Mtangazaji Redio Uhuru auawa na majambazi Dar
December 21, 2007
MTOTO wa Kaka wa Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Phillip Mangula, Japhet Kenneth Mangula (26), ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi na kufa papo hapo.
Tukio hilo lilitokea juzi katika eneo la Kiwalani, jijini Dar es Salaam majira ya saa 5:00 usiku, wakati akiwa baa na marafiki zake. Marehemu alikuwa Mwandishi wa Habari Mwandamizi wa Redio Uhuru.
Akizungumza na mwandishi wa Mwananchi kwa njia ya simu jana kutokea Njombe, mkoani Iringa, Baba mkubwa wa Marehemu, Philip Mangula, alithibitisha kifo hicho na kusema marehemu alifariki dunia baada ya kupigwa risasi mbili usoni na majambazi hao.
Mangula alisema kabla ya kumuua marehemu, majambazi hao walivamia baa hiyo alipokuwa na marafiki zake wakinywa ndipo majambazi hao walipowalazimisha wateja wote walale chini na kuwapora kila kitu walichokuwa nacho. Mangula alisema baada ya majambazi hao kutoa amri hiyo, marehemu alikaidi na kuanza kuhoji kilichokuwa kinatokea na ndipo majambazi hao wakasema analeta kiburi kisha wakamfyatulia risasi kichwani iliyomuuwa papo hapo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Redio Uhuru, Juma Penza, alidhibisha tukio hilo na kuwaeleza ndugu na marafiki wa marehemu waliofika ofisini kwake kuwa risasi iliyomuua marehemu ilifumua kichwa chake.
Penza alisema alipigiwa simu usiku na kufika eneo la tukio, ambapo alikuta mwili wa marehemu ukiwa umelazwa chini baada ya majambazi hao kutokomea kusikojulikana huku marehemu akiwa ameharika sana kichwani, kisha wakachukuwa mwili na kuupeleka hospitali ya Amana usiku huo.
Taarifa hizo pia zilidhibitishwa na mdogo wa marehemu, Malumbo Mangula ambaye alisema ni kweli ndugu yake alipigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi na kwamba mwili wa kaka yake uko katika hospitali ya Amana. Baadhi ya marafiki waliokuwa na marehemu katika baa hiyo walizungumza na mwandishi wa habari hii walisema wakiwa na marehemu ghafla kundi la watu liliingia katika baa hiyo wakitokea nyuma ya meza yao na kuamrisha watu wote waliokuwepo hapo baa walale chini na kutoa vitu vyote walivyo navyo mifukoani , lakini marehemu alisimama na kuuliza kwani kuna nini hapa.
Mmoja wao alisema marehemu kusema hivyo, alisikia mlio wa risasi kisha akalala na kuitupa simu yake uvunguni mwa meza na baada ya majambazi hao kuondoka, aliamka na kumkuta marehemu akitokwa damu nyingi kichwani akiwa ameshakata roho. Meneja Uhusiano wa Redio Uhuru, Fred Mkanza, alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Amana na unataratibu wa kuusafrisha kwenda Kijiji cha Imalinyi Wilayani Njombe mkoani Iringa kwa mazishi.
Mkanza alisema mwili utaagwa leo saa sita mchana na saa saba na kisha kusafurishwa kwenda Njombekwa mazishi yatakayofanyika kesho.
KUTOKA: MWANANCHI

