Maximo awaona Chuji, Machuppa
January 29, 2008
MSHAMBULIAJI Athuman Machuppa, kiungo Athuman Iddi ‘Chuji’ na chipukizi Jerry Tegete wanatarajiwa kuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kitakachotangazwa leo na Mbrazili Marcio Maximo.
Hata hivyo, kipa Juma Kaseja hayumo kwenye kikosi hicho kitakachocheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya Malawi baadaye mwezi huu baada ya Maximo kuziba pengo la Ivo Mapunda kwa kumuita kipa wa timu ya taifa ya Zanzibar, Farouk Ramadhan.
Maximo anatarajiwa kumpa nafasi Machupa kuonyesha uwezo wake baada ya kumuona kwa mara ya kwanza mshambuliaji huyo mkongwe wakati Simba ilipoishinda Coastal Union kwa mabao 2-1, huku Machupa akikosa penati.
Tegete, ambaye hakuitwa kwenye kikosi cha Kilimanjaro Stars baada ya kutosajiliwa Ligi Kuu, ameonyesha cheche zake katika mechi alizopangwa na kocha Mserbia Kondic Dusan na kufunga mabao mawili, huku Chuji akionyesha umaridadi mkubwa katika mechi zote tatu ambazo Yanga imecheza jijini Dar es salaam tangu irejee kutoka Afrika Kusini.
Chuji alikuwa tegemeo katika sehemu ya kiungo ya Maximo, lakini akalazimika kuachwa baada ya kufungiwa kwa miezi mitatu na Shirikisho la Soka (TFF) kwa kosa la kutaka kumpiga mwamuzi.
Maximo, ambaye ana jukumu kubwa la kuhakikisha Stars inafuzu kucheza fainali zijazo za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Angola mwaka 2010, pia amemwita beki Kigi Makasi wa Mtibwa Sugar na kipa Farook Ramadhan wa Miembeni ambaye alionyesha ustadi mkubwa alipoichezea Zanzibar kwenye Kombe la Chalenji.
Machupa amekuwa kipenzi cha mashabiki, akionekana kama ndio dawa ya tatizo sugu la umaliziaji, lakini juzi alishindwa kudhihirisha hilo kwenye mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Coastal, akishindwa kuziona nyavu na kupoteza penati huku Maximo akiwa jukwaani.
Mshambuliaji huyo alikuwa akiichezea Atraco ya Rwanda na alikuwa akiongoza kwa mabao kwenye ligi ya nchi hiyo kabla ya kuhamia Simba.
Amekuwa akiziona nyavu katika mechi kadhaa za kirafiki ambazo Simba ilicheza katika kujiandaa kwa duru la pili la Ligi Kuu.
Maximo pia amewaita wachezaji wawili wanaosakata soka nchini Kuwait, Nizar Khalfan na Danny Mrwanda wanawe baada ya wawili hao kumfungia mabao akiwa na timu ya Kilimanjaro iliyotolewa katika robo fainali ya Kombe la Chalenji.
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

