Macho ya taifa yanakutizama Rais Kikwete
August 20, 2008
ENDAPO Rais Jakaya Kikwete, atatumia nafasi ya hotuba yake kwa Bunge hapo kesho kuelezea maamuzi mbalimbali aliyochukua au atakayochukua, kwa kiasi kikubwa kutaamua kama rais anastahili nafasi nyingine ya kuliongoza taifa letu mwaka 2010.
Atakaposimama kuzungumza na wawakilishi wetu bungeni na kupitia kwao, taifa zima kwa hakika, kutaonyesha kile ambacho wengi wa wakosoaji wake tumekuwa tukikinyoshea kidole, nacho ni ukosefu wa uthubutu wa kufanya maamuzi magumu na ya makusudi.
Kwa muda mrefu sasa, matumaini ya Watanzania ambayo yalipandwa mioyoni mwao wakati wa kampeni za urais na hasa katika mikutano mbalimbali ambapo mgombea Kikwete, alionekana kuvutia wengi, matumaini hayo yamepungua na kwa wengine yametoweka kabisa.
Saa na wakati huu, Watanzania wameyaweka mashakani matumaini yao na sasa kila mmoja anajaribu kufanya mambo kwa ajili yake yeye mwenyewe zaidi na familia yake.
Yale matumaini ya kujenga “Taifa letu” ambamo ndani yake kila Mtanzania anafurahia matunda ya uhuru, matumaini hayo yameanza kuzimika na kama yangekuwa maembe bolibo tungesema yameanza kudoda.
Hivyo naamini hotuba ya Kikwete kesho kwa taifa kama haitakuwa ya kuleta matumaini kwa Watanzania basi itakuwa ni ya kukata maini na kuwafanya watu wakate tamaa zaidi na kujihisi kushindwa.
Siwezi kuona jinsi gani nyingine Rais Kikwete na waandishi wake wa hotuba watatumia muda kutoa hotuba yoyote ile isipokuwa ile ya matumaini.
Hotuba ya kisiasa Watanzania hawaihitaji, hotuba ya kufafanua mambo hawahitaji, hotuba ya kutoa udhuru wa jambo hawaihitaji; wanachohitaji ni hotuba itakayowapa matumaini.
Matumaini kuwa mambo hayataachwa yaendelee kuharibika; matumaini kwamba rais wetu ana ‘control’ ya mambo nchini, matumaini ya kwamba hakuna mtu aliye juu ya sheria hata kama jina lake likitajwa kengele zinalia.
Matumaini ya kwamba Tanzania moja, yenye mafanikio na yenye nafasi sawa kwa watoto wake ipo na itaendelea kuwepo na pale ambapo haipo basi itafanywa iwepo! Hotuba ya Kikwete kesho isipokuwa na matumaini kwa hakika itakuwa inaongeza kina cha shimo ambalo utawala umejichimbia na kama nilivyosema huko nyuma asipoangalia atakuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania kutawala kwa mhula mmoja!
Ni kitu gani basi tukikisikia katika hotuba ya Rais Kikwete kitaashiria pambazuko jipya la matumaini saa na wakati kama huu nchini mwetu? Ni mambo gani ambayo Rais Kikwete akiyazungumzia na kwa jinsi gani yataashiria kuwa kweli amedhamiria kuleta matumaini kwa wana na mabinti wa taifa letu?
Naamini kuna mambo makubwa mawili ambayo Watanzania wanasubiri kusikia rais atasema nini juu yake. Na katika hicho atakachosema Watanzania wanatarajia kuona vitendo vinavyoendana na uzito wa mambo hayo.
Mambo hayo ni suala la ufisadi uliofanyika Benki Kuu na kusababisha wizi wa mabilioni ya shilingi na pili ni suala la nafasi ya Zanzibar katika Muungano.
Hilo la pili ndilo jambo kubwa zaidi na changamoto inayoukabili urais wa Kikwete na kwa hakika utaamua katika historia, atakumbukwa kwa lipi. Mambo haya mawili kwa kweli ni mifano ya mambo mengine madogodogo ambayo yanaikabili nchi yetu.
Suala la Benki Kuu likiwakilisha matatizo mengine yote ya ufisadi kwenye vyombo na taasisi za umma wakati suala la Zanzibar likiwakilisha matatizo ya kisiasa na kikatiba ambayo yanawakabili watawala wetu leo hii. Katika haya mawili Rais Kikwete hana budi kuleta matumaini. Macho yetu yanakutazama Kikwete.
Jumatatu (juzi) Rais Kikwete alipokea ripoti ya uchunguzi wa EPA kutoka kwa mwenyekiti wa timu aliyounda kuchukua hatua kwa watu waliofanya “uhalifu” huo. Taarifa ya Idara ya Mawasiliano ya rais (Msiniulize kwanini inaitwa hivyo) iliyotolewa muda mfupi baada ya rais kupokea taarifa hiyo ilisema kuwa rais baada ya kuipokea “amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wa timu hiyo kwa kazi kubwa na ngumu lakini nzuri”.
Baada ya kusoma hapo nikaendelea mstari unaofuata ambao unasema hivi: “Rais, baada ya kuwa ameisoma na kuitafakari ripoti hiyo, ataitolea maamuzi katika siku chache zijazo”.
Sasa mwenzenu nikajiuliza, kama Rais bado hajaisoma taarifa hiyo na ndiyo amepewa, aliwezaje kusema kuwa kazi ilikuwa “kubwa na ngumu lakini nzuri”? Isipokuwa kukabidhiana kwao taarifa hiyo ambayo rais hakuiagiza ilikuwa ni kutuzuga sisi wengine wakati tayari walishajua kilichomo?
Sasa angalia mstari uliofuatia ambao ulisema hivi: “Taarifa rasmi ya maamuzi hayo ya rais itatolewa kwa wananchi.” Hapa ninapata matatizo mawili, la kwanza nimeshalisema mara nyingi na wengine wamelirudia vile vile kwamba rais hakupaswa hata kidogo kupokea ripoti hiyo.
Kitendo cha Johnson Mwanyika, Saidi Mwema na Edward Hosea kwenda kuandika ripoti kubwa na kuiweka kwenye jalada la rangi nyekundu linalometameta kilikuwa ni utovu mkubwa wa nidhamu na dalili ya wazi ya kutokutii maelekezo ya rais. Rais hakuwaomba waandike ripoti na waiwasilishe kwake.
Lakini pili ni kuwa rais hakusema kuwa wakiandika ripoti yeye ataitolea maamuzi baadaye, sasa kuna sababu gani kutuambia kuwa baada ya kuipitia na kutafakari rais “ataitolea maamuzi siku chache zijazo?”.
Katika maagizo yaliyotolewa na rais kupitia Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, hakuna mahali aliposema kina Mwanyika wampe taarifa rais ili achukue maamuzi. Hivyo kitendo cha wao kumrudishia mpira rais kinadhihirisha mambo makubwa mawili.
Kwanza, kina Mwanyika katika kufuatilia suala hili lote na katika kukusanya ushahidi wote, hawakuona hata kipengele kimoja cha sheria ambacho wangeweza kukitumia kuwafikisha wahusika wa EPA mahakamani.
Kwa maneno mengine, walipoangalia sheria ya wahujumu uchumi ya mwaka 1984 hawakuona makosa dhidi ya wezi wa fedha zetu Benki Kuu, walipopitia sheria ya Kuzuia Fedha za Magendo hawakuona chochote, katika kupitia sheria ya kusimamia mapato yanayotokana na uhalifu hawakuona kitu na katika sheria zote zinazohusiana na makosa ya fedha na ukiukwaji wa maadili, kote huko hawakuona sheria hata moja ambayo wangeweza kwenda mahakamani kuidai ili “watu na makampuni” yaliyohusika na “uhalifu huu” washitakiwe kwa hayo. Hakuna.
Ni kwa sababu hiyo baada ya kutumia muda mwingi, fedha nyingi waliona hakuna ujanja isipokuwa kumrudishia rais mpira huo. Kwa maneno mengine, Rais Kikwete, atakachoweza kufanya ni kile ambacho hakikuweza kupatikana mahakamani!
Kwa maneno mengine, Mwanasheria Mkuu na maofisa wa Usalama wa nchi yetu wamekwepa jukumu lao na matokeo yake wamekimbilia kwa “Mfalme Kikwete” ili atoe uamuzi wa mwisho na kuchukua hatua.
Lakini la pili ni kuwa kama Rais Kikwete ataamuru watu fulani wafikishwe mahakamani baada ya kuwatimua kazi, ina maana ya kuwa kina Mwanyika waliogopa kuwachukulia hatua watu hao kwa sababu waliona hawana uwezo huo au walitaka kibali cha rais ili wawafikishe mahakamani.
Kama hili ni kweli, basi kina Mwanyika na timu yake si tu wameonyesha udhaifu mkubwa wa kuwajibika bali pia wameonyesha kuwa hawafai kabisa kushikilia madaraka yao.
Ni kwa sababu hiyo kwa wao kutochukua hatua za kisheria jinsi walivyoagizwa na Rais Kikwete dhidi ya “watu na makampuni” na badala yake kwenda kuandika ripoti ndefu, basi natumaini Rais Kikwete kabla hajawawajibisha wezi wa EPA atawatimua kwanza kina Mwanyika, Mwema na Hosea kwa kujitungia majukumu ambayo hawakuagizwa wakitarajia kupigiwa vigelegele.
Hili liwe somo kuwa rais au kiongozi akikuagiza kufanya kitu kama hujaelewa unauliza na kama umeelewa unatekeleza, usiende kujitungia majukumu yako na kusubiri kubebwa juu juu kwa shangwe.
Ni kwa sababu hiyo basi naamini, hata kama Rais Kikwete atatangaza hatua dhidi ya watu na makampuni yaliyochukuliwa hatua, kufilisiwa au kurudisha fedha, ukweli utabakia kuwa pongezi hizo atazipata Kikwete na kwa hakika zitathibitisha kuwa timu ya Mwanyika ilipoteza muda kwani kama rais alikuwa na uwezo wa kufanya atakachofanya sasa kulikuwa na ulazima gani wa kuunda timu wakati ushahidi tayari alikuwa nao?
Kimsingi, tumezugwa na tumezugika. Na “next time” Rais Kikwete, asiunde tume au timu kama hizi na badala yake afanye anachoweza kufanya yeye mwenyewe kwani asipoangalia kila timu atakayotuma mwisho watamrudishia taarifa yeye.
Mwisho kuhusu hili la EPA ni kuwa kwa vile Rais Kikwete hakuiagiza taarifa hii na kina Mwanyika wakaamua kujitungia majukumu wao wenyewe, basi ni vizuri tena ni haki kwa wananchi kutoambiwa juu ya maamuzi ya rais kuhusu ripoti hii.
Badala yake Rais Kikwete kwa kuonyesha uthabiti wa uongozi wake aitoe ripoti hiyo hadharani na asiseme maneno mengi na badala yake amrudishie Mwanasheria Mkuu ili achukue hatua za kisheria dhidi ya watu wote waliohusika. Kikwete asifanye kazi ya Mwanasheria Mkuu au ya majaji wa Tanzania.
Kama hakuna wenye makosa waacheni huru, kama wapo wafikishwe mahakamani na chombo husika. Rais Kikwete awashukuru kwa ripoti hiyo na asitoe uamuzi wowote juu ya mtu yeyote na awaache kina Mwanyika wafanye walichoagizwa mwanzo.
Huu mtindo wa kukwepa majukumu kwa kuogopa kuchafuka alikokuwa nako Mwanyika lazima kukome. Alisema yeye amekuwa “msafi” wakati wote na sasa tunataka tuone “usafi” wake anaposhughulikia uchafu badala ya kumuacha rais asafishe pale ambapo yeye Mwanyika angeweza kusafisha. Kama hataki kukutana na uchafu, ajiuzulu na kutafuta kazi kiwanda cha sabuni!
Hilo jambo la kwanza
La pili naamini ni kubwa zaidi nalo ni nafasi ya Zanzibar katika Muungano. Hofu yangu ni kuwa Rais Kikwete hatagusia suala hili wala kulipa uzito unaostahili kwa kudhania ni suala la “tofauti za mitizamo” au “maneno tu ya wanasiasa”.
Bila ya shaka anaweza kufanya alichokifanya katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa saba ambapo alibakia kusema tu hivi: “Napenda kuitumia nafasi hii kuwatoa wasiwasi na kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa, taifa letu bado ni moja na watu wake bado ni wamoja.
“Tofauti za mawazo na fikira miongoni mwetu hazitakosekana. Naomba tuyaone mawazo na fikira hizo kuwa changamoto za kushughulikia katika kuimarisha umoja wa taifa letu na mshikamano wa watu wake.”
Kama alitarajia maneno hayo yangezima mjadala wa Zanzibar “nchi si nchi”alikosea, kwani sasa hata wakongwe wa muungano kama kina Mzee Mwakanjuki wanasimama kutangaza kuwa Zanzibar waliyoitumikia wao ni nchi! Uasi umeanza, usipozimwa usambaa!
Na ninapotumia neno uasi silitumii kirahisi; kinachoendelea Zanzibar sasa hivi ni uasi wa viongozi wa Zanzibar na si kujibishana maneno na viongozi wa Muungano kama Dk. Harrison Mwakyembe, alivyotuonyesha.
Wanachofanya ni kutangaza kuwa Zanzibar ni nchi ndani ya nchi nyingine na kimsingi wana “challenge” dhana nzima ya Muungano.
Wanachofanya viongozi wa Zanzibar ni sawa na wana ndoa wawili ambao walifunga ndoa halali na watu wakasherehekea. Ndoa hiyo ikadumu na kuzaa watoto. Baadaye mmoja wao anasimama na kusema kuwa yeye “bado single”. Yeye kapera.
Watu wanamuuliza mbona ulitia sahihi kuuacha uhuru wako na kuamua kujiunga na huyo mwenzio, iweje leo useme wewe “bachelor”? Yeye anasema, “shauri yake yeye mwenyewe, nani alimwambia abadilishe jina lake”?
Mwanandoa wetu huyo anaendelea kudai kuwa alipoingia kwenye ndoa alijua ataendelea kuwa kapera na hivyo akabaki na nyumba yake nyingine, mali zake, akaunti zake n.k na hivyo basi yeye bado kapera!
Hoja ambayo imekuwa ikitolewa mara nyingi kuwa ati kwa vile Zanzibar ina Rais, Baraza la Wawakilishi na Mahakama, basi Zanzibar ni “nchi” ni hoja ya kipuuzi, kwani ina lengo la kulaghai watu wa Zanzibar kusherehekea maisha ya Ukapera ambao hawana! Zanzibar siyo nchi.
Kama kuwa na chombo cha utendaji (urais), chombo cha kutunga sheria (Baraza la Wawakilishi) na chombo cha kutoa haki (mahakama) kunaifanya jamii ya watu kuwa nchi basi Marekani ni nchi hamsini! Majimbo ya Marekani ambayo yanajulikana kama “States” yana wakuu wa majimbo hayo (wanachaguliwa na wananchi wa majimbo hayo).
Majimbo hayo yana alama zote za kitaifa ikiwemo bendera, vikosi vya usalama na Mkuu wake (yaani gavana) anapigiwa saluti na vikosi vya ‘National Guard’ ambavyo ni vikosi vya kijeshi na viko chini ya majimbo hayo. Lakini majimbo hayo si nchi.
Majimbo hayo ni “mataifa” kwani kuanzia yaliyokuwa makoloni ya kwanza 13 ya Marekani na majimbo yaliyojiunga baadaye, makoloni hayo yalikuwa huru kila moja kutoka jingine na yakaamua kuungana kuunda tunachokifahamu sasa kama nchi ya Marekani.
Lakini tunaweza kukubali matumizi ya neno “nchi” kwa maana nyepesi na isiyo ya kisheria kwamba ni muendelezo wa jamii ya watu ambao awali walikuwa nchi na bado wanaendelea kuwa na utambulisho wao.
Ni kwa sababu hiyo utakuta maeneo yanayounda Ufalme wa Uingereza yakijulikana kama nchi kwenye orodha ya sehemu mbalimbali. Lakini siyo nchi kwa maana ya kisheria kwamba jamii ya watu ambayo ina uwezo wa kujiamulia mambo yake yote (si sehemu tu) na ambayo ina mamlaka yote ya hatima ya jamii hiyo pasipo kuingiliwa na mtu mwingine yoyote au jamii nyingine ya watu.
Utaona Zanzibar haikidhi maana hiyo. Kwa sababu haina mamlaka yote, na hata hiyo mamlaka ya kuwa na Rais, Baraza la wawakilishi na Mahakama, vyote vinakuja sababu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Ni Katiba ya Muungano inayotoa nafasi kwa kuwepo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hili tutalifafanua siku nyingine.
Lakini ninachoogopa mimi na ambacho kama Mtanzania sina budi kukilinda ni kuwa hawa ndugu zetu wa Zanzibar wanapigia kelele “nchi” wanachogombania kwa kweli ni kuwa nchi kamili, kisheria na kwa kila hali.
Hadi hivi sasa sijawasikia wazee hawa wa Zanzibar wakisimama kutetea Muungano na kutambua Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kukiri kuwa kuna nchi moja (ambayo ipo kikatiba).
Kama kuna mtu anataka kuzungumzia upungufu wa kikatiba kama ulivyoonyeshwa na Mahakama ya Rufaa katika kesi ya kilichodhaniwa kuwa ni uhaini, hilo linaweza kufanyika ndani ya Muungano.
Ni kwa sababu hiyo basi, ukimya wa muda mrefu wa Rais Kikwete kuhusu suala hili kumekuwa ni baraka kwa chembe za uasi zinazoendelea. Rais Kikwete alikiita hiki kinachoendelea kuwa ni “Tofauti za mawazo na fikira miongoni mwetu.”
Siamini na sijashawishika kuwa ni tofauti, bali ni jaribio la kutangaza kuwa kilichotokea Aprili 26 mwaka 1964 hakikuwa ndoa! Wanachotaka ni kusema kuwa ilikuwa ni kuchumbiana tu na sasa wanataka kuwa nje ya ndoa hiyo.
Kama hamuamini maneno yangu, Rais Kikwete asikike akitangaza kuwa Tanzania ni nchi moja na Zanzibar ni sehemu ya Muungano si nchi. Zanzibar hakutakalika, kwani CCM Zanzibar itameguka kutoka bara, watashikamana na CUF na kwa pamoja watatangaza nchi huru! Yaangalieni maneno yangu.
La maana katika kujadili matatizo ya ndoa yetu ni kusema kuwa kwanza ndoa ipo na halali; kwamba Muungano upo na halali. Na la pili ni kukubali ‘on principle’ and in fact kuwa zile nchi mbili zilizoungana hazipo tena (siyo kuwa moja ipo nyingine haipo) na kilichopo ni nchi moja. Ni kutoka hapo ndipo mjadala wa kero za Muungano unaweza kufanyika. Hili la kusema ati mmoja bado ni nchi na mwingine siyo nchi ni kuzugana.
Hivyo naamini katika yote atakayosema Rais Kikwete Alhamisi, endapo maeneo hayo mawili hayatagusiwa kwa kiasi ambacho kitaleta matumaini kwa wananchi wa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani (Zanzibar), basi atakuwa anashiriki katika kuivunja nchi yetu.
Na endapo Rais Kikwete ataacha uasi uendelee wa CCM kule Zanzibar au ukue kiasi cha kutishia kuvunja muungano wetu, nitakuwa wa kwanza kuitisha kujiuzulu kwake kama wananchi wa Pakistan walivyofanya na kusababisha Musharaff kujiuzulu juzi na akisita tutataka Bunge limfungulie mashitaka ya kibunge (impeachment) kwa kushindwa kutimiza kiapo chake cha kikatiiba. Hili halina utani. Asimame azime uasi huu, au atoe baraka zake.
‘On the question of the territorial integrity of our nation, the singular and undivided sovereignty of the United Republic of Tanzania under its two governments’ tusikubali kamwe mtu hata mmoja auchezee, kuudharau au hata kutishia kuuvunja kwa kuchezea maneno.
Kwani vurugu kubwa zimeanza duniani kwa maneno tu. Tujifunze kutoka Marekani na hatua ambazo rais wao mpendwa Abe Lincoln alichukua kuhakikisha kuwa Marekani inabakia kuwa moja, pale majimbo ya kusini yalipojaribu kutangaza kuwa ni ‘nchi huru’ nje ya shirikisho.
Kuna watu ambao wanataka tusihangaike hata kidogo kulinda Muungano wetu; watu hawa ni waoga wa kisiasa. Watu wa aina hii hawawezi kulinda mipaka ya nchi yetu.
Tanzania ni moja, nayo ni Jamhuri ya Muungano. Matatizo tuliyonayo kwenye ndoa yetu ni matatizo ambayo yanaweza kabisa kutatulika endapo CCM itaondoa ukiritimba wa kujiona ndio peke wanaopaswa kuutetea Muungano.
Tukishindwa kutetea Muungano ulivyo sasa kwa sababu ya manung’uniko ya hapa na pale, tutashindwa kuutetea inapokuja Tarime, ambako watu wengine wanajihisi si sehemu ya Jamhuri yetu au kule Pemba au kule Mtwara. Muungano upo na lazima tuulinde kwani ndiyo wito wa kila Mtanzania.
Kama Muungano utakuja kuvunjika, basi uje kuvunjika kwa sababu nyingine, isije kuwa ya watu kushindwa kuulinda na kufanya kila wawezalo kuuboresha. Jamani hata Marekani miaka 200 na ushei, baadaye bado wanahangaika na mahusiano kati ya serikali za majimbo na serikali kuu na wanazungumza na kufikishana mahakamani.
Hata leo hii Scotland na Great Britain wanahangaika kuhusu uhusiano wao; hata Qubec na Serikali Kuu ya Canada, wanahangaika kuhusu uhusiano wao pia.
Wanachofanya si kuacha Scotland kujitenga, au Qubec kujitenga, bali wanaangalia ni jinsi gani wataweza kuuboresha muungano vizuri zaidi. Tunashindwa kufanya hilo? Muungano ni suala la Watanzania wote na si suala la CCM, na wakati umefika jamii za kiraia na Watanzania kuanza kuutetea Muungano badala ya kuwaachia wanasiasa ambao wanaongozwa na vyeo vya kisiasa na ahadi za ukubwa.
Rais Kikwete tumuombee atakaposimama Alhamisi asimame kuliamsha taifa, kulipa matumaini na kuliongoza kuelekea kwenye neema kweli.
Vinginevyo, Watanzania tusimame kuliombea taifa letu kwa upya kabisa ili tuweze kupata kiongozi shujaa wa kweli, madhubuti wa vitendo na anayethubutu kuongoza, hasa wakati anapohitajika. Bado naamini Kikwete anaweza kuwa kiongozi, sijakata tamaa.
Wasiliana nami: mwanakijiji@jamiiforums.com

