MCL yalipa kodi ya Sh1.1 bn serikalini

December 21, 2007

KAMPUNI ya Mwanachi Communications Limited (MCL) inachangia kiasi cha Sh 1.1 bilioni kwa Serikali ya Tanzania kama kodi ya mapato kwa mwaka.

Kauli hiyo ilitolewa juzi (Jumatano) na Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Sam Shollei alipokuwa akiwapongeza wafanyakazi wake katika sherehe za kuuaga mwaka 2007 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2008 zilizofanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya MCL yaliyoko Tabata Relini, jijini Dar es Salaam.

Shollei aliwapongeza wafanyakazi kwa ufanisi pamoja na ushirikiano waliouonyesha kwa mwaka 2007 ambao umeileta MCL mafanikio katika soko la biashara ya magazeti.

Aliwataka waandishi na wahariri kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na haki ili kuboresha ubora wa magazeti yanayozalishwa na kampuni hiyo. Alisema pamoja na mafanikio ya kampuni hiyo kuongoza katika biashara ya magazeti nchini, pia ina mkakati wa kuboresha ubora wa gazeti kwa kuyapa sura mpya, kuhakikisha kwamba yanazidi kuongoza. Vile vile, MCL iliwatunuku zawadi wafanyakazi wake bora kutoka idara zote.

Miongoni mwa wafanyakazi hao waliotunikiwa zawadi hizo ni Muhibu Said, Salehe Ally, Subira Ruhinda na Hassan Muhidin kutoka Idara ya Habari. Wengine ni Barnabas Kalula (Usambazaji Morogoro); Moses Mbena (Uzalishaji); Vailence Simon (Usafirishaji); Ruth Liana(Rasilimali Watu); David Paul, Judith Kachopa (Matangazo) na Julius Mtui.

Mbali na wafanyakazi hao pia aliwapongeza waandishi wengine walioshinda tuzo za uandishi bora wa habari za rushwa na za uchunguzi. Waandishi hao ni Dismas Lyasa, Eric Kabendera, Tom Mosoba na Stella Barozi.

KUTOKA: MWANANCHI