Mwakyusa kutangaza ripoti ya MOI leo
December 21, 2007
RIPOTI ya tukio la upasuaji tata dhidi ya wagonjwa wawili waliofanyiwa upasuaji kinyume na magonjwa yao katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) inatarajiwa kutangazwa leo. Ripoti hiyoTume iliyoundwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa itatangazwa na waziri huyo leo zikiwa ni siku 32 tangu wagonjwa hao wafanyiwe upasuaji huo tata.
Wagonjwa hao ni Emmanuel Didas (20), aliyefanyiwa upasuaji wa kichwa badala ya mguu, ambaye na kwa sasa yuko nchini India kwa matibabu zaidi na Emmanuel Mgaya (19), ambaye ni marehemu alipasuliwa mguu badala ya kichwa. Afisa Mawasiliano Msaidizi wa wizara hiyo, Victor Nyalali alisema Profesa Mwakyusa, atatangaza ripoti hiyo leo asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa wizara hiyo.
Ripoti hiyo ilikuwa itangazwe Desemba 19, mwaka lakini iliahirishwa kufuatia msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Kiteto (CCM), Benedict Losurutia, aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo Proesa Mwakyusa alikuwa mmoja wa viongozi wa serikali waliokwenda kwenye mazishi hayo.
Tume hiyo iliundwa na Waziri Mwakyusa, baada ya tume ya awali, iliyoundwa na Bodi ya Wakurugenzi wa MOI chini ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Profesa Laurent Museru kuwa na mapungufu.
Tume hiyo iliundwa na Mwakyusa Novemba 22 na ilianza kazi yake Novemba 26 na kukamilisha kazi Desemba 2 na kumkabidhi waziri ripoti Desemba 11. Tume ya Profesa Museru yenye wajumbe sita ilikuwa chini ya Profesa Victor Mwafongo kutoka Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu na ya Waziri Mwakyusa yenye wajumbe watano ilikuwa chini ya Profesa William Mahalu wa Hospitali ya Bugando. Mwisho.
KUTOKA: MWANANCHI

