipandishwa kizimbani mahakamani hapo akisaidiwa na wenzake, kutokana na kupatwa na maradhi ya kiharusi akiwa mahabusu juzi.
Wakisomewa mashitaka yao na wakili wa Serikali, Angaza Mwaipopo, alidai Januari 14, 2006, katika msitu wa Pande, Mbezi Louis, Dar es Salaam, washitakiwa kwa pamoja waliwaua watu wanne, huku wakidai kuwa ni majambazi.
Pamoja na Zombe na Makele, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mrakibu wa Polisi Christopher Bageni, F. 5912 Konstebo Noel Leornad, WP. 4593 Konstebo Jane Andrew, D. 6440, Koplo Nyangelera Moris na D.1406 Koplo Emmanuel Mabula.
Wengine ni E. 6712 Koplo Felic Sandsy Cedrick, D. 8289 Konstebo Michael Shonza, D. 2300 Koplo Abeneth Saro, D. 4656 D/Koplo Rajabu Bakari na D. 1367 D/Koplo Festus Gwabisabi. Washitakiwa hao wanatetewa na Wakili Majura Magafu.
Pamoja na wafanyabiashara hao watatu wa madini, mtu mwingine anayedaiwa kuuawa na askari hao ni Juma Ndugu, mkazi wa Sinza, Dar es Salaam, ambaye ni dereva wa teksi iliyokodiwa na wafanyabiashara hao.
Zombe na wenzake walifikishwa mahakamani hapo majira ya saa 2:30 wakiwa wamepakiwa katika mabasi mapya yanayotumika kuwasafirisha mahabusu, wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari magereza, ambao walivalia fulana za kuzuia risasi.
Watu wengi walifurika mahakamani kusikiliza kesi hiyo, ambayo itasikilizwa mfululizo kwa siku 15 katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

