Serikali yagoma kuilipa IPTL
April 18, 2008
SERIKALI imegoma kulipa gharama za kuzalisha umeme kwa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), baada ya kampuni hiyo kukataa kurekebisha viwango vya malipo vilivyopo katika mkataba.
Kutokana na hatua hiyo, mkataba tata kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na IPTL, huenda ukavunjwa au baadhi ya vipengele vinavyoumiza Taifa vikarekebishwa.
Dalili za kuvunjwa au kurekebishwa kwa mkataba huo zinatokana na ushindi wa Serikali dhidi ya IPTL, katika kesi iliyokuwa imefunguliwa na kituo hicho nchini Marekani, ikidai kulipwa dola milioni 27.2 za Marekani (karibu Sh bilioni 30).
Msingi wa kesi hiyo ni uamuzi huo wa Serikali kuitaka TANESCO kutolipa gharama zozote kwa IPTL, kuanzia Januari, mwaka huu.
Mbali na TANESCO, Serikali pia iliagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kutolipa fungu lolote la fedha kwa IPTL kama makubaliano ya mkataba yanavyoelekeza.Kutokana na uamuzi huo, IPTL ilikimbilia katika Mahakama jijini New York, Marekani, wakitaka Mahakama hiyo itoe uamuzi wa kuishinikiza Serikali ya Tanzania, hususan TANESCO kuilipa kiasi hicho cha fedha, ambazo ni malipo yasiyo na utata, yanayostahili kulipwa kwa kituo hicho kwa kuzingatia mkataba.
Katika madai yake, IPTL inaeleza kuwa Serikali ya Tanzania kama mdhamini mkuu wa TANESCO, imeshindwa kulipa kulingana na mkataba uliopo wa kuuziwa Megawati 100 za umeme, kwa shirika hilo pekee la umeme nchini. Madai ya jumla ya IPTL ni kwamba, Serikali inatakiwa kulipa dola milioni 45 pamoja na riba ya dola milioni 1.44 za Marekani, katika kipindi cha Novemba mwaka jana.
Hata hivyo, katika madai yake hayo, IPTL inasisitiza kulipwa deni inalolitambua kuwa “halina utata” linalofikia dola 26,016,487.15 za Marekani, pamoja na riba ya dola 1,53,395.52 kwa Novemba, mwaka jana. Kiasi hicho ndicho kinachofikia karibu Sh bilioni 30 za Tanzania.
IPTL imekiita kiasi hicho cha fedha kuwa ni malipo yasiyo na utata ambayo Serikali ni lazima iyakamilishe kulingana na mkataba. Hatua hiyo ya IPTL imetokana na mvutano uliopo, hasa baada ya Serikali kukataa kulipa dola milioni 45.
Kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa na Jaji Hellerstein wa New York. Akitoa uamuzi, Jaji huyo alisema kwa mujibu wa mkataba, IPTL inapaswa kuwasilisha kwanza malalamiko yake katika Baraza la Usuluhishi, kabla ya kuipeleka mahakamani kama ilivyofanya.
Alitoa miezi sita kwa Mwanasheria wa IPTL anayesimamia kesi hiyo, Robert Sentner, kuwasilisha taarifa yake kuhusu hatua anayopaswa kuchukua ya kufikisha suala hilo katika Baraza la Usuluhushi.
Hata hivyo, akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana kutoka New York, Mwanasheria anayeiwakilisha Serikali, Nimrod Mkono, ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Vijijini, alisema IPTL ilitaka kutumia njia ya mkato kujichotea mabilioni kutoka serikalini.
“Hoja yetu ya msingi katika hii kesi ni kwamba viwango vya malipo kwa IPTL ni vikubwa mno. Lakini pia hawa IPTL hawajawekeza inavyotakiwa, huduma si za kuridhisha,” alisema Mkono.
Alipoulizwa kuhusu hatima ya mkataba huo, Mkono alisema kwa hali ilivyo IPTL itahofu kwenda katika Baraza la Usuluhishi kwa kuwa inatambua kuwa udhaifu uko upande wake.Alisema badala yake, IPTL wanaweza kuzungumza na Serikali kuhusu kurekebisha viwango vya malipo (tariffs). Hivyo basi, kama mazungumzo hayo yatafanyika, ni dhahiri kuwa vipengele vya mkataba wa IPTL ambavyo vimekuwa vikiliumiza taifa vitarekebishwa
Na endapo, IPTL itapuuza kwenda katika Baraza la Usuluhishi kutokana na kuhofia udhaifu wake wa kutoa huduma na pia kugomea mazungumzo ya kurekebisha viwango vya malipo, Serikali itakuwa katika nafasi nzuri ya kuvunja mkataba huo, kama ilivyokuwa kwa Kampuni ya Huduma ya Maji Safi, Dar es Salaam (City Water).
Serikali kupitia TANESCO iliingia mkataba na IPTL, Juni 8, 1995. Mkataba huo ulianza kutekelezwa Mei 26, 1995. Kulingana na mkataba huo ambao umekuwa ukilalamikiwa kwa miaka mingi na wananchi, TANESCO imekuwa ikilipa takriban Sh bilioni 3 kila mwezi, na ingeendelea kutoa malipo hayo kwa kipindi cha miaka 20.
Imeandikwa na Gazeti la Mtanzania la leo

