Matumizi ya simu za mkononi hayaendani na vipato vya wengi

January 13, 2009

KILA mtu katika jamii anahitaji kuwa na maendeleo, ikiwa ni moja ya hali za kuiridhisha nafsi yake.

Tunapozungumzia maendeleo tunalenga mabadiliko katika mwenendo mzima wa maisha ya mwanadamu, baada ya kujibidisha kufanya jambo la kuleta badiliko hilo jema.

Inasikitisha kusikia kwamba nchi yetu ni moja ya nchi maskini duniani na kuangukia kwenye kundi la nchi zinazoendelea.

Kwa maana hiyo basi, ni lazima kuwe na vigezo vya mtu kuonekana ameendelea kutoka hatua fulani ya maisha hadi nyingine.

Kwa mfano, kama jana kwenye mtihani wa hisabati ulipata alama 30 na katika mtihani wa leo umepata 40, basi hapo tunasema ameanza kuwa na maendeleo.

Vile vile mfugaji ambaye mwaka jana alikuwa na ng’ombe watano lakini mwaka huu ana ng’ombe 10, naye pia ana maendeleo mazuri.

Kabla ya Serikali ya Awamu ya Pili, Tanzania ilionekana maskini sana, lakini mara baada ya kuruhusa kuingiza bidhaa ambazo awali zilionekana si za muhimu kwa ustawi wa Mtanzania tulishangaa kuona nchi imebadilika ghafla kimuonekano.

Mwaka 1987 tukaanza kusikia na kuona luninga, majokofu, magari ya kifahari, vipodozi vya kila aina na nguo za kila namna na hapo kila mwenye uwezo alinunua kile alichokifurahia.

Baada ya muda fulani zikaingia simu za mkononi, maarufu kama mobiteli.

Kutokana na kuwa ghali kila aliyekuwa nayo alihesabika ameendelea au mwenye uwezo wa kifedha.

Kisaikolojia waliokuwa na simu walionekana kama watu wa kipekee na ndiyo maana kila aliyepata fedha zake alinunua simu kwa gharama ya kujinyima hata kula.

Hata hivyo kadiri teknolojia ya mawasiliano ya kisasa ilivyopanuka na kuenea ilionekana kuwa Watanzania walikuwa mstari wa mbele kuichangamkia. Kwa maana ni watu wanaopenda maendeleo.

Walio wengi maendeleo yakawa ni kuwa na simu na wala si jambo jinginelo katika maisha ya kila siku.

Katika maisha ya kawaida ya mfanyakazi wa kima cha kawaida inaaminiwa kuwa kipato chake ni wastani wa dola moja ya Marekani.

Lakini uhalisia wa matumizi ya kumuwezesha kuishi akiwa amejipatia japo kipoza njaa, gharama yake ni takriban dola tatu kwa siku.

Mchanganuo katika familia moja ya kawaida, yaani baba, mama na watoto wanne kwa matumizi ya mwezi yanafanana kama ifuatavyo:

Chakula ni wastani wa sh 150,000; kodi ya nyumba ni sh 20,000; kuchangia umeme sh 20,000; maji sh 30,000; na nauli ya baba kwenda kazini na kurudi ni sh 30,000 na matumizi mengine sh 10,000; jumla ya vyote ni sh 260,000 kwa mwezi.

Sasa tuitazame hii familia ambayo baba kipato chake hakizidi sh 120,000 wa mwezi tena akiwa amebahatika kuwa na mwajiri mwenye utu.

Sasa kama bajeti nyingi zinafanana, hivi watu wanaishije majumbani mwao hata tunawaona wakiwa barabarani kila siku?

Hapo wengine tunakuwa na alama za kuuliza na kutuaminisha kwamba bila shaka baba yule ana namna nyingine za kuongezea kipato.

Iwe kupitia kwa shughuli anazofanya mkewe za kuuza mandazi au yeye hujiongezea kipato kwa kumdanganya mwajiri wake na pengine kumwibia kabisa.

Lakini tukiwa na bajeti hiyo kichwani, hebu tuone pia kuwa kila Mtanzania anajibidisha kuwa na simu ya kiganjani ambayo inaongeza mzigo wa matumizi yasiyoepukika ili mtu aone maana ya kuwa na kifaa hicho.

Kwa kadiri makampuni ya biashara ya simu yanavyosukumwa na upepo wa ushindani wa kibiashara, kidogo kumekuwa na unafuu wa gharama za kumiliki na kutumia simu binafsi.

Hata hivyo matumizi ya simu yanatofautiana kati ya mtu na mtu maana wengi hasa wafanya biashara huzitumia simu kwa mawasiliano ya utafutaji wa pesa, si kutumia pesa bila kuingiza pesa.

Lakini bado wapo wanaowasiliana kwa maana ya kujuliana hali na kupeana taarifa fulani za kimaisha.

Ingawa bajeti zetu kwa kweli ni ngumu lakini watu bado tumeng’ang’ania chombo hiki.

Kama nilivyoeleza kuwa mara nyingi matumizi ya simu nayo yanaweza yakaongozwa na uwezo wa mtu kifedha, kwani wapo wanaotumia wastani wa sh za Tanzania zisizopungua 30,000 au zaidi kwa siku moja.

Na kwa walalahoi walio wengi hujibana akijitahidi ili atumie wastani wa sh 1,000 kwa siku, hata, hivyo wakati mwingine hudai hana mtu wa kumpigia.

Gharama hii kwa mwezi yaweza ikawa sh 30,000 na tukiongeza katika bajeti yetu pale juu tunapata jumla ya sh 300,000.

Je, familia hii haioni kuwa ina kuwa na maisha magumu kila wakati kwa kushindwa kuishi kulingana na kipato?

Bajeti hii ambayo hailingani na vyanzo vya mapato ndivyo vinavyomsaidia ibilisi kumwingia mtu ashiriki kufanya maovu ili awe na kipato cha kukidhi hitaji la bajeti.

Kumbuka bajeti yetu haina gharama kwa ajili ya watoto kwenda shule kila siku sasa wewe msomaji utatafakari hilo mwenyewe.

Lakini pengine niwashawishi wenzangu kuwa ni heri mtu ujiweke katika maisha yanayolingana na unachopata ili usiije ukashawishika kuingia majaribuni na kuwakosea wanadamu na hata Muumba wako.

Ni kweli, kuwa na jokofu, gari, luninga na simu, vyote ni vya maana na muhimu kwa maisha yetu ya kila siku lakini ni vizuri zaidi kujipima ubavu wa kuwa na vitu hivyo.

Kuna rafiki yangu mmoja alinineleza atamuomba mjomba aliye nje ya nchi amletee gari ili naye aweze kuzalisha pesa.

Lakini nilimwambia rafiki yangu kuwa wazo lake ni jema lakini endapo atabahatika kuletewa gari kwa hali aliyonayo hatamudu kulifanya litembee barabarani.

Baada ya rafiki yangu kufikiria gharama ya mafuta pekee lakini akasahau kuwa kuna zaidi ya mafuta ili gari liwe barabarani kila siku.

Si nia yangu katika makala hii kuwakatisha tamaa Watanzania wanaodhani kuwa kumudu kununua simu ndiyo yote katika yote bila kufikiria gharama za muda wa maongezi za kila wakati ili ilete maana ya mtu kuwa na simu.

Ili maendeleo haya yasiwe mzigo wa kupasua vichwa vyetu, ningedhani ni vema tusijiingize kuiga maendeleo ya juu kabla ya kutosheleza bajeti zetu za kila siku, hususan hitaji la ugali na shule kwa watoto.

Nisingependa kulaumu walio na bahati mbaya ya kuwa na simu kwa kufuata mkumbo bali naamini kila mtu afungapo safari huwa tayari amekuwa ameagana na kisigino chake kwa ajili ya safari hiyo.

Binafsi nimeliona tatizo la kwamba simu zetu zinafanya maisha kuwa magumu siku kwa siku, maana watu hutumia gharama hata kupunguza bajeti ya mlo wa nyumbani.

‘Kupanga ni kuchagua,’ lakini hekima inatakiwa katika maamuzi tunayofanya.

Tuwe na simu na tuzitumie kadiri kipato kinavyoturuhusu.

Makala hii imeandikwa na Daniel Misheto na kuchapishwa na Gazeti la Tanzania Daima la leo


Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post
 |  TrackBack URI for this post

Comments

3 Responses to “Matumizi ya simu za mkononi hayaendani na vipato vya wengi”

  1. MOMBE on January 15th, 2009 11:49 am

    NI KWELI KABISA KIPATO CHA MTANZANIA HAKILINGANI KABISA NA MATUMIZI YAKE YA KILA SIKU,KIUJUMLA TEKINOLOJIA INAFAIDA NA HASARA ZAKE KATIKA MAISHA YA MWANADAMU,KWA MFANO TUKIZUNGUMZIA MATUMIZI YA SIMU ZA MKONONI,NIUKWELI USIO PINGIKA KUA SIMU ZA MKONONI ZIME RAHISISHA SANA MAWASILIANO ILA KIWANGO KINACHOTOZWA NA MAKAMPUNI YANAYO TOA HUDUMA HII NICHA JUU MNO KIASI KWAMBA KWA WATANZANIA WALIOWENGI INAKUA VIGUMU KUMDU GHARAMA HIZO JAPO KILA MTU ANAPENDA KUTUMIA TEKINOLOJIA HII.KWAMAONI YANGU NIJUKUMU LA SERIKALI KUHAKIKISHA KWAMBA MAKAMPUNI YA SIMU ZA MKONONI YANA TOZA VIWANGO VYA CHINI KULINGANA NA VIPATO VYA WANANCHI WALIO WENGI.NI HAYO TU.

  2. james on December 2nd, 2009 12:12 pm

    KWELI KABISA KIPATO CHA MTANZANIA HAKILINGANI KABISA NA MATUMIZI YAKE YA KILA SIKU,KIUJUMLA TEKINOLOJIA INAFAIDA NA HASARA ZAKE KATIKA MAISHA YA MWANADAMU,KWA MFANO TUKIZUNGUMZIA MATUMIZI YA SIMU ZA MKONONI,NIUKWELI USIO PINGIKA KUA SIMU ZA MKONONI ZIME RAHISISHA SANA MAWASILIANO ILA KIWANGO KINACHOTOZWA NA MAKAMPUNI YANAYO TOA HUDUMA HII NICHA JUU MNO KIASI KWAMBA KWA WATANZANIA WALIOWENGI INAKUA VIGUMU KUMDU GHARAMA HIZO JAPO KILA MTU ANAPENDA KUTUMIA TEKINOLOJIA HII.KWAMAONI YANGU NIJUKUMU LA SERIKALI KUHAKIKISHA KWAMBA MAKAMPUNI YA SIMU ZA MKONONI YANA TOZA VIWANGO VYA CHINI KULINGANA NA VIPATO VYA WANANCHI WALIO WENGI.NI HAYO TU.

  3. LUGAILA on January 26th, 2010 3:56 pm

    MATUMIZI BORA NI KWAAJIRI YA KUWAWEKA WATU KARIBU KWA MATHUMUNI YA KUWAWEKA KARIBU HASA KWA MAENDEREO YA TAIFA.

Got something to say?