Majaji Bongo Star Search wanakanganya
December 21, 2007
SHINDANO la Bongo Star Search (BSS), linakua kwa kasi na kujinyakulia mashabiki kila kukicha kwa hapa nchini. Nimekuwa mmoja wa wafuatiliaji wa shindano hilo ambalo linarushwa na kituo cha televisheni cha ITV kila Jumapili.
Napenda kuwapongeza waandaaji wa shindano hilo kwa ubunifu wao katika kuwaibua wasanii wachanga.
Kupitia shindano hilo, tunashuhudia baadhi ya wasanii wanaoshika nafasi za juu wakipata fursa za kutengenezewa albamu zao, ikiwa ni pamoja na kuzisimamia katika kuzitangaza kitu ambacho naweza kusema kinakuwa ndoto kwa wasanii wengi wachanga.
Wengi wa wasanii wachanga, hasa wasiokuwa na uwezo kifedha, huwa wanapata wakati mgumu katika kutengeneza nyimbo na gharama za kujitangaza mpaka wafahamike, wao huita ‘Promo’.
Pia mshindi kwenye shindano la BSS, hupewa zawadi za kurekodi albamu bure, fedha taslimu zinazomuwezesha kujikimu kimaisha msanii husika katika kazi zake.
Kutokana na wazo la kuanzisha shindano hilo, narudia kusema kwamba ni zuri na kila mpenda burudani atakuwa anakubaliana nalo, kwani huwa najisikia furaha ninapoona wasanii wachanga wenye vipaji wakipata msaada.
Pamoja na mazuri yote hayo yanayofanywa na waandaaji hawa wa BSS, lakini pia wanayo mapungufu, hasa kwa upande wa waamuzi wakati wa utoaji wa maamuzi, kwa kweli utoaji wao maamuzi unakarahisha.
Nimeamua kuyazungumzia haya kutokana na mapenzi yangu niliyonayo katika fani hii ya muziki. Sitakuwa tayari kuona mambo mazuri yakiwa yanakwenda kinyume nikayanyamazia, kwa hilo ‘I’m sorry’.
Nimekuwa makini sana kuyafuatilia mashindano hayo, lakini nimeona nijaribu kuchangia, nia ikiwa kutoa changamoto ili kuyaboresha zaidi.
Jambo la kwanza ambalo limeweza kunisukuma kukaa chini na kuanza kundika, hasa ni kuhusu majaji kuwa na kauli mbaya za kebehi kwa washiriki, kwamba wanatumia nafasi zao kuwadhihaki.
Inafikia wakati mwingine nakuwa na mawazo ya kumfikiria jaji Salama Jabir kwamba huwa anakwenda pale akiwa amepata kilevi chochote kile kutokana na mambo anayokuwa anafanya, ikiwamo kujificha chini ya meza ikiwa ishara ya kuonyesha kutoridhishwa na uimbaji wa mtu anayeimba kwa wakati ule.
Pia kuna baadhi ya maneno ambayo yamekuwa yakinihuzunisha anapoyatoa kwa mtu anayefanya vibaya.
Mara nyingi hupenda kuwauliza swali ambalo si la kistaarabu: “Unafanya kazi gani? Na labda kwa mfano mshiriki akijibu kuwa ni mkulima, basi Salama na jaji mwingine, Master Jay wamekuwa wakiwavunja moyo kwa kuwaambia: “Acha muziki, afadhali ukalime mtu wangu, najua unaupenda muziki, lakini muziki haukupendi.”
Kwa kauli kama hizi si kwamba tutegemee kuzalisha wasanii zaidi, ila kuna uwezekano wa kuviua vipaji zaidi hasa kwa wale wanaokuja kujaribu bahati ya kutoka kupitia kwenye mashindano hayo.
Pia inawavunja moyo wengine waliokuwa na mawazo ya kutaka kushiriki.
Ningependa kuwashauri majaji watumie kauli nzuri ili kuwapa moyo wasanii waendelee kukaza msuli. Naamini itawezesha kuyaweka mashindano hayo katika sehemu inayostahili.
Pia kunakuwa na uwezekano wa kuendelea kujipatia umaarufu mwaka hadi mwaka, lakini iwapo wataendelea na maneno hayo ya kebehi, kuna uwezekano wa kujipunguzia mashabiki kila miaka inavyoendelea.
Ukiachilia mbali kuhusu hilo, pia jambo lingine linalonitia shaka ni kutokana na majaji hawa kuwa na tabia ya kupingana wao kwa wao mara kwa mara.
Kutokana na kupingana huko, kunanisukuma nijenge hisia ya kuamini kuwa upo uwezekano wa majaji hawa kutokuwa na muongozo unaowaongoza katika kumtambua msanii mwenye kipaji.
Kwa hili la kukosoana wenyewe ilifikia siku moja walijikuta wakibishana na baadhi wakitishia kususia kuendelea na kazi kutokana na wengine kumkataa mshiriki huku jaji mwingine akiwa anasisitiza ni mshiriki anayefaa kitu kilichosababisha jaji mwingine atishie kutoendelea kutoa maamuzi iwapo atamuona mshiriki huyo akionekana kwenye hatua iliyokuwa ikifuatia.
Mfano mwingine ulikuwa ni Jumapili iliyopita kulipotokea mkanganyiko baada ya mshiriki mmoja kuimba wimbo wa mmoja wa wanamuziki wa hapa nyumbani, ambako Salama akamponda kwa kumwambia kwamba ameimba tofauti kabisa na mwanamuziki husika wa wimbo huo.
Lakini Master Jay alisema hakufurahishwa naye kwani aliimba kawaida sana na jaji wa mwisho Rita yeye alimpongeza msanii huyo na kumwambia kwamba amemfurahisha kwa sababu amechukua wimbo wa mtu mwingine na kuufanya wake.
Sasa matukio kama haya yanaendelea kunitia shaka kuwa huenda kuna mapungufu kwa majaji katika kuelewa vigezo hasa vinavyostahili kutumika katika kumpata nyota wa BSS.
Kuna wakati nikafikiria huenda nyota wa BSS si kwamba anapatikana kwa vigezo ambavyo wameviweka bali anapatikana kwa kuwafurahisha majaji hawa.
Napenda kutoa ushauri kwamba kama wao wanakuwa si wataalamu wa masuala ya muziki, basi ni vema wangekuwa wanawachukua walimu kutoka Bagamoyo, wenye uwezo mkubwa wa kutambua vipaji.
Si kwamba kila mwenye kuupenda muziki huwa anakuwa na uwezo wa kumtambua vizuri msanii au mwanamuziki mwenye kipaji kama inavyofikiriwa.
Sidhani uwezo wa jaji hupimwa kwa kuendesha vipindi vya muziki na kuponda kazi za wasanii, bali jaji mzuri hutokana na yeye mwenyewe kuwa mwalimu mzuri wa kazi husika.
Hii ni sawa na kuwa mwalimu wa hesabu wakati hesabu zenyewe huzijui. Ni sawa na kuwa jaji wakati hata kwaya ya shule haujawahi kuimba wala kusomea muziki wenyewe, hapo kutakuwa na uwezekano wa kuwapata wasiokuwa wasanii wababaishaji.
Suala la kutambua kipaji si karama kama inavyodhaniwa kuwa mtu yeyote anaweza akaamka na kuanza kuibua vipaji.
KUTOKA: TANZANIA DAIMA

