Serikali iwe makini na utitiri wa makanisa

April 3, 2008

IBARA ya 19(1) ya Katiba ya nchi inasema kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake.

Ibara ya 19(2) inasema kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.

Kwa mujibu wa vifungu hivyo vya ibara hizo, tunaona taarifa zilizolisibu moja ya makanisa hivi karibuni kwamba watoto wachawi wawili, waliokuwa wanasafiri kwa ungo walivutwa na kudondoka katika eneo la ibada la kanisa hilo, ni za kusikitisha sana.

Kwanza, habari hizo zina lengo la kupambanisha imani ya kichawi na imani ya Mungu. Lakini zote ni imani, na tayari ibara 19(1) ya Katiba inampa kila mtu haki ya kuwa na imani anayoitaka.

Hao wanaoamini katika kusafiri kwa ungo nao wana imani inayolindwa na katiba sawa na wanaoamini imani ya Yesu.

Kwa hiyo tunashangaa ni kwanini watu waanze kuadhiriana kwa mambo yasiyo ya msingi, au labda ni ya kitapeli, ya kutafuta biashara ya waumini.

Lakini tujue kwamba, hili linatia dosari kwa wale wanaotangaza na kueneza dini, japo ibara 19(2) imewalinda na kuwahakikishia kwamba serikali haitaingilia shughuli za uendeshaji wa jumuiya za dini, watakapofanya mambo yanayoweza kuvunja amani ya jamii au hata kuhatarisha maisha ya waumini wao, dola haitakuwa na budi kuingilia kati.

Uhuru wa kuabudu hauwezi kutumika pale baadhi ya wachungaji watakapogeuza taasisi za dini kuwa vyombo vya ufisadi, ambapo matendo machafu yanayovunja maadili, biashara chafu zinazoenda kinyume cha sheria na utapeli wa kawaida unafanyika.

Tukumbuke mfano mmoja wa Uganda pale mchungaji mmoja aliyeitwa Kibwetere alipoangamiza wafuasi wake kwa kutumia wafuasi wa dini.

Jambo kama hilo hilo liliwahi kutokea Novemba 18 mwaka 1978 nchini Guyana, ambapo James Warren aliyejulikana kwa jina la Jim Jones alipounda kanisa lake kule Guyana katika visiwa vya Caribbean na kuua waumini wake 900 kwa sumu ya cyanide, wanaenda kumuona Yesu.

Basi, kwa kuwa dunia imejaa matapeli wa aina hii na dini sasa hivi zimekuwa biashara kubwa hapa nchini ambapo baadhi ya wajanja anakimbilia huko, ingefaa jamii itahadharishwe kuwa si kila anayehubiri dini ni kweli ni mtumishi wa Mungu.

Wapo manabii na watumishi wa Mungu feki wengi sana huko mitaani na yafaa wananchi wachukue tahadhari, kwani hawa wanasingizia kufanya miujiza lukuki na kutoa upako kwa jinsi ambavyo ni ya kushangaza.

Hivi sasa kuna kanisa limetangaza kutoa misukule. Yaani mtu aliyefariki miaka mitano au zaidi iliyopita, eti mchungaji anaweza kumrudisha? Hii inatisha!

Wanajua wananchi wengi wako katika hali ngumu ya maisha, wanakabiliwa na umaskini wa kupindukia, maradhi yasiyoponyeka kama ukimwi, kansa, na msambaratiko wa maisha ya ndoa, basi kwa kuhisi kuwa wana ufumbuzi wa haya yote, wanafanya ibada feki za kuwahadaa wananchi.

Kwa upande mwingine, tunaitahadharisha serikali kwamba utitiri wa taasisi za kidini ni ishara mbaya kwa utawala uliopo madarakani.

Ina maana kwamba hayo matatizo tuliyoyataja hayajapatiwa ufumbuzi na wananchi wamekata tamaa, hivyo ni rahisi kughiribiwa na wajanja wanaotumia dini kujinufaisha.

Tusije tukashangaa yale ya Jim Jones na Kibwetere yakitokea hapa Tanzania na hilo linaweza kuhatarisha amani ya nchi.

Tujiulize maswali, je, hawa watoto matapeli ambao Jeshi la Polisi Kinondoni lina rekodi zao, waliwezaje kumhadaa mchungaji mwenye aiba ya upako wa Roho Mtakatifu?

Tujiulize pia kazi iliyofanywa na taasisi za dini kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, na baada ya hapo, mbona viongozi wa dini na madhehebu ya Kikristo walishiriki kuwarubuni waumini wao kupigia kura mgombea waliyemtaka kwa madai kuwa mgombea huyo alikuwa amechaguliwa na Mungu wao?

Je, huo haukuwa utapeli wa wazi? Walikutana wapi na Mungu wao akawanong’oneza kwamba mwanasiasa huyo alikuwa chaguo lake?

Tangu lini mtu asiyemwamini Yesu kuwa ni mwana wa Mungu na Mungu kamili kwa sura ya binadamu na kwamba alikufa na kufufuka, akawa chaguo la Mungu wa Wakristo?

Mbona hata baadhi ya viongozi wa dini wametumia nafasi zao za dini kujitafutia vyeo kwenye vyama vya siasa?

Je, hizo sadaka na michango wanayopokea kutoka kwa mafisadi na hizo shughuli za uchangishaji wa fedha kwa ajili ya uendeshaji wa kidini unaofanywa na wanasiasa na baadhi ya mafisadi wanaojulikana, ndiyo njia muafaka ya kueneza shughuli za dini?

Sasa mwananchi wa Tanzania akimbilie wapi, akienda kwenye dini anakuta ufisadi, akienda kwenye jamii anakuta ufisadi, akienda kwenye siasa anakuta ufisadi, sasa kimbilio la Mtanzania litakuwa wapi?

Matukio ya kiimani yanayotokea katika baadhi ya makanisa siku hizi, yatufumbue macho na masikio ya kila mmoja wetu, kwani nyakati zimebadilika, viongozi wametugeuka na hakuna wa kumuamini.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0755 312859
katabazihappy@yahoo.com
www.katabazihappy.blogspot.com


Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post
 |  TrackBack URI for this post

Comments

One Response to “Serikali iwe makini na utitiri wa makanisa”

  1. Limbu kissellah on January 29th, 2010 12:14 pm

    Nashangaa na kusikitishwa na huduma zinazotolewa na shirika la umeme jijini Mwanza,wamekuwa wakikata umeme kadri wanavyojisikia bila hata kutoa taarifa kwa wateja wake hali ambayo inasababisha uharibifu wa vitu,tunaomba watoe maelezo ya kina ni kwa nini wanakata umeme hasa saa za usiku?

Got something to say?