Rais Kikwete aagiza kuwajibishwa kwa watumishi wabovu
January 29, 2008
RAIS Jakaya Kikwete ametaka Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuhakikisha inawashughulikia wafanyakazi wasio waadilifu, ikiwa ni hatua ya kuwezesha mpango wa awamu ya pili ya programu ya kuboresha utumushi wa umma.
Akizindua programu hiyo jijini jana, Kikwete alisema licha ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mpango huo, kuna malalamiko mengi ya wananchi kuhusu huduma zisizoridhisha kwa baadhi ya idara za serikali.
Miongoni mwa malalamiko hayo yanahusu ubabaishaji na vitendo vya rushwa, suala lisilotakiwa kuendelea kuwepo kwa wakati huu.
Alisema malalamiko mengi ya wananchi yamekuwa yakielekezwa kwenye sekta za elimu, afya, usalama wa raia, utoaji haki, mambo ya ndani na ardhi, hali inayodhihirisha kutokuwepo kwa uwajibikaji wa kutosha kwa baadhi ya watumishi wa umma.
“Nimefurahi kusikia kwamba tatizo la kutowajibika litashughulikiwa awamu hii ya maboresho. Hii ni kuandaa utaratibu wa uwajibikaji wa taasisi zote za umma ngazi zote, ni vyema tuharakishe uandaaji wa utaratibu huo ili ukamilike mapema. Tusichukue muda mrefu sana kwa kazi ya uandaaji, naamini tukiutekeleza vizuri utaratibu huu utasaidia kuimarisha utendaji wa serikali na utoaji huduma kwa wananchi,” alisema.
Aliongeza kuwa, ni vizuri watumishi wa umma kuendelea kutambua kuwa ni haki ya wananchi kudai na kupata huduma nzuri kutoka kwao, kwa sababu utumishi wa umma upo kwa ajili ya kuhudumia wananchi.
“Pia, nafurahi kusikia awamu hii ya pili ni kuboresha maslahi ya watumishi wa umma na kujenga utumishi wa umma wenye nidhamu na unaozingatia maadili. Hili nalo ni jambo muhimu sana. Hakuna mafanikio bila nidhamu kazini” alisisitiza.
Aliwataka kuangalia uwezekano wa kuanzisha Chuo cha Taifa cha Uongozi, kitakachotoa mafunzo kwa viongozi na watendaji kwa sababu nchi inahitaji viongozi makini, wabunifu, wanaoona mbali na wachapa kazi hodari.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), Hawa Ghasia, alisema kupitia programu hiyo itakayogharimu dola za Marekani 103.8 milioni kwa miaka mitano, ofisi yake itaweza kushughulikia kwa kina uboreshaji mifumo ya utoaji huduma, kuongeza uwajibikaji na usikivu wa serikali, kuboresha maslahi ya wtumishi, kuboresha mifumo ya usimamizi wa watumishi, utungaji wa sera na kuimarisha uongozi wa utumishi wa umma.
Aliongeza kuwa awamu hiyo yab pili itaendeshwa kwa michango iliyozishirikisha Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), serikali za Uingereza, Canada, Denmark, Japan na Ireland.
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

