Richmond yamuibua Kiula
February 27, 2008
KASHFA ya Richmond iliyomlazimisha aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na mawaziri wengine wawili kujiuzulu na hatimaye Baraza la Mawaziri kuvunjwa takriban wiki mbili zilizopita, inazidi kuchukua sura mpya kila kukicha. Sakata hilo la Richmond jana lilimuibua kutoka mafichoni, waziri wa zamani wa Ujenzi na aliyepata kuwa mbunge wa Iramba, Nalaila Kiula, ambaye miaka 11 iliyopita Tume ya Rais ya Kuchunguza Mianya ya Rushwa iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ilimtuhumu kuhusika na rushwa, hatua iliyosababisha ashitakiwe na kutiwa mahabusu kwa siku tatu.
Akizungumza na wanahabari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dar es Salaam jana, Kiula alieleza kushangazwa na ukimya wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa ambaye vyombo kadhaa vya habari vimemhusisha na taarifa za kukiuka maadili ya uongozi wakati akiwa madarakani.
Aidha, mbali ya hilo, Kiula alieleza kushangazwa kwake na kauli aliyoitoa hivi karibuni Jaji Warioba ya kupinga sababu za kutomhoji Lowassa kulikofanywa na Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza utata katika mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura kati ya Richmond Development Company LLC na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe (CCM).
Akifafanua, Kiula aliwaambia waandishi wa habari kuwa anashangaa kuona mtu yuleyule (Warioba) aliyeandaa ripoti ndefu ya tume yake mwaka 1996, akimtuhumu kwa kufuja fedha za umma wakati akiwa waziri wa Ujenzi na kufikia hatua ya kutaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake bila ya kumpa fursa ya msingi ya kumsikiliza.
“Naamini tume ya Warioba ingeniita na kunihoji ile ripoti yao isingekuwa vile ilivyokuwa. Nimeshasamehe na Warioba atalipwa kwa mabaya aliyofanya juu yangu na mimi nitalipwa kwa mazuri yangu. Ni bahati kwamba nilishinda kesi Mahakama ya Kisutu na baadaye Mahakama Kuu nikashinda pia,” alisema Kiula.
Alisema hatua hiyo ya Tume ya Warioba ambayo aliilalamikia hata ndani ya Bunge na kufikia hatua ya kusema ana hakika Mungu ndiye atakayemlipia, ilisababisha akamatwe na akalazwa rumande siku tatu akiwa amevuliwa nguo zote na baadaye akafikishwa mahakamani.
“Warioba ameilaumu kamati ya (Dk. Harrison) Mwakyembe (aliyekuwa mwenyekiti), eti haijampa Lowassa nafasi ya kujitetea, je, yeye sasa alaumiwe na nani kwa haya anayoyafanya yasiyokuwa na msimamo, ninasema hivi kwa sababu hii ni nchi yangu.
“Niliposoma gazeti na kukuta Warioba aliyeninyima mimi fursa ya kusikilizwa akihoji sababu za Kamati Teule ya Bunge kutomhoji Lowassa, sikuamini, kwani mtu huyo ndiye yule yule ambaye mwaka 1996 aliandaa ripoti nzito dhidi yangu na akatoa mapendekezo ya mimi kuchukuliwa hatua za kisheria pasipo kunihoji. Hilo ndilo lililonileta leo hii hapa kuzungumza nanyi wana habari,” alisema Kiula.
Akifafanua huku akifunua kwa nyakati tofauti kurasa kadhaa za Ripoti ya Tume ya Warioba, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 1995, lundo la magazeti ambavyo vyote alikwenda navyo katika mkutano huo wa jana, Nalaila alimgeukia Mkapa aliyekuwa rais wakati huo na mtu aliyeunda tume hiyo na akamtuhumu kwa kukiuka maadili ya uongozi wakati akiwa madarakani.
Alisema ni jambo la ajabu kwamba, wakati akiwa madarakani, Mkapa, kiongozi ambaye wakati akikabidhiwa urais wa nchi aliahidi kuwa hatakuwa na simile na mla rushwa yeyote, yeye mwenyewe alipokuwa kiongozi alijikopesha shilingi milioni 500 benki pasipo kuwa na dhamana.
Kiula alikielezea kitendo hicho cha Mkapa kuwa ni cha ukiukwaji wa maadili ya uongozi, ambacho iwapo wanasheria watakitumia kinaweza kusababisha rais huyo mstaafu asitishiwe malipo ya marupurupu anayolipwa hivi sasa.
Alisema ni jambo la ajabu kwamba wakati Mkapa akikiuka maadili, yeye alifikishwa mahakamani akituhumiwa kujipatia sh milioni 12 tu isivyo halali, wakati ikijulikana bayana kwamba alikopa fedha hizo benki akiweka dhamana kitabu chake cha akiba ya benki kilichokuwa na sh milioni sita na kile cha marehemu mkewe kilichokuwa na sh milioni tano.
“Kama hiyo haitoshi, nilishitakiwa kwa kosa la kukopa sh milioni 12 benki ili ninunue daladala wakati ushahidi wa mkopo huo ninao na umekwenda kwa haki, lakini nilipelekwa sero wakati Mkapa aliyekuwa madarakani kwa wakati huo alikopa NBC dola 5,000,000 bila ya kuwa na dhamana yoyote. Mtu anayefanya hivi ndiye yule yule aliyesema hatakuwa na simile na wala rushwa,” alisema Kiula kwa mshangao.
Kiula alisema ni jambo baya kwa rais ambaye anapostaafu anapewa mamilioni ya fedha kuwa mdokozi, jambo alilosema anaamini iko siku tsunami itashuka na itamlazimisha Mkapa ambaye amegoma kujibu tuhuma hizi kuzijibu.
“Hivi ni kitu gani kinachokufanya wewe kama rais ambaye unapostaafu unatunzwa hadi ufe, uwe mdokozi, tena katika maeneo tofauti, EPA, Richmond, Buzwagi na IPTL? Lakini ipo siku tsunami itashuka atalazimika kujibu,” alihoji Kiula ambaye alikanusha kutumwa na mtu yeyote.
Kutokana na hilo, aliwataka wananchi kumpa Rais Jakaya Kikwete ‘gloves’ kama zile alizopewa wiki mbili zilizopita na Bunge kupitia Kamati ya Mwakyembe ili aweze kuchukua hatua za kukabiliana na watu waliokiuka maadili ya uongozi kama Mkapa.
Kiula aliyeonekana kuwa na dukuduku na Mkapa na Warioba, alisema anaamini kwamba yeye alipelekwa mahakamani na akadhalilishwa si na serikali bali watu wachache ndani ya serikali waliokuwa na malengo yao binafsi.
Alisema Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 iliitaja sekta ya ujenzi aliyoisimamia wakati akiwa waziri kuwa ni moja ya maeneo ya mfano, yaliyoonyesha mwelekeo wa mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 10 cha kati ya mwaka 1985 na 1995.
Mbali ya hilo, alisema anaamini kuwa Bunge likifikia maamuzi kama yale ya kuitaka serikali irudishe nyumba zote za wananchi walizouziwa baadhi ya watumishi wa umma, Rais Kikwete atatekeleza maamuzi hayo mara moja bila kujali iwapo yeye (rais) naye amenunua nyumba.
Akizungumzia Ripoti ya Kamati Teule ya Mwakyembe, Kiula alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edward Hosea na naibu wake kuachia madaraka yao kama ilivyopendekezwa na kamati hiyo ya Bunge.
Kiula alisema bado ana nguvu na moyo wa kurudi katika siasa na tayari mwaka 2006 alikutana na Rais Kikwete na katika maongezi yao walikubaliana amtumie katika kazi zake, lakini si kumuweka katika uwaziri au ubalozi.
Aliwataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Kikwete ili aendelee na kazi yake ya kusafisha wale wote wasiokuwa makini katika kazi.
Kwa upande mwingine, aliwaasa wabunge kuukataa muswada wa kuruhusu uraia wa nchi mbili utakapoletwa bungeni kujadiliwa, akisema iwapo utapitishwa kuwa sheria, wezi wanaoiba fedha kupitia mambo kama ya EPA au Richmond watapata fursa ya kuficha fedha nje ili kujijengea mazingira ya kwenda kuishi huko.
Alisema kuwa yeye anapinga sheria hiyo kwa sababu tayari baadhi ya watu wameshaanza kupeleka mabilioni ya pesa nje ya nchi ili waende kuishi huko pindi mambo yao yatakapowaharibikia hapa nchini.
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

