Mabondia watamba kumalizana ulingoni Dar Jumamosi
November 18, 2007
BONDIA maarufu nchini, Maneno Oswald ‘Mtambo wa Gongo’ ameapa kuwa atamnyamazisha mpinzani wake, Yusuph Jibaba leo katika pambano lao la raundi nane la uzito wa Super Middle litakalopigwa kwenye Ukumbi wa Super Stereo Temeke jijini Dar es Salaam.
Oswald alisema atahakikisha mpinzani wake anazindukia hospitali kwa jinsi atakavyomshushia kisago cha nguvu.
”Kutokana na historia yangu huwa mimi sina maneno mengi ila huwa nina kawaida ya kuzima kelele za mpinzani wangu kwa vitendo ulingoni hivyo namwambia huyo atakosa nguvu za kuondoka leo na atazindukia hospitali,”alisema Maneno
Wakati Oswald akitamba, mpinzani wake Yusuph Jibaba alisema siku ya leo itakuwa ni siku ya kukumbukwa kwa familia ya Maneno kwa vile atamstaafisha kucheza mchezo wa masumbwi.
” Havuki raundi ya tatu huyo na ataondolewa jukwaa kwa machela kwa kipigo nitakachokitoa”alisema jibaba
Raisi wa Shirikisho la Masumbwi Tanzania, Emmanuel Mlundwa alisema pambano hilo litatanguliwa na mapambano ya utangulizi kati ya Haruna Mnyalukolo atakayezipiga na Hassan Kidebe, Mussa Hassan atapambana na Ibrahim Amandus.

