Richard usiishie kujuta,rekebisha mabaya (Mhariri)

November 18, 2007

MOJA ya mambo ambayo Richard Bezuidenhout amekuwa akisitikia sana tangu atangazwe mshindi wa shindano la Big Brother Africa II ni uhusiano wake na mshiriki kutoka Angola, Tatianna. Richard na Tatianna walikuwa na uhusiano mzito uliovuka mipaka ya urafiki wa kawiada na kuwa penzi zito ambalo lilimfanya mkewe Richard, Ricky kuamua kurejea kwao Canada, akieleza kuwa hakupendezwa na uhusiano huo.

Katika shindano hilo, washiriki 12 kutoka nchi mbalimbali za barani Afrika waliwekwa kwenye jumba la BBA II lililo jijini Johannesburg. Washiriki hao walivalishwa vinasa sauti maalum na kulikuwa na kamera 68 zilizokuwa zikichukua kila tukio ambalo kila mshiriki alikuwa akifanya bila ya kujijua ni wakati gani hasa anaangaliwa na kamera.

Baadaye, watazamaji wa televisheni ya M-net, iliyokuwa ikirusha moja kwa moja shindano hilo kwa siku zote 98, walitakiwa kuwapigia kura washiriki ambao hawakutaka waendelee kuwemo kwenye jumba hilo.

Inaonekana kuwa uhusiano wa Richard na Tatianna ulivutia wengi kiasi kwamba wawili hao wakafanikiwa kukaa kwenye jumba hilo kwa siku zote 98.

Lakini baada ya Richard kutangazwa mshindi na kujinyakulia kitita cha zaidi ya Sh125 milioni, doa limebakia kwa Richard, ambaye anaonekana kuwa msaliti wa ndoa yake na mtu asiyefaa kuigwa na hasa vijana, baada ya urafiki wake na Tatianna kuvuka mpaka.

Richard amekuwa akijitetea kuwa alilazimika kufanya yale aliyoyafanya kwa sababu mazingira yalikuwa magumu sana kiasi cha kushindwa kuvumilia. Anaeleza kuwa mazingira ambayo waliwekwa yalikuwa magumu kwa mtu yeyote kuweza kukabiliana nayo.

Richard pia ameeleza kujutia kile alichozidisha katika uhusiano wake na Tatianna na zaidi ya yote ameahidi kuwa atafanya kila jitihada kuhakikisha anaokoa ndoa yake na kuendelea na maisha na mkewe.

Kwa kutambua hilo, Richard sasa hana budi kuanza kuijenga taswira hiyo mpya kwa jamii kuonyesha kuwa vitendo vya kutoka nje ya ndoa si vizuri, hata kama wanandoa wako mbali kimwili kwa muda.

Kwa kuwa jamii, hasa ya rika lake, imeshamkubali au inamuhusudu, Richard hana budi kutumia fursa hiyo kufuta madoa yote yaliyojionyesha kutokana na maisha yake kwenye jumba hilo na kujenga picha mpya ya mwanamume muadilifu kwenye ndoa anayeweza kujutia makosa yake.

Richard hana budi kusimama mstari wa mbele kupinga vitendo viovu kwenye maisha ya ndoa na kutumia umaarufu alionao sasa kuwaelimisha vijana na jamii kwa ujumla kuwa mahusiano nje ya ndoa na kabla ya ndoa hayana budi kuwa na mipaka yake na kujifunza kuheshimu ndoa.

Hilo litasaidia kufuta fikra zinazoonekana kuingia akilini mwa wengi ambao walivutiwa na uhusiano wa Richard na Tatianna kwamba ulikuwa usaliti ambao haufai kushabikiwa.

Na pia litasaidia kuyakuza yale mazuri ambayo Richard aliyaonyesha wakati akiwa kwenye jumba hilo kama upole, kuwa muwazi, kutopenda vikundi vya majungu na kuishi maisha ya kuigiza.

Hii ni nafasi yako Richard kufuta madoa ili kuelimisha vijana na jamii kwa ujumla. Kujuta kwako kusiishie mdomoni, bali kuambatane na matendo.


Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post
 |  TrackBack URI for this post

Comments

Got something to say?