Mashauri ya ardhi katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya

February 28, 2008

WIKI iliyopita nilieleza kwa utangulizi tu kuhusu Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya hasa kuhusu muundo wake. Leo hii ntaeleza namna ya kufungua kesi/shauri katika Baraza.

Mtu yeyote anayedhani haki yake ya umiliki au kutumia ardhi imevunjwa ama kukiukwa na mtu mwingine anaweza kupeleka shauri/malalamiko yake katika Baraza la Ardhi na Nyumba lililopo katika eneo analoishi au katika eneo ambako mgogoro umeibukia.

Kabla ya kufungua shauri katika Baraza, lazima mtu ajiridhishe kuwa thamani ya ardhi inayogombewa haizidi shilingi milioni hamsini (ikiwa mgogoro utahusu mgogoro wa kuondolewa mtu katika eneo/vacant posessio) na isizidi shilingi milioni arobaini na tano kama mgogoro unahusu mambo mengine kama vile fidia.

Shauri la ardhi linatakiwa kupelekwa katika Baraza la Ardhi na Nyumba katika fomu maalumu ya maombi (Application Form) ambayo katika form hiyo, majina ya mlalamikaji na mlalamikiwa lazima yaoneshwe. Pia katika fomu hiyo lazima Jina la Baraza ambako kesi inafunguliwa litajwe.

Katika fomu hiyo ya maombi, mlalamikaji anatakiwa pia kueleza anuani yake na ya yu/wale anaowadai. Anapaswa pia kueleza eneo linalogombewa lipo wapi, kiini cha mgogoro wenyewe na lini mgogoro ulianza. Mlalamikaji(Applicant) anatakiwa pia kuelezea thamani ya eneo/jengo linalogombaniwa.

Baada ya kujaza fomu hiyo, mlalamikaji anatakiwa kuifaili katika Baraza la wilaya husika na pia atatakiwa kumpelekea mlalamikaji nakala ya maombi/malalamiko aliyoyafaili katika Baraza. Lengo la kumpelekea mlalamikiwa nakala ya malalamiko ni kumpa mlalamikiwa kujibu malalamiko/madai husika. Baada ya kuyapata madai husika, mlalamikiwa atatakiwa ndani ya siku zisizozidi ishirini na moja (21) kujibu malalamiko husika.

Ikiwa hakuna madai kinzani (Counter claim), basi shauri litapangiwa siku ya kusikilizwa ambapo wadaiwa watatakiwa kuwasilisha vielelezo pamoja na mashahidi wao kuthibitisha haki ya kila upande. Ikiwa kutakuwa na madai kinzani basi mlalamikaji atatakiwa kujibu pia madai hayo kabla ya kuanza kusikiliza shauri zima.

Kwa ujumla wake mashauri yote katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya huendeshwa katika Mahakama ya wazi. Mtu yeyote wakiwemo waandishi wa habari wanaruhusiwa kusikiliza na kuripoti mashauri husika.

Katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya, wadaiwa wanaruhusiwa kujieleza mwenyewe au kuwakilishwa na mawakili au ndugu yeyote au mwanafamilia aliyeteuliwa na mhusika.

Kama mlalamikaji/mlalamikiwa ni kampuni iliyosajiliwa, itawakilishwa na mkurugenzi au ofisa mwingine aliyeteuliwa. Kwa mujibu wa sheria namba 2 ya mwaka 2002, Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya litatumia lugha ya Kiingereza au Kiswahili kama Mwenyekiti wa Baraza atakavyoelekeza, isipokuwa kumbukumbu na hukumu ya mashauri ya Baraza yataandikwa kwa Kiingereza.

Kwa ujumla wake, mamlaka ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya yapo katika maeneo yafuatayo: Kusikiliza kesi zote zinazotokana na Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999, Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999, Sheria ya Kusimamia Miliki za Kimila ya mwaka 1992. Vilevile Baraza lina mamlaka ya kusikiliza mashauri ya ardhi ambayo yanatajwa chini ya sheria zote ambazo zinatoa mamlaka kwa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya.

Tofauti sana na lililokuwa Baraza la Nyumba la Mkoa, Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya lina uwezo wa kutekeleza amri zake. Kwa maneno mengine lina mamlaka ya kutumia nguvu kutekeleza maamuzi yake yenyewe.

*Kwa maoni, maswali tuma kwa anuani hii, S.L.P 2616, Dar es Salaam. Barua pepe: magondza@yahoo.com Wakatabahu!