Rita Mlaki: Nawajua makandarasi uchwara
May 27, 2008
MBUNGE wa Jimbo la Kawe, Rita Mlaki, amesema anawajua makandarasi uchwara wanaowaunganishia watu maji kinyemela. Amewataka kuacha tabia hiyo haraka kabla hawajashughulikiwa.
Mlaki alitoa onyo hilo jana wakati wa ziara ya Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam na Pwani (Dawasco) ya kumkabidhi mradi wa maji uliofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) katika jimbo hilo.
“Kuna makandarasi uchwara wanaowaunganishia wananchi maji…mimi nawajua na nawaonya waache mara moja kazi hiyo, wananchi pia msikubali kufanyiwa hayo na watu hao,” alisema mbunge huyo.
Akizungumzia kuhusu mradi huo, alisema amehangaika kwa muda mrefu kuwawezesha wananchi wa jimbo lake kupata maji na sasa ndoto hiyo imetimia. Aliahidi kuusimamia mradi huo vilivyo.
Awali, Meneja Uhusiano wa Dawasco, Badra Masoud, alisema katika mradi huo, ADB imetoa sh bilioni nane na kuwa ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kukamilika Aprili, mwakani. Mabomba yatatandazwa katika maeneo mbalimbali ili kuwawezesha wananchi kupata maji.
Alibainisha kuwa watekelezaji wa mradi huo utakaowanufaisha wananchi zaidi ya 10,000 wa jimbo hilo, ni Kampuni ya Engeneering Group Corpotarion, chini ya usimamizi wa kampuni ya ushauri wa kihandisi ya Porty ya Ujerumani kwa kushirikiana na kampuni za Inter Consult Ltd na FBNE Ltd za Tanzania.

