Mkapa anamfunika Rais Kikwete kiutendaji - REDET

August 20, 2008

RIPOTI ya utafiti wa hali ya kisiasa nchini iliyotolewa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet) imeonyesha kuwa Benjamin Mkapa alifanikiwa zaidi kiuntendaji katika miaka kumi yake ya uongozi kuliko miaka miwili ya Rais Jakaya Kikwete.
Utafiti huo wa Redet uliyotolewa jana jijini Dar es Salaam, umeonyesha kuwa Mkapa aliweza kudhibiti mfumuko wa bei na kupunguza malalamiko ya wananchi dhidi ya serikali yake tofauti na serikali ya sasa ambayo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya kuongezeka kwa mfumuko wa bei unaosababisha hali ngumu ya maisha kwa ujumla.

Hata hivyo, pamoja na Mkapa na mafanikio hayo utafiti huo umeonyesha kuwa kiongozi huyo wa Awamu ya Tatu alitumia nguvu ya dola kuzima sauti za watu, tofauti na Rais Kikwete anayetumia umaarufu wake kuongoza.

Naye Dk Bernadeta Killian alisema katika mada yake kuhusu Mtiririko wa Kihistoria katika kudai uwajibikaji nchini aliyotoa jana katika mkutano huo kuwa, wakati Rais Mkapa alimaliza kipindi cha mwisho cha uongozi wake akiwa na matukio 18 ya watu kudai uwajibikaji kwa maandamano na migomo, Rais Kikwete ameshakuwa na matukio 34 katika kipindi cha miaka miwili tangu aingie madarakani.

“Na kwa vile kuna kipindi kilichobaki cha takribani miaka miwili na nusu hadi hapo 2010, huenda matukio hayo yakaongezeka zaidi,” alisema Dk Killian.

Alisema historia ya mtiririko wa kudai uwajibikaji Tanzania imeonyesha kuwa Rais Mkapa pia ameongoza kwa kuwa na serikali iliyopunguza malalamiko ya watu ilikinganishwa na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.

Alisema uongozi wa Rais Mwinyi ulitawaliwa na shutuma, rushwa na ukwepaji mkubwa wa kulipa kodi hali ambayo pia ilisababisha Tanzania kusitishwa misaada kutoka kwa baadhi ya wafadhili.

Hata hivyo, Dk Killian alisema wingi wa matukio hayo katika serikali ya Rais Kikwete umetokana na kuwepo kwa uhuru wa kutoa maoni na kujieleza zaidi kuliko ilivyokuwa wakati wa utawala wa Mkapa.

Alisema Mkapa aliweza kudhibiti malalamiko ya wananchi kwa kuwa alitumia nguvu ya dola zaidi na kufinya uhuru wa kutoa maoni tofauti na Kikwete ambaye anatoa uhuru huo kwa kiasi kikubwa.

Alisema matukio hayo yameongezeka pia katika uongozi wa Kikwete kutokana na kushindwa kutimiza matarajio ya wananchi ambao waliomchagua kwa wingi wakitarajia mabadiliko makubwa ya hali ya maisha.

“Matokeo ya utafiti iliyofanywa na Redet ulionyesha kuteremka kwa kiwango cha uridhishwaji na utendaji kazi wa seriakali miongoni mwa raia,” alisema Dk Killian.

Alisema madai ya wananchi kuhusu uwajibikaji wa serikali ya Mkapa yalihusu zaidi masuala ya ardhi, maeneo ya makazi, matumizi ya maliasili hasa madini na madai kuhusu kufahamishwa au kushirikishwa katika mapato na matumizi ya fedha za halmashauri.

Kwa mujibu wa Dk Killian, matukio mengi ya kudai uwajibikaji wa serikali ya Rais Kikwete yanaelekezwa kwa serikali yake na kuhusu matumizi mabaya ya rasilimali za umma ikiwamo ufisadi.

Naye Profesa Amos Mhina alisema serikali ya Rais Kikwete imekuwa na utiriri wa madai ya uwajibikaji kutoka kwa wananchi na kuyumba kwa dola yake kumesababishwa na mabadiliko ya hali ya uchumi.

Akitoa mada ya Mtiririko wa Kihistoria Mintarafu Majibu ya Dola kwa Madai ya Wananchi katika mkutano huo, Profesa Mhina alisema uwajibikaji wa dola kwa wananchi unategemea sana hali ya uchumi wa nchi.

Alisema hivi sasa hali ya uchumi nchini ni mbaya kutokana na mfumuko wa bei kuongezeka na kusababisha gharama ya maisha kuwa juu.

CHANZO: Gazeti la Mwananchi