Mawazo ya Ole Naiko ni ya hatari kwa utaifa

February 28, 2008

JUMATATU ya wiki hii, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel ole Naiko, alitoa taarifa kuhusu ripoti ya Richmond ambayo pamoja na mambo mengine, aligusia kuhusu utata uliogubika mazingira ya upatikanaji wa hati ya kupewa sifa ya uwekezaji kwa kampuni hewa ya Richmond Development Company, LLC. Kwenye taarifa yake hiyo, Ole Naiko alieleza kusikitishwa na namna Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe ilivyomhusisha yeye binafsi na TIC katika suala zima la utoaji wa hati ya uwekezaji iliyokuwa ikitoa nafuu kwa Kampuni ya Richmond.

Katika hatua moja ya taarifa yake hiyo, mbali ya kuilaumu kamati hiyo kwa namna ilivyomhusisha yeye na TIC katika uchunguzi wake na hususan mwelekeo wa vitu alivyotakiwa kuwasilisha na maswali walioulizwa baadhi ya mashahidi kuhusu TIC, Ole Naiko alizungumzia pia jambo jingine jipya kabisa.

Taarifa hiyo ya Ole Naiko katika mazingira ambayo msingi wake si rahisi kuyaelezea, alilalamikia kuhusishwa katika sakata hilo na watu wa Monduli na akamnukuu Askofu Thomas Laiser wa Monduli ambaye alitahadharisha na kukemea tabia iliyoibuka, ambako kila Mmasai anayeonekana anaitwa ‘Richmond’.

Aliendelea kueleza kuwa, kama nia ni kuondoa watu wa sehemu fulani ya nchi serikalini, wafanye hivyo kwa kuwatendea haki na si kuwajengea mazingira ya aina hii.

Mbali na hayo, Februari 26 mwaka huu, gazeti moja la kila siku lilimnukuu Ole Naiko akidai kuwa kuanguka kwa Edward Lowassa ni mwendelezo wa usafishaji wa kikabila dhidi ya Wamasai wa Monduli!

Tunasema mawazo haya ya Ole Naiko ni hatari kwa taifa kwa sababu, mtu anayejua siri ya utangamano na mshikamano wa Tanzania licha ya kushangaa na kusikitika, ataona kama anachokozwa yeye na taifa lake.

Hakuna nchi inayojivunia mshikamano usioangalia makabila kama Tanzania katika Afrika. Ingawa ukabila upo Tanzania, ni kwa kiwango cha chini ikilinganishwa na nchi kama Kenya, Nigeria, Rwanda, Uganda na nchi nyingine.

Kutokana na kauli hii, tunadhani kwamba Ole Naiko alitamka suala hili kabla ya kulifikiri ama kama ni vinginevyo tunapata wasiwasi juu ya uelewa hata elimu yake.

Kama suala ni ukabila, mbona shujaa Hayati Edward Sokoine ambaye kimsingi pengo lake ndilo lililowaibua akina Lowassa na wengineo, alikubaliwa na kupendwa?

Kwa kweli tukianza kufuatilia ukabila wa watu, taifa letu halitafika kokote, zaidi ya kubaki katika wakati mgumu pamoja na kupoteza amani yetu ambayo tumekuwa tukijivunia kwa muda mrefu.

Mawazo haya ya kikabila licha ya kuwa ya kijima ni hatari kwa taifa ambalo kwa miongo zaidi ya mitano limekuwa likijitahidi kupambana na hisia za ukabila, ujimbo, udini na hali ya kipato cha mtu.

Kwanini waanze kupigwa vita Wamasai wakati tunaweza kuwavumilia Wahindi ambao wamekuwa kila mara wakihusishwa na kashfa za fedha nyingi za umma?

Suala la ukabila hivi sasa ndilo lililowaingia jirani zetu wa Kenya katika hali ya mgogoro wa kisiasa ambao umegharimu maisha ya watu wengi ambao Rais Mwai Kibaki anaonekana kuendelea kuwapo madarakani kutokana na ukabila.

Ole Naiko anataka kupandikiza suala jingine, ili Watanzania waache kujadili suala lenye maslahi ya taifa na kujadili suala ambalo halina manufaa kwa nchi. Tuachane na mawazo yake ambayo ni hatari.