Redet yamuonyesha Kikwete pa kunyoa
December 21, 2007
* Asema ni kioo kwa utendaji wa serikali yake
* Kukiwa na haja atavunja Baraza la Mawaziri
* Asema ahadi zake zitatimia ifikapo 2010
* Akanusha Gavana BoT kutorokea Marekani
Na Dennis Msacky
RAIS Jakaya Kikwete amesema ripoti ya hivi karibuni iliyofanywa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (Redet) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni nzuri na kwamba imemsaidia kujua mahali pa kunyoa.
Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Ikulu, jijini Dar es Salaam katika kuadhimisha miaka miwili tangu aingie madarakani, Rais Kikwete alisema ameisoma kwa makini ripoti yote ya Redet na kusema kwamba imemsaidia kujua mahali pa kunyoa.
Kikwete aliisifia ripoti hiyo akisema kuwa serikali yake inaichukulia kama kioo cha kuangalia ili kujua ni wapi pamevimba na kufanya marekebisho ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Rais Kikwete alisema kwamba tafiti za aina ya Redet zinafanyika duniani kote kwa ajili ya kujua maoni ya wananchi juu ya utendaji wa serikali.
“Tafiti za aina hii zinatumika sana duniani. Kitu muhimu katika ripoti ni nini maoni ya watu juu ya utendaji wa serikali kuhusu mambo mbali mbali. Ripoti ambayo serikali inaiona kama kioo cha kujitazamia ili kujua eneo lililovimba ni lipi na kama nywele zimezidi kumtafuta kinyozi …,” alisema.
Alisema kwamba ameisoma ripoti hiyo na kujionea jinsi ambavyo wananchi wanavyouona utendaji wa serikali yake na kwamba ni changamoto kwa serikali kujichunguza na kufanya mabadiliko.
Utafiti huo wa Redet, ulionyesha kwamba utendaji wa serikali ulikuwa umeshuka, huku ule wa rais ukiwa umeshuka, lakini si kwa kasi kama ile ya mawaziri, taasisi za serikali, Bunge na Mahakama.
Katika utafiti huo, pia wananchi walipata fursa ya kupendekeza ni mawaziri gani ambao wangependa waondolewe katika Baraza la Mawaziri.
Hatua ya kuikubali ripoti ya Redet na kuahidi kuifanyia kazi inamaanisha kuwa huenda Kikwete atafanya mabadiliko kwa wale mawaziri ambao jamii imeonyesha kutoridhika na utendaji wao, ingawa katika mkutano wake na vyombo vya habari hakuzungumzia hilo.
Rais Kikwete pia alisema anaweza kulivunja Baraza la Mawaziri wakati wowote kama kutakuwa na haja, lakini kwa sasa bado hajaamua kufanya hivyo na kwamba uvumi ulioenea mitaani anauchukulia kama hisia za wananchi.
Sambamba na hilo, Rais Kikwete pia amesema kwamba ushauri wa kupunguza ukubwa wa baraza hilo utafanyika pale ambapo mahitaji ya uundwaji wake yatakuwa yamekamilika.
Rais Kikwete alisema hayo kufuatia swali aliloulizwa na mwandishi wa habari mmoja kuwa uvumi umeenea mitaani kwamba kufuatia ripoti hiyo ya Redet anataka kulivunja Barala la Mawaziri.
“Baraza la Mawaziri tunaweza kulibadili wakati wowote, lakini kwa sasa bado iendelee kubakia kuwa ni uvumi tu au tusema kwamba ni matakwa ya watu. Kukiwa na haja tutalibadilisha wakati wowote, kukiwa hakuna haja tutaendelea mbele na safari,” alisema.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na uvumi kwamba Rais Kikwete anatarajia kuvunja Barala la Mawaziri wakati wowote, ikiwa ni pamoja na kupunguza ukubwa wake.
Hata hivyo, vyanzo mbalimbali kutoka ndani na nje ya serikali vinasema kwamba Rais Kikwete atafanya mabadiliko ya baraza hilo, lakini kwa sasa ataanzia kwa watendaji wa chini yaani, wakurugenzi, wakuu wa wilaya na mikoa.
Pia Rais Kikwete alisema wakati anaunda Baraza la Mawaziri alizingatia mahitaji na kama ataona halijafanya kazi aliyotaka hatasita kulifanyia mabadiliko. “Tuliunda serikali kwa mahitaji, sasa tuone kama linahitaji marekebisho,” alisema Rais Kikwete.
Wakati huoho Rais Kikwete alisema Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Balal sasa yupo Marekani kwa matibabu na kwamba hajatoroka kama inavyodaiwa na baadhi ya watu na wanasiasa.
“Gavana wa BoT anaumwa, yuko Marekani ambako anatibiwa, anaumwa, hajatoroka nchini,” alisema Kikwete.
Kwa zaidi ya miezi mitatu, bosi huyo wa BoT amekuwa nje ya nchi kwa maelezo kwamba anapata matibabu, lakini taarifa rasmi ilikuwa haijatoka.
Kuhusiana na ahadi ambazo alitoa wakati akigombea nafasi ya urais, Kikwete alisema ana uhakika kwamba ifikapo mwaka 2010, atakuwa ametimiza ahadi zote ambazo aliahidi.
” Katika miaka miwili tumefanikiwa kuweka misingi, sasa kilichobakia ni kuweka matofali, mimi mwenyewe sina wasiwasi, mwaka 2010, wakifanya tathimini tutakuwa tumeshinda kwani misingi tumeweka. Tutatimiza ahadi ambazo tulitoa. Katika kipindi hicho, Watanzania watapata huduma bora na maisha bora kwa Mtanzania yatabadilika,” alisema.
Kuhusu mazungumzo ya muafaka kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), Rais Kikwete alisema yanaendelea vizuri na hakuna mtafaruku wowote.
“Mazungumzo yanaendelea vema, hakuna matatizo kwa kuwa yangekuwako ningeambiwa,” alisema Rais Kikwete.
KUTOKA: MWANANCHI
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

