Mwenge wa Olimpiki kuja na neema Tanzania

October 29, 2007

MWENGE wa Olimpiki, ambao unatarajiwa kuwasili Tanzania, Aprili mwakani, ikiwa ni katika kuelekea michezo hiyo nchini China, utaleta neema katika mchezo wa riadha ambako kwa mara ya kwanza kutarindima mbio za Nusu Marathoni jijini Dar es Salaam, imefahamika. Habari za uhakika zilizopatikana kutoka vyanzo mbalimbali jijini Dar es Salaam, zinasema kuwa mbio hizo za kilomita 21 zitafanyika kabla ya kuanza kukimbizwa kwa mwenge huo ambao umepangwa kuanzia maeneo ya Tazara jijini Dar es Salaam.

Mwenge huo utaanza kukimbizwa majira ya saa 8:00 mchana ambako mbio hizo zitaanza asubuhi.

Mbio hizo zimepangwa kufanyika kuanzia viwanja vya Biafra, Kinondoni na kupita wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam.

Mbio hizo zinatarajiwa kuwa na zawadi mbalimbali nono, ambako mshindi wa kwanza ataondoka na kitita kisichopungua sh milioni tatu kutoka kwa moja kati ya wadhamini wa mbio hizo za mwenge wa Olimpiki, Kampuni ya vinywaji ya Coca Cola.

Kufanyika kwa mbio hizo itakuwa ni neema kwa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani, kwani ni miaka mingi hakuna mashindano makubwa ya mbio ndefu za barabarani, yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

Pia habari za kufanyika kwa mbio hizo ni neema kwa Chama cha Riadha Tanzania (RT), ambacho nacho hakina mbio ndefu za marathoni au nusu marathoni za kitaifa.

Jiji la Dar es Salaam ni pekee katika Bara la Afrika ambako mwenge huo wa Olimpiki utakimbizwa kati ya miji 49 duniani, nje ya wenyeji China.

Mwenge huo ambao unabeba ujumbe wa kuhimiza amani, utakimbizwa kuanzia maeneo ya Tazara na kupitia barabara mbalimbali ikiwamo, Mandela, Taifa, Samora, Sokoine, Ali Hassan Mwinyi, Bibi Titi, Morogoro, Lumumba na kuishia viwanja vya Mnazi Mmoja.