Mwekezaji Reli ya Kati matatani
February 27, 2008
WAFANYAKAZI wa Shirika la Reli nchini (TRL) wametangaza mgogoro na mwajiri wao, na sasa wanapanga kufanya maandamano ya nchi nzima kushinikiza nyongeza ya mishahara yao. Wafanyakazi wa TRL wa Dar es Salaam, jana walikutana na kukubaliana kimsingi kuwa wawasiliane na wenzao nchini kote, kupitisha azimio la kumpa saa 48 mwajiri wao kufikiri kuwaongezea mishahara, na iwapo atashindwa kufanya hivyo katika muda huo, basi wagome.
Wakizungumza kwa uchungu na jazba katika mkutano huo, walisema wanasikitishwa na manyanyaso wanayofanyiwa na mwajiri wao mpya kwa sababu wakati amekataa kuwalipa wao mishahara mipya, watumishi wengine walioajiriwa kutoka nje ya nchi wanalipwa mishahara mikubwa.
Wakizungumza katika mkutano ulioitishwa na Chama cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU) na kufanyika katika karakana ya TRL, wafanyakazi hao walisema kuwa, wamejaribu kufanya kila jitihada za kukaa na uongozi wa shirika hilo, ili watekelezewe madai yao, lakini imeshindikana.
Katika mkutano huo waliwagawia waandishi wa habari karatasi zinazoonyesha kuwa wafanyakazi 18 wa shirika hilo wenye asili ya Kiasia wanalipwa mishahara yao kwa dola za Marekani kati ya 1,500 na 2,880 pamoja na marupurupu yanayoanzia dola 2,233 na 4,740 sawa na wastani wa sh 2,888,000 hadi 5,894,000 huku Watanzania wakilipwa sh 86,000.
Katibu wa TRAWU, Sylvester Rwegasira alisema kuwa, baada ya kuketi na uongozi wa TRL na kujaribu kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo, uongozi uliwakatalia kwa madai kuwa, kampuni ya Rites, ambayo imelikodi shirika hilo, haijaanza kupata faida.
Kilio cha wafanyakazi hao ni kutaka kuongezwa mishahara kutoka kiwango cha sasa cha sh 86,000 kwa kima cha chini hadi kufikia sh 400,000.
Hata hivyo, menejimenti hiyo ilisema kuwa ipo tayari kuongeza mishahara kwa asilimia 15 ya ile wanayolipwa sasa, kiasi ambacho kilipingwa na TRAWU na kuamua kulipeleka suala hilo katika Baraza la Usuluhishi kama sheria zinavyosema.
Mkutano wa usuluhishi ulifanyika Februari 22, mwaka huu, lakini jibu halikuweza kupatikana na msuluhishi akaomba muda zaidi. Wafanyakazi hao walipokwenda Feburuari 25 walipewa cheti kinachoonyesha kuwa, msuluhishi ameshindwa kuutatua mgogoro huo, hivyo kutakiwa kwenda mahakamani iwapo bado walikuwa na malalamiko.
Wafanyakazi hao wamesema hawakubaliani na majibu hayo na kwamba si kazi ya msuluhishi kuwataka waende mahakamani, hivyo wakaamua kurejesha ajenda hiyo kwa wafanyakazi wote ambao walikaa na kupiga kura ya siri iliyopendekeza mwajiri apewe notisi ya saa 48 na iwapo atashindwa kuwapandishia mishahara, watagoma nchi nzima.
Kati ya wafanyakazi 483 waliohudhuria mkutano huo, 481 walipiga kura za kuunga mkono azimio hilo, huku mfanyakazi mmoja akipinga.
Mwenyekiti wa TRAWU, Bakari Kiswala, alisema kuwa, notisi hiyo itatolewa baada ya kupata matokeo ya maamuzi yatakayofikiwa na wafanyazi wengine kutoka Kigoma, Mwanza, Dodoma na Morogoro watakaoanza kupiga kura leo.
Alisema wafanyakazi hao wana uhuru wa kulikubali pendekezo hilo au kupendekeza kufuata njia ya mahakama ili kudai haki zao.
Mwenyekiti huyo alisema pia kuwa, katika mgomo huo hawatafanya vurugu, bali watabaki kwenye vituo vyao vya kazi bila kufanya kazi, hadi pale madai yao yatakapotekelezwa.
Alisema kuwa wanaamini uamuzi huo utaigusa serikali ambayo bado ina asilimia 49 ya hisa katika shirika hilo na hivyo kuwasimamia wao kupata haki zao.
Alipotafutwa kwa njia ya simu ili aelezee suala hilo, Waziri wa Miundombinu, Andrew Change, alimtaka mwandishi awasiliane na msaidizi wake, ili aweke miadi ya kukutana naye kwani hayuko tayari kuzungumza kwenye simu.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa upande wa wafanyakazi, TRL nayo imezidi kujiimarisha katika shughuli zake baada ya jana kupokea vifaa kadhaa, vinavyotarajiwa kuimarisha hali ya usafiri katika reli inayohudumiwa na shirika hilo.
Ratifa Baranyikwa anaripoti kuwa, TRL imepokea vichwa tisa vya treni ambavyo imevikodi toka Kampuni ya RITES yenye makao yake makuu nchini India, ambayo pia ndiyo iliyokodishwa kuendesha TRL.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kwenda bandarini kushuhudia vichwa hivyo vikishushwa, Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Narasimhaswaml Jayaram, alisema vingine vitano vinatarajiwa kuingia nchini wakati wowote, lakini kwa sasa vimekwama kwenye bandari ya Sharjah.
Jayaram alisema kuwa, vichwa hivyo ambavyo vina ukubwa wa kati wa 73 class, gharama yake ya kuvikodi ni dola za Marekani milioni sita kwa mwaka.
Aidha ukodishwaji wa vichwa vyenye ukubwa huo umekuja, baada ya India kutokuwa na vichwa vya treni vyenye ukubwa na uwezo zaidi kama ule wa 89 class, 88 class, 74 class, hata hivyo mjumbe wa bodi wa TRL, Siraju Kaboyonga alisema shirika lina vichwa vya treni vya aina hiyo ambavyo kwa sasa linavifanyia ukarabati kutokana na kuwa vibovu.
Akizungumzia kuhusu ubora wa vichwa hivyo, mkurugenzi huyo alisema kuwa vimetengenezwa miaka kumi iliyopita, hata hivyo baadhi ya wataalamu waliozungumza na mwandishi wa habari hizi bandarini wakati vikishushwa, walisema kuwa vina umri wa zaidi ya miaka ishirini tangu kutengenezwa isipokuwa vimepakwa rangi ili vionekane vipya.
Wakati huo huo, Jayaram alisema kuwa, TRL pia imekodi mabehewa mengine 23 kutoka India ambayo yanatarajiwa kuingia nchini mwezi ujao. Alisema kuwa gharama ya kukodi mabehewa hayo kwa mwaka ni dola za Marekani 0.6 milioni.
Aidha, alisema kuwa wamelazimika kukodi mabehewa na vichwa vilivyotumika kwa sababu gharama zake ni rahisi ukilinganisha na kununua vipya.
Akizungumza na mwandishi wa Tanzania Daima aliyehoji kama ubora wa vifaa hivyo na matumizi yake yamethibitishwa na Mamlaka ya usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Jayaram alisema kuwa, SUMATRA ilishatoa baraka zake miezi mitatu iliyopita na walikubali viingizwe nchini.
Akizungumzia kuhusu reli ya Tanga ambayo kwa sasa shughuli zake zimesimama, Kaboyonga alisema kuwa tatizo lililopo kwenye njia hiyo hadi kufikia hatua ya kusimamisha ni ukosefu wa vitendea kazi ikiwemo mabehewa na injini ambazo nyingi zilizorithiwa si nzima.
Hata hivyo, alisema kuwa TRL ina mpango wa kurejesha tena huduma katika njia ya Tanga mara baada ya kupatikana kwa miundombinu iliyotengemaa na kurudisha biashara ya TRL ambayo inategemea zaidi kwenye ubebaji mizigo.
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

