Rwanda uso kwa uso na Sudan fainali Chalenji

December 21, 2007

TIMU ya soka ya Rwanda ‘Amavubi’ jana ilifanikiwa kutinga fainali za mashindano ya Chalenji baada ya kuifunga Uganda bao 1-0 katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam. Kwa ushindi huo, Rwanda itakutana na Sudan ambayo juzi ilitangulia fainali baada ya kuitoa Burundi kwa mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja huo huo.

Katika mchezo kati ya Rwanda na Uganda, timu zote zilitandaza soka safi na kushambuliana kwa zamu ambako hadi dakika 90 za kawaida, mwamuzi Victor Mwandike wa Tanzania akipuliza kipenga cha mwisho, timu hizo zilitoka zikiwa suluhu na hivyo kuongezwa dakika 30.

Katika dakika 30 za nyongeza, Rwanda ilifanikiwa kupata bao lake la pekee na la ushindi katika dakika ya 117 lililofungwa na Roger Tuyisenge, baada ya kupiga shuti lililowababatiza mabeki wa Uganda na kutinga wavuni.

Mchezo huo wa nusu fanali ya pili ulikuwa ni mgumu, ambapo baadhi ya mashabiki walidai kuwa ni mgumu kuliko hata fainali, ambayo itawakutanisha Amavubi na Sudan, mchezo utakaopigwa kesho katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mara baada ya mchezo huo, Kocha wa Rwanda, Kuze Josip, alisema mchezo ulikuwa mgumu, kwani Uganda ilistahili kushinda, ila walishindwa kutokana na mabeki wao kujichanganya.

Alitabiri kuwa atakuwa na kibarua kigumu pia katika mchezo wa fainali kama ilivyokuwa kwa Uganda, kwani Sudan ni timu nzuri.

KUTOKA: TANZANIA DAIMA

h.sep