Mtoto wa Keenja arudishiwa dhamana
March 27, 2008
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana ilimpa dhamana mtoto wa Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Charles Keenja, Eliasa Keenja, saa chache baada ya kumfutia dhamana hiyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya wakili wa utetezi, Edward Chuwa, kuiomba mahakama kuangalia upya amri iliyotolewa dhidi ya mteja wake kutokana na kupata msiba wa mume wake wiki iliyopita.
Awali, mtuhumiwa huyo alifutiwa dhamana baada ya kutokufika mahakamani hapo wakati kesi yake ilipokuja.
Keenja na wenzake wawili wanakabiliwa na kesi ya wizi wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya sh milioni 300, mali ya raia wa China, Li Jinglan.
Hakimu Benadeta Beda kabla ya kumpatia dhamana alimtaka wakili huyo kwenda kwa Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Sevangilwa Mwangesi, ili kupata msaada zaidi.
Naye hakimu mfawidhi baada ya kuitisha jalada na kulipitia, alisema hana mamlaka ya kupangua uamuzi huo na kuwataka waende Mahakama Kuu kwa uamuzi zaidi.
“Mahakama ikisha kutoa tamko hakuna wa kulipangua hadi mkate rufaa Mahakama Kuu, kwa hiyo mimi sina uwezo wa kufanya hivyo,” alisema Mwangesi.
Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Charles Keenja, pamoja na wakili, walikwenda kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Semistokes Simon, ambako ilitolewa amri ya kuliangalia upya jalada hilo na kumpatia dhamana.
Hakimu Beda aliliangalia upya jalada hilo na kumpatia dhamana ya masharti, ya kuwa na wadhamini wawili na kuwasilisha hati yake ya kusafiria.
Baada ya kutoa dhamana hiyo, Hakimu Beda alisema anajitoa katika kusikiliza kesi hiyo. Kesi imeahirishwa hadi Aprili 8, mwaka huu itakapotajwa.

