Mradi wa vitambulisho vya uraia usifanyiwe ufisadi
May 27, 2008
BAADA ya kilio cha muda mrefu kuhusu kupatikana kwa vitambulisho vya uraia, hatimaye serikali imeamua kutangaza zabuni kwa kampuni mbalimbali kujitokeza ili kupata tenda hiyo.
Nasema kilio hiki cha muda mrefu, kutokana na ukweli kwamba kila mwaka utasikia serikali inasema mwaka huu maandalizi ya vitambulisho yako tayari lakini matokeo yake huwa mabaya.
Nimeanza kusikia suala la vitambulisho hivi hata sijaanza elimu ya msingi, mpaka imefikia hatua nimekata tamaa, kwa kuwa viongozi wetu wamekuwa mabingwa wa ‘porojo’.
Kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inafanikiwa kutengeneza vitambulisho wakati wa zoezi la uchaguzi mkuu, serikali hii inashindwaje kutengeneza vitambulisho vya uraia kwa kipindi chote hiki?
Hapana, umefika wakati wa kubadilika jamani!
Tanzania ni nchi inayosifika kwa amani, umoja na utulivu wa hali ya juu, licha ya dosari mbalimbali za mapigano kama wale ndugu zetu Wanchari na Walanchoka, wanaopigana mapanga na kuchomeana nyumba, Tarime kila siku.
Lakini licha ya mapigano haya kuwa ya koo ni dosari kubwa kwa taifa linaloheshimika duniani, inawezeka ni mapigano ya enzi na enzi, tangu mababu zetu, umefika wakati sasa serikali kuchukua maeneo yanayosababisha mapigano na kujenga vitu kama magereza kwa ajili ya kutumikia jamii.
Ni ukweli ulio wazi kwamba matengenezo ya vitambulisho hivi yanahitaji maandalizi makubwa, yakiwemo ya fedha na mambo mengine ambayo naamini yamo ndani ya uwezo wa serikali.
Pamoja na ukweli kwamba dhana nzima ya kitambulisho cha uraia bado ni ngeni miongoni mwa Watanzania wengine, sasa umefika wakati wa kubadilika haraka.
Wiki iliyopita Mratibu Mkuu wa Vitambusho taifa, Dickson Maimu, alisema mambo yote yamekamilika licha ya matatizo yaliyokuwepo huku akiyasihi makampuni ya kizalendo kujitokeza haraka.
Mtaratibu huyo anasema kumekuwa na jitihada mbalimbali za serikali zinazofanywa ili kuhakikisha na wageni wote wanapatiwa vitambulisho vya uraia.
Anasema jitihada hizo hazikuweza kuzaa matunda yaliyotarajiwa kwa kipindi kirefu kutokana na sababu mbalimbali, mimi nasema jamani viongozi wamezidisha sababu kwa kila jambo lililo mbele yao.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Joseph Mungai, aliliambia Bunge kuwa serikali imetenga kiasi cha fedha kwa ajili ya mradi huo katika bajeti ya mwaka 2006/2007. Swali, je, fedha hizi zilikwenda wapi wakati wote huo? Kama ilivyo kawaida, zilitafunwa na wajanja, au kwa jina maarufu sasa mafisadi ambao wanaonekana kuwa mchwa mkali katika matumizi ya fedha za serikali?.
Aibu hii itakwisha lini jamani? Nchi za Kenya, Burundi na Rwanda mbona zenyewe zimefanikiwa kuwa na vitambulisho kama hivi kwa kipindi kirefu? Ina maana wao wana akili nyingi kuliko viongozi wetu?
Nani kaziroga nchi za Tanzania na Uganda ambazo zimeshindwa kutengeneza vitambulisho hivi?
Umefika wakati sasa kumaliza ujanja ujanja katika mpango huu.
Hali hii imesababisha nchi yetu kufuga majambazi na wezi wengi kutoka nchi jirani, kwani tumekuwa tukisikia kila siku katika mikoa yetu ya Kagera, Kigoma na Mara wakifanya uhalifu, tena wa kutumia silaha, nasema upole utatuponza! Watu waliokabidhiwa jukumu hili tunawaomba waache tabia ya kuwa na matumizi makubwa, tofauti na ilivyokusudiwa ili kufanikisha mpango huu.
Kwa siku za karibuni tenda hii imekuwa ikilalamikiwa sana na wadau mbalimbali kwamba imeghubikiwa na vitendo vya rushwa kila kukicha…sasa Maimu na timu yako hatutaki kuona nanyi mnajichotea mamilioni yetu na kuanza kuyaita vijisenti.
Vitambulisho vina umuhimu mkubwa sana katika nchi hii, ikiwa ni pomoja na kutambua mtu pale anapofanya uhalifu wa aina fulani, kutambua wakwepaji wa kurejesha mikopo kutoka kwenye benki zetu na kuweka kumbukumbu katika matukio ya uhalifu katika daftari.
Napenda kuishauri serikali kwamba kama watu wote waliopewa jukumu la vitambulisho wakivurunda, wachukuliwe hatua kali za kisheria, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
Wasifanye mchezo wa mawaziri wetu wanaotuhumiwa kwa kashfa za ufisadi eti nao wajiuzulu, tunasema hatutaki tabia hii iendelee.
Hawa watu wanatumia fedha za wavuja jasho wa nchi hii ambao wengi wao wanashindia mlo mmoja tu kwa siku.
Narudia wito wangu kwa wahusika kwamba katika zoezi hili hatutaki ujanja ujanja, tumechoshwa, tunataka kuona mafanikio kama inavyokusudiwa. Namalizia kwa kusema kuwa wale wote wenye dhamana ya kuongoza umma muogopeni Mungu.
Mungu ibariki Tanzania, fukuza mafisadi kwa nguvu kubwa na haraka, ili taifa letu lisonge mbele.
0756 511 845
Karedia2005@yahoo.co.uk
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

