Muziki sawa, lakini filamu zetu…
October 31, 2007
HAKUNA ubishi kwamba kwa sasa Tanzania iko juu katika shughuli mbalimbali za sanaa.
Hivi sasa tuna watunzi wa muziki wanaotunga nyimbo zilizokwenda shule kama dada yangu Irene Sanga aliyetunga wimbo wa ‘Salaam kwa Mjomba’ uliompandisha chati Mrisho Mpoto aliyeimba shairi lake kwa umahiri mkubwa.
Niweke wazi tu kwamba kwa kweli na kutoka ndani kabisa ya nafsi yangu, nampenda sana dada Irene Sanga kiasi cha kuombea itokee awe rafiki yangu.
Nampenda mno dada huyu kwa kazi zake za muziki zilizokaa kisomi kisomi namna hii kama huo wa ‘Salaam kwa Mjomba’, ‘Utandawazi’ na ‘Pangisheni.’
Mbali ya wataalam kama dada Sanga, tuna vijana wanaojitahidi mno katika muziki wa kizazi kipya na muziki wa dansi.
Kwenye muziki wa kizazi kipya, kila kijana yuko safi kwa eneo tofauti. Kwa mfano MwanaFA ni mzuri sana katika fasihi, Wagosi wa Kaya ni wakali katika Uwazi na Ukweli wakati Professor Jay ni mzima sana katika tungo za hadithi (visa). Pia yumo Mr Ebbo asiyeshikika kwa “rap katuni” wakati Kylnn ni mkali kwa hisia kali za mahusiano ya kimapenzi.
|
Juma Nature |
Wanaume wote-Halisi na Family- ni nambari wani katika uchangamfu majukwaani. Hizo ni ‘kategori’ chache tu katika vipaji vilivyojaa ndani ya Muziki wa kizazi kipya.
Kwenye muziki wa dansi wa vijana nako kumetulia sana kukiongozwa naAlly Choki anayetunga tungo za kiutu uzima na zenye mantiki.
Wapo kina Rogart Hegga ‘Katapila’ ambaye utunzi wake wa wimbo ‘Katapila’ akiwa na Mchinga Generation unasimama eneo moja na utunzi wa Akudo Impact wa ‘Ukisikia Nimekufa Usiweke Msiba’ kwa mapigo matamu mno ya taratibu na ujumbe mzito ndani yake.
Dansi ya wazee akina Msondo na Sikinde, haihitaji maelezo marefu juu ya ubora wake.
Kwa upande wa filamu, nako tuko juu mno. Hivi sasa watu wanajitahidi sana kuwafukuza Wanigeria katika kutengeneza filamu bora.
Lakini kwangu binafsi nawafurahia sana wanaoigiza tamthilia ya Jumba la Dhahabu inayoonyeshwa na Televisheni ya Taifa kwani kila mmoja ameuvaa uhalisia kwa nafasi aliyopangiwa.
Aidha, namsifu sana mtunzi wa tamthilia hiyo, Tuesday Kihangala, kwa jinsi alivyoupangilia mfuatano wa matukio.
Kama ilivyo kwa dada Sanga, wasanii wa kundi hilo hawahangaiki kulazimisha kukwezwa bali wanakwezwa na kazi yao nzuri tofauti na baadhi ya wasanii ambao tumefikia mahali pa kuwachoka magazetini na kwenye televisheni wakilazimisha kukwezwa!
Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na wasanii wetu, bado tunahitajika umakini mkubwa katika kuweka sawa mambo madogo madogo yatakayosababisha kushusha hadhi ya kazi zao nzuri.
Tatizo la kwanza ni matumizi ya lugha isiyo sahihi. Kuna filamu inaitwa DILEMA.
Kutokana na maelezo ya waliohusika kutengeneza filamu hiyo, jina lililokusudiwa lilikuwa DILEMMA, neno la kiingereza lenye maana ya mtu kuwa katika hali tata ya kuamua afanye lipi kati ya mambo mawili au zaidi wakati yote ni muhimu kwake lakini hali inamlazimisha afanye moja tu.
Hali hizo zimejitokeza sana kwenye filamu hiyo,mojawapo ni ile ya kijana aliyetakiwa kwenda kufunga ndoa lakini anakutana na mpenzi wake aliyezaa naye na waliyepoteana.
Kijana huo alikuwa kwenye ‘dilemma’ aendelee na taratibu za kufunga ndoa au aachane nazo akaishi na mzazi mwenzake?
Kwa waandaaji kukosa umakini, jina la filamu hiyo limekuwa neno lisilo la kiingereza bali labda la lugha kadhaa za kibantu ambapo ‘lema’ maana yake ni kataa ambapo ‘kalema’, kakataa na ‘dilema’ inamaanisha limekataa!
Hayo hayakuwa makusudio ya waandaaji wa filamu hiyo wanayotaka itambe hadi nje ya mipaka yetu.
Hivi huyu Mcheza filamu maarufu,Ramsey Noah wa Nigeria aliyehudhuria uzinduzi wa filamu hiyo aliiweka filamu hiyo kwenye kiwango kipi cha hadhi baada tu ya kuelewa kuwa tumekosea neno rahisi la Kiingereza, ‘Dilemma’, kama jina la filamu hiyo?
Hivi sasa tena tuna filamu inayoitwa ‘Darkness Night’ inayotafsiriwa kuwa Usiku wa Giza. Hapana, Darkness Night haina maana yoyote kwenye lugha ya kiingereza! Kwa kushindwa kuiita ‘The Dark Night’ au ‘Night in Darkness’ ambayo ni sahihi, ingetosha filamu hiyo kuitwa ‘Usiku wa Giza’ kwani ni ya Kiswahili kwa ajili ya Waswahili.
Hiyo Darkness Night inafanya wanaoelewa Kiingereza kuanza kuishusha hadhi filamu hiyo kabla ya kuiangalia.
Vile vile kuna utunzi mmoja mzuri sana wa maombolezo ya msiba wa mama wa mwanamuziki wa bendi moja ambayo mwanzoni mwa wimbo, mtunzi wa wimbo, akieleza hisia zake, alisema: “Mama I misses you” badala ya kusema kwa usahihi “Mama I miss you”.
Mtunzi huyo angekuwa salama kama angeyasema maneno hayo kwa Kiswahili, au asingeyasema kabisa ama angeyasema kwa kiingereza baada ya kuulizia kwa wataalam wa lugha hiyo endapo angekuwa sahihi kama angesema alivyosema.
Hili tatizo la kupotosha lugha litatutesa sana Watanzania kwa sababu ya kupenda ujuaji. Hatupendi kuulizana ili tupate uhakika. Tungefanya hivyo wala tusingekuwa na filamu inayoitwa “Dilema”, wala “Darkness Night” na wala mwanamuziki yule asingesema “I misses you.”
Inawezekanaje kazi ya sanaa ifike hadi hatua ya mwisho na kosa lake? Hii haishangazi kwa sisi Watanzania tulio na tabia ya kutengeneza maneno yetu ya Kiingereza kama “salon”(pa kutengenezea nywele) kupaita ‘saloon’(gari dogo).
Kibao cha namba ya gari,” number plate”, kukiita “plate number, neno ‘ku-panic’ kulitumia kama kuhamaki badala ya maana yake halisi ya kuogopa na ‘ku-acquit’ kulitumia kama kuachiwa huru Mahakamani badala ya kusema “kuwa-acquitted” iliyo sahihi kwa maana hiyo.
Hata kwenye kiswahili chetu, hivi hili “lisaa limoja” linalotamba hata kwenye redio zetu, limeingiaje kwenye nafasi ya maneno sahihi “saa moja”?
Zaidi kwa upande wa suala la lugha, nashauri wachekeshaji wetu wasitumie kisingizio cha kuchekesha kuzungumza Kiingereza kibovu.
Wakitaka kutumia Kiingereza kutuchekesha, wasikiharibu bali watuchekeshe kwa lafudhi ya ajabu ajabu ya lugha hiyo inayopaswa iwe sahihi kama wanavyofanya wachekeshaji wa Kenya katika Vioja Mahakaman na Vitimbi.
Tukiachana na suala la lugha, waigizaji wetu wanapowaigiza Polisi wanaovaa sare za Jeshi hilo, ni vizuri watumie sare halisi badala ya sare kama za makampuni ya ulinzi ya watu binafsi (security guards).
Hali hiyo inaondoa uhalisia wa kinachoigizwa. Kama ni kukosekana kwa kibali cha kutumia mavazi hayo halisi, inakuwaje kwa Tanzania tu kisipatikane wakati dunia nzima kinapatikana kama tunavyoona kwenye filamu kutoka India, Marekani, Nigeria na kadhalika?
Usalama unahatarishwaje kwa mtu kuigilizia tu nguo fulani kwa masharti na uangalizi aliopewa? Hilo nalo tulirekebishe kupata uhalisia wa kazi zetu za sanaa hiyo.
Vile vile, ni vizuri waigizaji wetu wakaelewa hali halisi ya mifumo mbalimbali ya utendaji katika vyombo mbalimbali vya utendaji ili wasipotoshe wanapoigiza.
Kwa mfano, kwa askari wawili wa polisi,Afande ni yule tu mwenye cheo kikubwa zaidi ya mwenzie.
Na yeye tu ndiye anayetoa amri. Kwemye maigizo na filamu zetu, ni aghalabu kukuta askari wawili wanaitana “Afande” kila mmoja na yeyote anaweza kumuagiza mwingine atekeleze jambo!
Hii si sahihi kabisa na inapojitokeza, wanaoewa taratibu hizo, wanaidharau filamu nzima kwa kuiona ni ya ubabaishaji.
Naomba niishie hapa nikisisitiza kwa wasanii wote Tanzania tuwe makini na uhalisia kwenye sanaa zetu. Kwa sasa tumepiga hatua kubwa.Tusitie dosari kazi zetu nzuri kwa makosa niliyoyaeleza.
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?


