Mwakyembe azua jambo Mbeya
February 28, 2008
MAPOKEZI makubwa yaliyoandaliwa kwa ajili ya kumpokea Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, inadaiwa kuwa yameanza kuhujumiwa kutokana na chuki za kisiasa. Hujuma hizo zinatoka kwa baadhi ya watendaji wa serikali na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao hawakuwa kwenye kambi ya mbunge huyo katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu mwaka 2005.
Wakati hali hiyo ikiwa imejidhihirisha hivyo, viongozi wa serikali na CCM wilayani humo wamekana kujihusisha na njama za kuzuia mapokezi hayo licha ya kutokuwa tayari kuelezea kama wameyaunga mkono au kutoa baraka za kuruhusu kufanyika kama wananchi walivyokusudia.
Habari kutoka kwa baadhi ya wananchi na wajumbe wa kamati ndogo ya mapokezi ya mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge ya kuchunguza mkataba wa Kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond, zimeeleza kuwa tangu kuanza kwa maandalizi hayo, wahusika wamekuwa wakikumbana na vikwazo na vitisho katika ushiriki wao.
Wananchi hao waliozungumza na Tanzania Daima jana, walisema walikuwa wakiitwa mmoja mmoja na baadhi ya vigogo wa serikali na chama na kuwatolea vitisho huku wakionywa kuacha mara moja kuendesha mikakati ya mapokezi ya mbunge huyo bila kutolewa sababu za msingi.
Wakizungumza kwa sharti la majina yao kutowekwa wazi, walisema maandalizi yaliyopangwa kufanyika Machi 2, mwaka huu yana lengo la kumpongeza kwa niaba ya wajumbe wote wa kamati hiyo teule ya Bunge kwa kazi nzuri na ujasiri waliouonyesha katika kuchunguza suala hilo.
Walidai uamuzi wa kuandaa maandamano hayo umeibua upya uhasama na chuki za awali za kisiasa zilizokuwa zimeliandama jimbo hilo mwaka 2005 na kuligawa makundi mawili - lile lililokuwa likimuunga mkono Dk. Mwakyembe aliyeibuka mshindi na la John Mwakipesile, ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Aidha, imebainika kuwa wakati wananchi wakiendelea na mikakati ya kumpokea mbunge huyo, kundi la pili limedaiwa kuwatumia viongozi waandamizi wa chama na serikali kuhakikisha wanazuia kufanyika kwa mapokezi hayo.
Mwenyekiti wa kamati ya mapokezi hayo, Christopher Mullemwa, alikiri kuwepo kwa vitisho vinavyodaiwa kufanywa kwa baadhi ya wananchi wanaojitolea kuandaa mapokezi ya Dk. Mwakyembe, na kusema hali hiyo imesababisha baadhi ya wananchi kuacha kuhudhuria vikao vya maandalizi.
Alisema pamoja na jitihada za kutaka kukwamishwa kwa maandalizi hayo, kwa upande wao wamekamilisha maandalizi yote ya awali, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha taarifa za kimaandishi serikalini za kuomba kibali kwa Jeshi la Polisi, ambalo alidai limekubali.
Alieleza kushangazwa na baadhi ya wananchi wanaoogopa kushiriki katika maandalizi hayo, na kusema mapokezi hayo yamefanywa bila kujali itikadi za vyama.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kyela, Japhet Mwakasumi, alikana chama hicho kujihusisha na mapokezi hayo.

